Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla - Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano Mkoani Mtwara

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akipokea zawadi ya picha ya Mfanano wa Bandari ya Mkoa wa Mtwara wakati alipotembelea banda la maonesho la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, Bandari ya Mtwara katika Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika Viwanja vya Saba Saba Mkoani Mtwara.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema kuelekea Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mafanikio makubwa yamepatikana kwa pande zote mbili za Muungano ikiwemo kujenga misingi imara inayodumisha umoja, amani, mshikamano na utulivu.

Ameyasema hayo katika hafla ya maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika katika viwanja vya saba saba  Mkoani  Mtwara.

Amesema kuwepo kwa Amani, mshikamano na utulivu nchini kumechochea kukuwa kwa maendeleo katika nyanja zote kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia ambapo amewataka wananchi wa Mkoa wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla kushiriki katika shughuli zote za ulinzi na usalama ili kuhakikisha Mkoa huo na Taifa kwa ujumla  linaendela kuwa na Amani na Utulivu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema shughuli za kiuchumi kama vile viwanda, biashara na kilimo zimeongezeka na kuchochea kukua kwa harakati za usafirishaji wa bidhaa kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar na Zanzibar kupata fursa ya kupeleka bidhaa Tanzania Bara jambo linaloongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema serikali zote mbili hazitomvumilia mtu yoyote atakae onesha viashiria vya uvunjifu wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambo ndio tunu ya nchi nyingi duniani na wenye manufaa makubwa kwa wananchi wote wa Tanzania.Aidha, Mhe.Hemed amefahamisha kuwa shilingi Bilioni 83.65 zimetumika katia ujenzi wa miundombinu mbali mbali Mkoani Mtwara ikiwemo shule mpaya 22 na madarasa 941, matundu ya vyoo 1,175 , vyumba vya maabara 102, Mabweni 9 na nyumba za waalimu 17.

Sambamba na hayo Serikali imetumia shilingi bilioni 157 kwa ajili ya Uboreshaji wa Bandari ya Mtwara ambayo kwa sasa ina uwezo wa kuhudumia shehena ya Tani Milioni 1.9 ambapo fursa za ajira zimeongezeka kwa wakazi wa Mtwara na pia kuongezeka mapato Serikalini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewasisitiza wananchi wa Mtwara kuitumia haki yao ya kikatiba ya kushiriki katika uchaguzi Mkuu ifikapo mwezi Oktoba 2025 kwa kupiga kura na kwa wenye sifa za kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi kujitokeza kugombea nafasi hizo ili Taifa liweze kupata viongozi bora watakaoshirikiana nao katika kuleta maendeleo katika maeneo yao.

Akizungumzia suala la Afya, Mhe Hemed amesema Serikali imeimarisha na kuboresha huduma za afya Mkoani humo ikiweo miundombinu, ununuzi wa vifaa tiba na vitendanishi(reagents) hivyo amewataka mama wajawazito kuhudhuria kliniki kwa wkaati na kujifungulia kwenye vituo vya afya ili kuepuka vifo vya mama na mtoto vinavyoweza kutokea kutokana na kukosa huduma za kitaalamu kwenye jamii.

Amewakumbusha wananchi wa Mtwara kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia pamoja na kushiriki katika shughuli za uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti, usafi wa mazingira na uhifadhi wa fukwe jambo ambalo litasaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanal Patrik Kenani Sawala amesema katika kipindi cha miaka 61 ya Muungano Mkoa wa Mtwara umepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na kuwepo kwa Amani, Umoja na Mshikamano ulipo nchini.

Kanal Sawala amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewekeza  fedha  nyingi katika ujenzi na ukarabati wa miradi mbali mbali ya maendeleo Mkoani Mtwara ikiwemo miradi ya Afya, Elimu, Bandari,  Barabara, maji safi na salama, vyuo vya Veta pamoja na kuimarika kwa sekta ya kilimo ambayo imesaidia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao mbali mbali ikiwemo zao la Korosho linalolimwa kwa wingi Mkoani humo.

Akitoa salamu za Chama cha Mapinduzi Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara Komredo Mwalimu Mussa Said Nyengedi amesema licha ya baadhi ya watu kuutia dosari  Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lakini  uko Imara ndani ya Miaka 61 ambao umeleta mafanikio makubwa kwa pande mbili za Muungano.

Nyengedi amesema Muungano wa Tanzania ndio nguvu ya Umoja, mshikamano na Amani iliyopo nchini hivyo amewaomba Watanzania kuendelea kuulinda Muungano kwa nguvu zote na kutokusiliza maneno ya wasioitakia mema Tanzania .

Amewasisitiza wananchi wa Mtwara wakati wa uchaguzi  utakapofika kuhakikisha wanawapigia kura za ndio wagombea wa Chama cha Mapinduzi wa ngazi zote na kuwachagua kwa kishindo Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt. Hussein Mwinyi ili waendelee kuliongoza Taifa la Tanzania kwa mafanikio makubwa zaidi.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla ametembelea mabanda ya Maonesho kwa taasisi za kiserikali na binafsi na kujionea shughuli mbali mbali zinazofanywa na taasisi hizo zilizopo mkoani humo.

Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR ) leo tarehe 25 / 05 / 2025






No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.