KIKWETE AITAKA WHI KUBORESHA MFUMO WA KIDIJITALI KUVUTIA UWEKEZAJI MPANA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete akizungumza na watumishi wa Housing Investment (WHI) wakati wa ziara yake ya utambulisho ofisini hapo leo Novemba 27, 2025 jijini Dar es Salaam.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete ameitaka Watumishi Housing Investment (WHI) kuendeleza mfumo wa kidijitali wa kisasa na rafiki kwa mtumiaji ili kuchochea ushiriki mkubwa wa uwekezaji kutoka sekta binafsi, sambamba na mpango mkubwa wa makazi unaowawezesha watumishi wa umma kununua nyumba kwa hadi asilimia 18 tu ya thamani ya soko.

Kikwete ametoa wito huo leo Novemba 27,2025 wakati wa ziara yake ya utambulisho katika ofisi za WHI jijini Dar es Salaam,nakusisitiza umuhimu wa kuunganisha huduma kwa watumishi wa umma kupitia mfumo wa e-Wekeza na kupeleka ubunifu huo katika sekta binafsi hususan kwa vijana wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi.

Katika hatua nyingine amesifu mafanikio ya mpango unaoendeshwa na mfuko wa pamoja wa uwekezaji wenye thamani ya Sh bilioni 49, ukiwa na lengo la kufikia Sh bilioni 54, uliobuniwa kuwawezesha watumishi wa umma na wananchi wa kawaida kujenga maisha yao kupitia uwekezaji mdogo unaoendeka, ambapo mfuko huo ndio unaochochea mradi wa “B340” unaojenga nyumba katika maeneo teule yenye huduma muhimu kama shule na vituo vya afya. Awamu ya kwanza ya nyumba 221 inatarajiwa kujengwa mwaka huu katika mikoa ya Dodoma, Lindi, Kigoma na Mbeya.

“Ikiwa mmeweza kuunganisha huduma zenu na ESS kupitia e-Wekeza kwa watumishi wa umma, basi mnapaswa kufanya hivyo hivyo kwa sekta binafsi, hasa kwa vijana wanaojiajiri,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa WHI, Sephania Solomon amesema kuwa mfuko unaendelea kukua ambapo wanachama hai awemefikia watu 11,437 na uwekezaji umefikia Sh bilioni 49.4, huku akisisitiza kuwa WHI inaendelea kupanua wigo wake wa kufikia Watanzania wengi zaidi nchini.

Kikwete amesema kuwa mfumo ulio rahisi kutumia na wenye upatikanaji mpana, ukiandaliwa kwa kushirikiana na e-GA, utawezesha Watanzania wote kuwekeza bila kujali aina ya ajira zao, akisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia za kisasa zinazofuta uhitaji wa kufika ofisini.

“Mnaweza kushirikiana na e-GA kuanzisha mfumo ambao hauhitaji mwekezaji kufika ofisini. Huo mfumo wa kufanya mambo umepitwa na wakati. Lazima muunde mazingira rafiki yanayoheshimu muda wa uzalishaji wa watu,” alisema.

Aliwasilisha pia kipaumbele cha kupanua ujenzi wa nyumba hadi pembezoni mwa nchi na kusisitiza kuwa mpango huo hauwezi kutegemea bajeti ya serikali pekee, akisema ni lazima kufikiri nje ya boksi kutafuta vyanzo vingine vya fedha, pamoja na ushirikiano na Halmashauri zenye uwezo.

Aidha, alitoa maelekezo madhubuti kuhusu ubora, akisisitiza kuwa nyumba zote mpya zijengwe kwa viwango vya hali ya juu na kusema wazi, “Msikubali kupunguza ubora.”

“Mfumo ambao mtu anaweza kuwekeza akiwa nyumbani, kazini au hata akiwa safarini kupitia simu ya mkononi huo ndiyo mwelekeo wa kisasa tunaoutaka,” alisisitiza.

Pia,alihimiza WHI kushirikiana na e-GA kuunga mkono vijana wakiwemo waendesha bodaboda, wafanyabiashara wadogo pamoja na wawekezaji wakubwa, akisema urahisishaji wa taratibu utavutia wachangiaji wengi zaidi.

“Vijana hawapaswi kukutana na taratibu ndefu na ngumu. Mfumo rahisi utavutia wengi,” aliongeza.

Kikwete pia alitoa wito wa kuongeza uelimishaji kwa umma ili mfuko uweze kuvutia wawekezaji wengi na kufikia malengo yake, akisisitiza kwamba Faida Fund bado haijawafikia Watanzania wengi na kwamba si vyema kutegemea tovuti pekee, bali kutumia njia zinazowafikia watu kwa urahisi.

“Anzeni kwa kuwapa taarifa wahariri. Wakishaelewa mfuko, watasaidia kuutangaza na kuuelimisha umma,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa Watumishi Housing Investment (WHI) Arch. Sephania Solomon  (aliyesimama) akielezea mafanikio ya mradi wa kujenga nyumba za Watumishi ulipofikia kwa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete alipofanya  ziara ya utambulisho ofisini hapo leo Novemba 27,2025.

Post a Comment

0 Comments