RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Viongozi wa Masjid Quba Mbweni Wilaya
ya Magharibi “B” Unguja Jijini Zanzibar, alipowasili katika viwanja vya msikiti
huo kwa ajili ya Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika leo 10-5-2024.
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein
Ali Mwinyi ameahidi kuchangia nguvu za uendeshaji wa Masjid Quba ili
kuongeza ari na hamasa kwa viongozi na waumini wanaoutumia msikiti huo.
Alhaji Rais Dk. Mwinyi amesifu uongozi wa msikiti
huo kwa weledi wao wa kutoa taaluma bure kwa vijana na waumini wa dini ya
kiislamu na kuwaahidi kuwaongezea nguvu za mahitaji ya msikiti huo.
Al hajj Dk. Mwinyi alitoa ahadi hiyo mara baada ya
ibada ya sala ya Ijumaa msikitini hapo, Mbweni Mkoa wa Mjini Magharibi.
“Maadam na mimi mmenieleza haya mnayoyafanya basi na
mimi nitakuchangieni ili tuzidi kuliendesha gurudumu hili” Aliahidi Al hajj Dk. Mwinyi.
Akizungumzia suala la kuwaombea dua viongozi wa
Serikali, Al hajj Dk. Mwinyi amewasihi waumini na viongozi wa msikiti huo
wasichoke kuwaombea dua viongozi wa nchi ili Mwenyezi Mungu azidi kuwapa wepesi
wa kutekeleza na kuzikamilisha ahadi walizoziahidi kwa wananchi.
Al hajj Dk. Mwinyi alisema, ahadi nyingi tayari
zimetekelezwa na kukamilishwa kwa wakati lakini bado zipo nyingi pia zinahitaji
kukamilishwa kwa mafanikio makubwa na kueleza maombi mema kutoka kwa wananchi kwenda
kwa viongozi wao, bado yanahitajika katika kufika malengo ya nchi iliyojiwekea na
kufanyakazi kwa uadilifu.
Mapema, akizungumza
kwenye ibada hiyo ya sala ya Ijumaa msikitini hapo, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti
Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume alisifu juhudi
za Alhaj Dk. Mwinyi kwa uweledi wake wa
kushirikiana na wananchi na waumini wa dini ya kiislamu kwenye ibada ya sala ya
Ijumaa kwa maeneo mbalimbali nchini kutokana na dhamira na nia yake njema kwa
watu wa Zanzibar.
Alisema, uongozi wa Al hajj Dk. Mwinyi ni juhudi
zake za kuwafikia wa watu wote pamoja na hudumia kwani ni kiongozi wa wote.
Akitoa hutba kabla ya
sala ya Ijumaa, Khatib wa sala hiyo Sheikh, Ali Masoud amewasihi waumini wa
dini ya Kiislam kuwaombea mema na kuwatii viongozi wa nchi, kwani kufanya hivyo
ni kulitakia heri na baraka taifa na watu wake.
Mara baada ya ibada ya Sala hiyo ya Ijumaa, Al hajj
Dk. Mwinyi aliwatembelea wazee, akiwemo Mbunge wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), jimbo la Amani, Mzee Hassan
Rajab, nyumbani kwake Kisauni “Wilaya ya Magharibi B” na Mjumbe wa Baraza la
Wazee kupitia Chama Cha CCM Kisiwandui, bibi Maryam Hengwa nyumbani kwake Kwa
Mchina, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Al hajj Dk. Mwinyi amekua na utaratibu wa jukumuika
pamoja na wananchi na waumini wa dini ya Kiislam kwenye ibada ya sala ya Ijumaa
kwa maeneo mbalimbali ya visiwa vya Zanzibar
kwa kufanikiwa kusali zaidi ya misikiti 170 ndani ya kipindi
cha miaka mitatu ya uongozi wake, pia Alhajj Dk. Mwinyi amefungua misikiti mipya zaidi ya 30 kwa maeneo
mbalimbali ya Unguja na Pemba pamoja na kuwatembelea wananchi, wazee na
wagonjwa hospitalini.
IDARA YA MAWASILINO,
IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment