Habari za Punde

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR- KUKUTANA NA WALIMU WA MADRASA WANAWAKE- JIMBO LA KIWANI

Mgombea wa Uwakilishi Jimbo la Kiwani ndugu Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na kuomba kura kwa walimu wanawake wa madrasa waliomo katika kijiji cha Mwambe Kiunga Shehia ya Mwambe Jimbo la Kiwani.

Mgombea wa Uwakilishi Jimbo la Kiwani ndugu Hemed Suleiman Abdulla amewata walimu wa madrasa wanawake kuendelea kuekeza katika mambo ya kheri hasa katika kuwafundisha vijana kumtambua Mola wao.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na kuomba kura kwa walimu wanawake wanaofundisha madrasa pamoja na wanamadrasa  waliomo ndani ya Jimbo la kiwani huko katika uwanja wa Mwambe Kiunga.

Amesema akiwa mwakilishi wa Jimbo la Kiwani kwa kushirikiana na wenzake atahakikisha analisimamia na kulipa kipaombele kikubwa suala la kuhifadhisha qur-an ili liweze kuwa jimbo la kwanza kwenye majimbo yote katika masuala mazima ya kuhifadhisha qur-an.

Ndugu.Hemed amasema atahakikisha anaimarisha na kuzirekebisha madrasa zote 83 zilizomo jimboni humo kwa kuweka miundombinu ya kisasa ndani ya madrasa hizo ili kuweka mazingira mazuri ya kukusoma kitabu kitakatifu cha Qur-an.

Amewaahidi wanamadrsa hao kuwajengea jengo kubwa la kisasa litakakalotumika kwa ajili ya harakati za madrasa zote za wanawake waliomo katika jimbo pamoja na kuwapatia vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kukuza na kuendeleza harakati za kidini.

Amesema ili kuendeleza vyema harakati za mambo ya kheri atahakikisha anatafuta walimu wenye sifa ili kuwafundisha wanamadrasa hao kwa lengo la kuwapatia taaluma watakayoitumia katika kuendelezana wenyewe kwa wenyewe kupitia madrasa zao.

Mhe. Hemed amewataka wakinamama hao kuwasimamia watoto wao waweze kupata elimu ya dini na dunia ambazo zitawajenga katika kuishi maisha ya kumtambua Mola wao na kuishi kwa imani na hofu ya Allah.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amesema atahakikisha anawawezesha wanawake hao kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba, vitendea kazi, walimu wa kuwafundisha namna bora ya kufanya shughuli zao pamoja na kuwatafutia masoko ya kuuzia bidhaa zao ndani na nje ya nchi.

Amesema mara baada ya kuchaguliwa kuwa mwakilishi wa Jimbo hilo kwa kushirikiana na viongozi wenzake watahakikisha suala la changamoto ya maji na changamoto nyengine ndani ya jimbo wanaahidi kuzishughulikia pamoja na kuhakikisha miradi mbali mbali ya maendeleo inaendelea kujengwa jimboni humo.

Wakizungumza kwa niaba ya waalimu wenzao wa madrasa  Amira Sabila Salum Hamad na Ukhty Maryam Juma Khamis wamewaomba viongozi hao kuwasaidia katika kuzifanyia ukarabati madrasa ambazo ni chakavu lakini pia kulimalizia ujenzi jengo la ZAWIYATULKADIRIA lililopo katika kijiji cha Mapungwe ambalo hutumika kwa shughuli mbali mbali za dini ya kiislam.

Wameomba kuangaliwa kwa ukaribu walimu wa wanawake wa madrasa kwa kupatiwa mitaji ya kujiendeleza katika shughuli zao mbali mbali za kijamii ili kuweza kukifundisha kitabu cha Qur-an kwa utulivu mkubwa.

Wanamadrasa hao wameahidi kuhamasishana kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo Oktoba 29 kwa kuwachagua viongozi wa Chama cha Mapinduzi ili waendelee kuwaletea maendeleo zaidi jimboni humo.

Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe 18 / 10 / 2025

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.