Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Huemed Suleiman Abdulla Ajumuika na Wananchi Katika Sala ya Ijumaa Msjid As Habqahfi Mwanakwerekwe na Kumtembelea Sheikh Suleiman

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla  amewataka waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi kwa ujumla  kuzidisha jitihada katika kutafuta elimu zote mbili katika kila pembe ya Dunia ili kuweza kufanya Ibada iliyokamilika sambamba na  kuweza kufanya biashara kwa uwelidi wa hali ya juu.

Alhajj Hemed ameyasema hayo alipokuwa akiwasalimia Waumini wa Masjid AS- HAB QAHFI  uliyopo MWANAKWEREKWE SOKONI  mara baada ya kumalizika  kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema kuwa suala la kutafuta elimu kwa muumini ni jambo la lazima kama ilivyoamrishwa katika kitabu kitukufu cha Qur – an ili kuweza kufanya jambo lolote kwa uweledi wa hali ya juu ikiwemo kufanya ibada na shuhuli nyengine za kijamii zenye kuleta maendeleo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali imeamua kuwawekea mazingira mazuri wafanya biashara wadogo wadogo kwa  kuwajengea masoko ya kisasa ikiwemo soko kuu la mwanakwerekwe ili kuwaondolea usumbufu waliokuwa wakiupata hapo awali, hivyo ni wajibu kwa wafanyabiashara kutafuta elimu ya biashara itakayowawezesha  kufanya biashara zao kitaalamu zaidi na kufikia malengo waliojiwekea.

Alhajj Hemed amesema kuwa dunia ya sasa kila kitu kinahitaji elimu katika utekelezaji wake hivyo inatulazimu kujiendeleza ili kuisaidia Serikali kuwa na wataalamu mbaliwa fani mbali mbali wakiwemo wafanya biashara.

Mhe. Hemed amesema kuwa biashara inapofanyika kitaalamu ndio inayompelekea mfanya biashara kupata faida ya halali na kuweza kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum kwa moyo wa huruma huku wakitarajia kupata radhi za Allah (S.W).

Sambamba na hayo Alhajj Hemed amewashukuru Watanzania wote pamoja na Wazanzibari kwa kuendelea kuiunga  mkono Serikali ya Awamu ya Nane (8)  inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj  Dkt. Hussein Ali Mwinyi  katika kutekeleza miradi yote ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara kuu na za ndani kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Mapema akitoa Khutba katika Sala ya Ijumaa, Maalim SHAILAB SALUM  BAHESH    amewataka waumini wa dini ya Kiislam na Wazanzibari kuacha tabia ya kulipiziana kisasi kwa jambo lolote lile pindi wanapokoseana  kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na maamrisho ya Dini ya kiislamu.

Amesema kuwa  dini ya kiislamu  imekuja na mfumo mzima wa maisha ya mwanadamu hivyo ni wajibu wa kila muumini kuufuata ili kuishi kwa kumtegemea M.Mungu kwa kila kitu huku akitarajia malipo kutoka kwa kila jambo analolifanya hapa duniani.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amefika nyumbani kwa Mfanyabiashara Sheikh Suleiman Ali Mbarak Fuoni Zanzibar kutoa mkono wa pole kwa familia kufuatia kifo cha baba mzazi wa mfanyabiashara huyo kilichotokea 15 Mei, 2024.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.