Habari za Punde

Mhe Othman afanya ziara pangatupu kuangalia uharibifu wa mazingira

 


MKOA WA KUSINI UNGUJA,

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amezitaka mamlaka zinazosimamia raslimali ya ardhi    kuchukua hatua sahihi na pia kuwasaidia wananchi kushirikiana kurejesha hali ya maeneo yaliyoharibika kwa kuchimbwa mchanga ili ardhi hiyo iweze kuzalisha kwa tija na kuwa na manufaa zaidi.

Mhe. Othman ameyasema hayo alipotembelea eneo la Pangatupu Wilaya ya Kaskazini B Unguja lilioharibika vibaya kwa kuchimbwa mchanga ambalo lipo katika Mpango wa Taifa wa Kuirithisha Zanzibar kuwa ya kijani unaotarajiwa kuwa shirikishi kwa taasisi na makundi yote ndani ya jamii .

Amesema kwamba pamoja na mahitaji ya matumizi ya mchanga yaliyipo ambayo kimsingi hayawezi kusita,  lakini kuna haja kubwa ya kuwepo usimamizi bora wa maeneo hayo kwa kuwa na matumizi sahihi  bila kuendelea kuharibika kwa maeneo yaliyoruhusiwa kuchimbwa mchanga.

Amefahamisha kwamba ni muhimu kuwepo na utaratibu wa kuyatumia maeneo yaliyoriuhusiwa kisheria na kabla ya kuhamia kwenye maeneo mengine kuhakikisha  yanarekebishwa na kurejeshwa katika hali yauasili  ili pia yaendelea kutumika kwa uzalishaji wa kilimo na mazao mengine ikiwemo upandani wa minazi, miti ya matunda na aina nyenginezo.

Amesema hali ilivyo sasa inaonesha athari ni kubwa sana jambo ambalo ni funzo kubwa kwa nchi katika kuhakikisha kwamba pale eneo linapotumika kuchimbwa mchanga kunakuwepo na utaratibu bora ambao hautaharibu mazingira ya eneo husika kama ilivyo sasa ili kuepuka  athari kubwa kwenye ardhi mbali mbali za Zanzibar zilizochimbwa mchanga.

Amesema kwamba iwapo kutakuwa na utaratibu wa aina hiyo na kuwa endelevu kutaisaidia sana Zanzibar kuendelea kuwa ya kijani jambo ambalo hivi sasa linaonekana kupotea na ndio maana serikali imekuwa na mpango huo wa kuirithisha Zanzibar kuwa ya kijani.

Amefahamisha kwamba ni busara kutengeneza mpango sahihi wa kuyafufua maneo yote yaliyoharibika kwa kuwasaidia wananchi pamoja na kuwaelimisha kuilinda ardhi  ndogo iliyopo na kuitumia neema hiyo kwa tija kubwa katika uzalishaji wa mazao mbali mbali ikiwemo upandaji wa minazi inayoweza kuzalisha vyema kuliko ilivyo sasa.

Wakati huo huo, Mhe. Makamu amewataka wataalamu wa Kilimo wanaosimamia uzalishaji wa miche ya miti ya chakula na matunda  Zanzibar kuhakikisha kwamba wanatumia utaalamu wa kileo ikiwemo tekenolojia ya kisasa ili kuwawezesha vijana kuvutika na kuwa na mwamko mkubwa zaidi wa uzalishaji wa mazao kupitia teknlojia hiyo.

Amefahamisha kwamba nchi mbali mbali duniani zilizopata mafanikio katika maendeleo ya kilimo zimejitahidi kuitumia vyema kwa pamoja sayansi na teknolojia  pamoja na maarifa ya Sanaa za kisasa katika uzalishaji wakileo unaoleta mafanikio ya haraka.

Amesema hali hiyo inawezakana pia kutumika Zanzibar lakini muonekano wa kituo cha uatikaji mbegu na uzalishaji wa miche kilichopo Mwanyanya wilaya ya Magharib A Unguja haiakisi mahitaji ya kisasa na kuwapa matumaini wananchi kwa kujengea ushawishi vijana wa Zanzibar  kupenda kushiriki katika kazi za kilimo cha aina mbali mbali.

Amesema kwamba kunahaja na inawezekana kutumia utaratibu wa tetknolojia ya kisasa kufanya mageuzi makubwa kwenye sekata ya kilimo cha kuotesha miti ya matunda kuwa na miti midogo inayoweza kuzalisha matunda mengi na kuleta tija kubwa kiuchumi kwa wananchi.

Mhe. Othman katika ziara hiyo ametembelea eneo lilochimbwa mchanga la Pangatupu Kaskazini B, eneo linaloteshwa  miche ya mikoko Mtowapwani Fungurefu Kaskazini A, eneo lililopandwa miti la Chaani Masingini pamoja na Nasari ya uatikaji wa miche ya miti ya matunda na mazao mbali mbali ya Kilimo huko Mwanyanya wilaya ya Magharib A.


 

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.