Habari za Punde

Serikali Yawataka Wananchi Kufunga Kifaa cha Kuzuia Athari za Umeme Majumbani EME MAJUMBANI Lengo ni kujilinda na athari za umeme

Naibu waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga akijibu maswali ya Wabunge bungeni jijini Dodoma tarehe 13 Juni, 2024.


Lengo ni kujilinda na athari za umeme Kapinga ataja juhudi zinazofanywa na Serikali kuimarisha hali ya umeme Jimbo la Segerea

Asema usambazaji umeme vijijini unaendelea, vitongoji 4000 kupatiwa umeme 2024/2025

Naibu waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amewataka wananchi kuchukua hatua za  kufunga vifaa vya kuzuia athari za umeme kwenye nyumba (circuit breaker) ili kujilinda na majanga yanayoweza kutokea pale umeme unapokuwa mwingi au kupungua.

 Mhe. Kapinga amesema hayo leo Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Segerea, Mhe. Bonnah Kamoli aliyetaka  kufahamu mpango wa Serikali kwa wananchi wanaopata hasara kutokana na kukatika kwa umeme au nyumba kuungua.

Kapinga amesema uchunguzi unapothibitisha kuwa tatizo la kuungua kwa nyumba limesababishwa na TANESCO, Serikali inachukua hatua kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Akizungumzia hali ya umeme katika Jimbo la Segerea, Kapinga ameeleza kuwa changamoto ya kukatika kwa umeme katika jimbo hilo ilitokana na kuzidiwa kwa kituo cha kupokea na kusambaza umeme cha Gongo la Mboto ambacho kinapeleka umeme Segerea.

Ametanabaisha kuwa, hali ya umeme Segerea sasa imeimarika kutokana na Serikali kuchukua hatua ambapo wananchi wengine kutoka Jimbo la Segerea wanapata umeme kutoka kituo cha kupokea na kusambaza umeme cha Kipawa.

Ameongeza kuwa Serikali kupitia TANESCO pia  inatekeleza miradi ya upanuzi wa kituo cha Gongo la Mboto na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Ubungo hadi Tabata ili kuimarisha zaidi upatikanaji wa umeme.

 Katika hatua nyingine, akijibu swali la Mbunge wa Mpanda Vijijini, Mhe. Selemani Kakoso aliyetaka kujua mpango wa Serikali kupeleka umeme kwenye maeneo muhimu katika eneo la Mishamo hasa kwenye Soko na Kituo cha Afya,   Kapinga amesema ni mkakati wa Serikali kuhakikisha umeme unakwenda kila kijiji na miradi  ya usambazaji umeme inaendelea ambapo  kwa mwaka wa fedha 2024/25 vitongoji 4,000 vitapata umeme.

Akijibu swali la Mbunge wa Namtumbo, Mhe. Vita Kawawa aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali kuimarisha umeme kwenye vijiji vya Namtumbo vinavyopata umeme mdogo, Kapinga amesema Serikali tayari inao mpango wa kuongeza nguvu umeme kwenye maeneo ya vijijini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.