Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Akabidhi Sadaka ya Futari Dahalia ya Lumumba

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla akikabidhi sadaka ya futari kwa wanafunzi wa Dahalia wa Skuli ya Sekondari Lumumba Zanzibar .

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewataka walimu kuhakikisha wanazidisha jitihada na kutafuta mbinu mbali mbali za kufundishia ili kuhakikisha kiwango cha ufaulu kinaongezeka na kupata daraja la kwanza kwa watahiniwa wa kidato cha nne na cha sita kwa skuli zote za Zanzibar.

Ameyasema hayo kwakati wa kukabidhi ftari kwa wanafunzi wanaoishi Dahalia mbali mbali Kisiwani Unguja ikiwa na lengo la kuwapunguzia upatikanaji wa ftari hasa kwenye mwezi huu mtukufu wa ramadhani.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa elimu na hali halisi ya maisha ya dahalia wameona ipo haja ya kuftari pamoja na wanafunzi wanaoishi dahalia kwa kuwapatia ftari ambayo itawasaidia katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan hasa kwa vile wao wanakosa kujumuika na familia zao katika ftari.

Mhe. Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar  amesema Mkakati wa Serikali ni  kuendelea kuimarisha miundombinu ya elimu ili kuhakikisha inaondoa division zero kwa skuli zote za Zanzibar hivyo jitihada na utayari wa walimu katika kufundisha ndiko kutakakosaidia kutimiza adhma hio ilowekwa na Serikali kuu.

Mhe. Hemed amesema ufaulu mzuri kwa wanafunzi ni ule wa daraja la kwanza ndio jambo ambalo linapelekea Taifa kupata wataalamu wazuri wa sekata mbali mbali na kuondoa utegemezi wa wataalamu kutoka nchi jirani jambo ambalo hurejesha nyuma  maendeleo ya nchi.

Mhe Hemed amewaasa wanafunzi kuutumia vizuri muda wao kwa kujisomea na kuachana na yale yote ambayo yatakatisha malengo yao ambapo amewahakikishia kuwa Serikali itahakikisha kila mwaka bajeti ya Wizara ya Elimu inaongezeka hasa katika Kitengo cha Bodi ya Mikopo ya elimu ya juu ili kutoa fursa kwa wanafunzi watakaofanikiwa kujiunga na vyuo vikuu wanasoma pasipo na changamoto ya ada.

Sambamba na hayo amewataka wazizi na walezi kushirikiana na walimu na wanafunzi katika kuongeza ufaulu kwa wanafunzi jambo ambalo litapelekea  serikali kupata viongozi bora, ambao wameelimika na wenye maadili ya kazi kwa maslahi ya nchi na taifa kwa ujumla.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Lela Mohamed Mussa amemshukuru  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kuendelea kuwasaidia wanafunzi wanaoishi dahalia kwa kuwapatia ftari jambo ambalo linadhihirisha upendo walionao viongozi kwa wananchi wao.

Waziri Lela amesema walimu na wanafuzi wanatakiwa kuzithamini jitihada zinazofanywa na viongozi wakuu wa nchi kwa kuweka mkakati wa kutokomeza division zero na kupata ufaulu wa daraja la kwanza kwa wanafunzi wote wa kidato cha nne na kidato cha sita, hivyo ameiomba Serikali kuu kuendelea kuiongezea fedha bajeti bodi  ya mikopo ili kuweza wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu ndani na nje ya nchi.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi  wenzake wa skuli ya sekondari ya Donge  FATHIYA MACHU VUAI amemshukuru Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar kwa kuwatembelea na kuwaletea Ftari hio ambayo itaweza kuwasaidia hasa katika kipindi hichi cha kumalizia mwezi mtukufu wa ramadhan.

Aidha wamemuahidi Rais wa Zanzibar kuwa watafanya vizuri katika mitihani yao ya kidato cha nne na kupata Daraja la kwanza ili kuweza kuja kulisaidia Taifa kwa kuwa  na viongozi walio bora na wenye kueliimika.

Skuli zilizokabidhiwa ftari na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ni pamoja na Chuo cha Kiislam Mazizini, Skuli ya Sekondari ya Ufundi Mikunguni, Skuli ya Sekondari Lumumba, Skuli ya Sekondari Donge, Skuli ya Sekondari Mtule na Skuli ya Sekondari Hasnuu Makame Kizimkazi Unguja.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.