Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman - Kumuwakilisha Rais wa Zanzibar Mhe.Hussein Mwinyi Siku ya Chakula Duniani -- PEMBA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akitembelea mabanda ya wakulima katika  maonesho ya siku ya chakula Duniani yaliyofanyika katika Kiwanja cha Chamanangwe Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar na Mipango mikakati mbali mbali inaendelea kuwawekea mazingira wezeshi wananchi ya kuekeza katika kilimo chenye tija kwa chakula na biashara ambacho kitakuza  kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussen Ali Mwinyi katika hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya Siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika katika Kiwanja cha Chamanangwe Mkoa wa kaskazini Pemba.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo imeandaa mpango wa mageuzi ya sekta ya kilimo utakaobadilisha kilimo cha Zanzibar kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha biashara kitakacho wahusisha zaidi vijana na wanawake.

Mhe. Hemed amefahamisha kuwa Serikali itaendelea na uimarishaji wa zao la karafuu na nazi kwa kuzalisha miche bora ya minazi na makirafuu na kuigawa bure kwa wakulima pamoja na kutoa pembejeo za kilimo kwa utaratibu wa ruzuku pamoja na kuhamasisha wakulima kujikita katika kilimo hai ili kuhakikisha usalama wa chakula, afya ya udongo na kulinda mazingira.

Aidha, Makamu wa Pili wa Rais amesema ili kukuza biashara katika maeneo ya visiwa  ni lazima kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji  ikiwemo barabara, Bandari na viwanja vya ndege ambavyo vitachochea kukuwa kwa biashara na kuongeza wigo wa masoko ya ndani na nje ya nchi kwa biadhaa ambazo zinazalishwa na mkulima .

Sambamba  na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametoa wito kwa Wizara ya Kilimo kuweka utaratibu mzuri wa upatikanaji wa huduma ili wakulima na wafugaji waweze kulima na kufuga kisasa na kibishara pamoja na Wizara kuweka utaratibu nzuri wa uwekaji wa takwimu za makundi yote yanayojishughulisha na kazi za kilimo na Mifugo.

Nae Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Mhe. Shamata Shaame Khamis amesema maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanalenga kuwaongezea maarifa na ujuzi wakulima na wafugaji kwa kulima kilimo hai chenye tija na cha biashara kitakachosaidia kuinua kipato cha wakulima na wafugaji nchini.

Waziri Shamata amesema Mpango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuleta mageuzi makubwa katika Sekta ya kilimo kwa kuboresha miundombinu ya kilimo na Ufugaji kwa kuwashajihisha wananchi kulima kilimo chenye tija ili kuongeza uzalishaji wa chakula kwa matumizi na biashara.

Mhe. Shamata amesema kuwa Wizara imejipanga kutoa elimu ya Kilimo na Ufugaji kwa wakulima na wafugaji Unguja na Pemba ili kutanua wigo wa kulima na kufuga kisasa kwa uzalishaji wa uhakika na wenye tija kwa maslahi yao binafsi na Taifa kwa ujumla.

Aidha Mhe. Shamata ameiomba Serikali kujengewa barabara za lami katika eneo lote la maonesho ili kurahisisha utowaji na upatikanaji wa huduma katika maeneo hayo jambo litakalotoa hamasa kwa wakulima na wafugaji kuendelea kushiriki kwa wingi katika maonesho hayo ambayo hufanyika kila ifikapo tarehe 10 mwezi wa 10 ya kila mwaka.

Akitoa taafisa juu ya maonesho hayo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo ALI KHAMIS JUMA amesema Wizara ya Kilimo itaendela kutafuta mbinu bora na za kisasa zitazosaidia katika kuzalisha chakula bora na salama kwa wingi na nchenye tija kwa Wananchi wa Zanzibar na Taifa kwa ujumla.

Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya kilimo itayaendeleza na kuyaboresha maonesho hayo ya siku ya chakula duniani ili yaendelee kutoa hamasa  kwa wakulima, wafugaji na kuziomba Taasisi mbali mbali kuendelea kushiriki katika maonesho hayo yenye adhma ya kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Kilimo nchini.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametembelea mabanda mbali mbali  ya maonesho ya wakulima walioshiriki maonesho hayo.

Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR)

Leo tarehe … 10 / 10 / 2024.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.