Habari za Punde

Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya Atembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke

 

Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Hamad Nyembea, amefanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke(TRRH) kwa lengo la kuona utoaji huduma katika hospitali hiyo. Katika ziara hiyo Dkt. Nyembea ametembelea wodi ya usafishaji damu, wodi ya watoto wachanga pamoja na wodi ya kina mama waliyojifungua kwa njia ya kawaida.

Dkt. Nyembea amepata nafasi ya kuzungumza na uongozi wa hospitali hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora wa huduma. Amewataka viongozi wa idara na vitengo mbalimbali kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa watumishi na wagonjwa kuhusu dhana ya ubora wa huduma, kwani watumishi na viongozi wa eneo husika ndio wanaowajibika na muonekano wa hospitali.

Aidha, Dkt. Nyembea ameeleza kuwa huduma zinazotolewa zinapaswa kumlenga mgonjwa, kumuelimisha kuhusu hali yake ya kiafya na aina ya matibabu anayopokea ili aweze kuelewa na kushiriki kikamilifu katika matibabu yake. Pia aliwasihi mabingwa wa afya kuhakikisha wanatoa huduma na majibu kulingana na miongozo na taratibu za kisayansi kwa kutumia viwango vilivyowekwa na Wizara ya Afya pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke (TRRH), Dkt.Joseph Kimaro, ameeleza kuwa hospitali inaendelea kuboresha huduma zake na kusema uanzishwaji wa huduma ya usafishaji damu (dialysis) hospitalini hapo, ni huduma muhimu sana kwa eneo la Temeke. amefafanua kuwa hospitali hiyo inahudumia wilaya tatu: Kigamboni, Temeke, na Mkuranga, na ni hospitali pekee ya serikali katika eneo hilo inayotoa huduma ya usafishaji damu.

Dkt. Kimaro pia ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu, hospitali hiyo imefanikisha upatikanaji wa dawa kwa asilimia 98 kwa bidhaa 500. Mafanikio haya yanatokana na jitihada kubwa za timu ya uendeshaji wa huduma za afya(RRHMT) hospitalini hapo, ambapo asilimia 80 ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba unafanywa na fedha za uchangiaji wa huduma. 

Dkt. Kimaro ametoa shukrani zake kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika hospitali za Tanzania, hususan Temeke, kupitia vifaa tiba vya kisasa na wataalamu wa mionzi. Pia amemshukuru Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu kwa kusimamia wizara na watumishi wake, na kuhakikisha miongozo na sera za wizara zinafuatwa ipasavyo.No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.