NA FAUZIA MUSSA.
RAIS wa Kamati ya Olimpic Tanzania (TOC), Gulam Rashid Abdalla, amewataka viongozi wa vyama vya michezo kuangalia katiba zao na ikiwezekana kubadilisha baadhi ya vipengele vinavyoonekana kukwamisha maendeleo ya vyama vyao.
Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya utawala kwa viongozi wa vyama vya michezo yanayofanyika ukumbi wa Maktaba kuu Maisara Mjini unguja.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuwa na miongozo ya kisasa itakayosaidia kuleta mafanikio na kuwafikisha walipokusudia na kuwakumbusha kuzijua na kuzifuata katiba hizo kwani kutozifahamu kunachangia viongozi hao kutoafanya vizuri katika vyama vyao nakushindwa kuiendeleza michezo Nchini.
“ikiwa bado vyama hivi vinatumia Katiba iliyopitwa na wakati havitafikia malengo niwashauri kuziangalia Katiba na tusione tabu kuzifanya marekebisho pale tunapohisi zinaturudisha nyuma” alisisitiza
Alisema Lengo la mafunzo hayo ni kuwaunganisha na kuwajenga viongozi kuweza kuleta mabadiliko chanya kupitia michezo na kuwaomba wana kozi hiyo kuwa huru na kueleza yanayowakwaza ili kupatiwa ufumbuzi na kuona kuwa wanafikia malengo waliyojiwekea.
Alieleza kuwa takwimu zinaonesha kuwa vyama visivyozidi asilimia 10 ndio vinavyoshiriki olympic kutokana na vyama vingi kutowezeshwa kiutawala na kushindwa kuwafanya wanamichezo wao kushiriki olympic na kushinda .
Mbali na hayo aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa watulivu na wasikuvu katika mafunzo hayo ili malengo yaweze kufikiwa .
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo Nassra Juma Mohammed alisema mafunzo hayo ni fursa Kwa viongozi wa vyama vya michezo kupata uwezo wa kutengeneza mpangokazi utakaowaongoza kuwagundua, kuwalea, kuwaendeleza na kuwatengeneza wachezaji kitaalamu na kuweza kuleta medali katika vyama vyao.
Nasra ambae pia ni mjumbe wa kamati tendaji TOC alisema pia hali hiyo itasaidia kufikia malengo na dhamira chanya ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ya kuwafanya wachezaji wa Zanibar kufanya vizuri katika michezo ya ndani na nje ya nchi.
Alisema wakati umefika kwa viongozi hao kujikwamua na kuonesha changamoto zinazowakabili ili kuendana na kasi ya mageuzi ya sekta ya michezo.
Naye Mkufunzi mkuu katika mafunzo hayo, Henry Tandau, aliahidi kuwa mafunzo yatakua jumuishi ambapo wakufunzi watawasikiliza walengwa na kuegemea katika maeneo yenye changamoto na kuzitafutia ufumbuzi na kusema kuwa mafunzo hayo yataendeshwa kivitendo zaidi.
alifahamisha kuwa wadhamini wakuu wa mafunzo hayo ni kamati ya Olimpic hivyo pia mafunzo hayo yatalenga kuutambulisha mfumo wa kamati hiyo, kujua stadi za michezo na majukumu muhimu ya viongozi pamoja na vyombo vikuu vinoongoza vyama hivyo.
"michezo ni tasnia Pana na vyama vingi havina Mipango na kuamini michezo ni kushindana Pekee mafunzo haya yatasaidia kutoa fursa ya kudadavua maeneo magumu ya tasnia hiyo ikiwemo masoko, utengenezaji wa mipango na namna ya kuwafikia wadhamini ili kupata wanachokitarajia."
Aidha mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa michezo ya baharini na ufukweni hali itakayosaidia kwenda sambamba na Dhana ya Uchumi wa buluu.
jumla ya viongozi 30 wa vyama vya michezo watanufaika na mafunzo hayo wakiwemo viongozi wa chama cha kuogelea, ZAWEA, shirikisho la mpira wa miguu Zanzibar, chama cha netball, shirikisho la riadha, na mpira wa mikono handball.
No comments:
Post a Comment