Habari za Punde

Wanakijiji wa Mlimboni -Matemwe waomba kuongezewa vyumba vya madarasa


 NA FAUZIA MUSAA

WANANCHI  wa kijiji cha Kijini Mlimboni -Matemwe kilichopo Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja wameiomba Serikali na wadau mbali mbali kuwasaidia kuongeza  vyumba vya madarasa katika  skuli ya maandalizi na msingi  Mlimboni ili kuondakana na  uhaba wa vyumba vya kusomea katika  skuli hiyo.

Wito huo umetolewa na wakaazi wa kijiji hicho wakati wa  ufunguzi wa madarasa mawili yaliyofunguliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Othman Ali Maulid  .

Nadhar Mtwana Khamis mkaazi wa Kijini Mlimboni akizungumza na mwandishi wa habari hii  alisema hatua hiyo itasaidia wanafunzi kuwa na mazingira rafiki ya kujisomea na kuongeza ufahamu hali aliyoitaja kusaidia kuwaandaa kuleta matokeo mazuri katika mitahani yao ya Taifa.

 “kutokana na kuwa na madarasa machache skulini hapa, wanafunzi wa madarasa mawili huchanganywa katika chumba kimoja kwa wakati mmoja, hali hii inasababisha mrundikano unaohataraisha afya za watoto wetu.” Alieleza mwana kijiji huyo

Hata hivyo aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa namna inavyoshirikiana vyema na wadau mbalimbali katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Akizungumza na walimu, wazazi na wafunzi wa skuli hiyo mara baada ya kufungua madarasa hayo Mkuu Wa Wilaya  Kaskazini  'A' Othman Ali Maulid  alisema, Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwasogezea huduma wananchi wake hasa wa vijijini ili  kuondokana na chaangamoto zinazorudisha nyuma  maendeleo yao.

Alieleza kuwa  kufunguliwa kwa madarasa hayo kunaenda sambamba na dhamira ya Serekali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Husen Ali Mwinyi inayolenga kupunguza mrundikano wa wanafunzi maskulini ili  kusoma katika mazingira yaliyo bora zaidi.

Mkuu huyo aliishukuru kampuni ya Andbeyond iliopo kisiwa kidogo Cha Mnemba huko Matemwe Mkoa Kaskazini Unguja na Shirika linalojishughulisha na Shuhuli za Maendeleo ya jamii Wild Impact kwa kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo ya  sekta ya elimu na kuahidi  kukabidhi mifuko 15 ya saruji  ili kukamilisha sehemu ndogo ndogo zilizobakia ikiwa ni kuunga mkono juhudi z aupatikanaji wa elimu katika kijiji hicho.

Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo, Makame Mwiga Kidawa alisema, skuli hiyo yenye  na  wanafunzi 276 wakiwemo wanaume 27  na wanawake 33 wa maandalizi, pamoja na wanaume 101 na wanawake 155 wa msingi  awali ilikuwa na vyumba vine, hivyo kupatikana kwa vyumba  viwili  kutapunguza idadi ya wanafunzi katika chumba kimoja.

 “ kukamilika kwa vyumba hivi  tumefarijika sana kwani hapo awali baadhi ya wanafunzi wetu  walisoma nje na wengine kujazana katika chumba kimoja .” Alisema mwalimu huyo.

Mbali na hayo  aliiomba Serikali kulipa mkazo suala la kuongeza matundu ya vyoo katika skuli hiyo ili kulinda afya za wanafunzi kwani kwa sasa skuli hiyo ina matundu manne ya vyoo ambayo hayatoshelezi kwa wawanfunzi waliopo hapo.

Naye  msimamizi wa miradi ya Kampuni ya Andbeyond, Bakari Jaha Muhidini alisema wataendelea kuiunga mkono Serekali katika  mambo mbalimbali  ya jamii hasa sekta ya elimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.