Habari za Punde

WANANCHI WAHIMIZWA KUJITOKEZA KUPIMA UGONJWA WA HOMA YA INI, HAUNA DALILI ZA WAZI

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WAKATI Dunia inaadhimisha Siku ya Ini, wananchi wametakiwa kujitokeza kwenda kupima ugonjwa wa homa ya ini kwakuwa hauna dalili za wazi na athari zake hupelekea maambukizi ya saratani pamoja na kifo.

Wito huo umetolewa na Dkt. Kasanga Bashiru wa hospitali ya Siha Poly Clinic ya jijini Tanga ambapo amebainisha kwamba ugonjwa huo dalili zake hazitofautiani sana na magonjwa mengine kiasi ambacho watu wamekuwa hawakumbuki kupima kuhusiana nao.

"Kwa hatua zile za awali, asilimia kubwa ya watu wanaopata huu ugonjwa huwa zile za moja kwa moja isipokuwa kwa asilimia ndogo ndiyo wanapaita dalili ambazo ni kali, na zile dalili za moja kwa namba zinafanana na magonjwa mengine, hivyo watu wanapuuzia kwenda kupima,

"Lakini kwa zile dalili ambazo ni viashiria vya moja kwa moja, kwanza ni umanjano kwenye macho, mkojo na hata kwenye ngozi lakini pia maumivu ya tumbo ambapo hupelekea kuvimba" amesema Bashiru.

Aidha Dkt. Bashiru amefafanua madhara yanayotokana na homa ya ini kuwa ni pamoja na ini kushindwa kufanya kazi yake lakini pia mwisho wake ni kupelekea kifo.

"Endapo mgonjwa arltachelewa kubaini ugonjwa wake, athari za ugonjwa huu ni kufeli kwa ini, lakini pia kupata saratani ya ini kwa urahisi, na hatima kabisa ni mgonjwa kupotezea maisha" amesisitiza.

Naye Awadhi Abdul amesema kuwa hospitali inahakikisha jamii inapata uelewa kuhusu magonjwa mbalimbali wamekuwa wakiwapatia ushauri na huduma na katika kuadhimisha siku hiyo wanatoa vipimo vya ugonjwa huo bure.

"Kama Siha Poly Clinic mbali na kutoa huduma za kimatibabu, pia tunao Madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali ikiwemo moyo, mifupa, meno na mengineyo, lakini pia tunazo machine za vipimo kama Cityscan pamoja na MRI na huduma za vipimo hivi zinapatikana kwa garama nafuu" amesema.

Vilevile Abdul amesema muitikio wa watu unaridhisha na wana imani lengo la kupambana na ugonjwa huo litafanikiwa, lakini pia jamii itakuwa imepata uelewa wa jinsi ya kujitunza ili wasipate maambukizi ya ugonjwa huo.

Baadhi ya wagonjwa waliofika kupata huduma za vipimo katika hospitali hiyo wamesema wamepata ari ya kwenda kupima ili kujua afya zao ambapo wameeleza kuwa wameona umuhimu wa kufanya hivyo.

"Ni vema tukajiwahi, kupima afya ni muhimu sana ili kujua kama umepata maambukizi uanze kupata tiba na vilevile kama umenusurika uweze kupata kinga, niliposikia hospitalini hapa wanatoa huduma ya kupima ugonjwa huu bure na mimi nikiamua kuja" amesema Ignance Mponji.

"Niwashauri tu wananchi wenzangu kuja kupima ili wajue wako upande wa kinga au tiba, lakini pia ukiwahi kujua ugonjwa ni rahisi kupata matibabu mapema kuliko kukaa na ugonjwa na baadae kuleta madhara makubwa zaidi" amesisitiza Edom Mwakimwagile.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.