6/recent/ticker-posts

Balozi Seif Afanya Ziara ya Ghafla kwa Baadhi ya Vituo vya Mafuta

Na Othman Khamis Ame

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amefanya ziara ya ghafla katika baadhi ya Vituo vya Mafuta ya vyombo vya moto ndani ya mkoa wa Mjini Magharibi.

Ziara hiyo imekuja kufuatia uhaba wa mafuta ya aina ya Petroli uliojitokeza kwa karibu mwezi mmoja sasa na kupelekea usumbufu kwa Wananchi walio wengi wanaotumia usafiri vya vyombo vya Moto.

Balozi Seif alishuhudia msongamano mkubwa wa Magari katika Kituo cha Mafuta cha uwanja wa ndege ambapo wauzaji wa Vituo hivyo wamesema mgao wanaopata katika kipindi hichi hauzidi Lita 1,000 tu ambazo hazikidhi hata kidogo mahitaji ya wateja wao.


Wauzaji hao walimueleza Balozi Seif kwamba hakuna ujanja unaotumika wa ufichaji wa Bidhaa hiyo kwa kisingizio cha kutaka kupandisha bei.

Balozi Seif alionya vikali tabia ya baadhi ya watu kuweka mafuta Majumbani na kwenye madumu kitendo ambacho ni hatari kwa maisha yao na Jamii inayowazunguuka.

“ Tumekuwa mashahidi wa matukio tofauti yanayojichomoza katika kipindi yanapoadimika mafuta ambayo mengi huleta athari ya vifo kutokana na uzembe wa uwekwaji wa mafuta ovyo katika makaazi ya Watu ”. Alionya Balozi seif.

Balozi Seif baadaye alivitembelea Vituo vya hifadhi ya mafuta vya Gapco, Zanzibar Petroleu, United Petroleu na BP Vilivyopo Mtoni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Meneja mkuu wa Zanzibar Petroelum Bw. Collin Chemngorem alimueleza Balozi Seif kwamba Mfumo uliopo hivi sasa wa uagizaji na usambazaji wa Matuta Nchini Tanzania wa kufanywa na Kampuni moja umepelekea huduma hiyo pungua hapa Zanzibar.

Bw. ColliN alisema upungufu huo umekuja kutokana na mlolongo mkubwa wa upakizi wa mafuta kwenye Meli katika kituo cha pamoja Mjini Dar es salaam hali iliyopelekea meli inayoleta mafuta Zanzibar
kukaa kwa karibu mwezi mmoja kutokana na ufinyu wa Kima cha Mafuta yake ya lita milioni sita ambazo hutumika kwa mwezi.

Alisema mfumo huo wa sasa { Belco System } unatoa fursa zaidi kwa Meli zenye uwezo wa kupakia Mafuta kuanzia kima cha lita Milioni 30,000,000/-.

Meneja mkuu huyo wa Zanzibar Petroleum alimueleza Balozi Seif kwamba Kampuni zao kwa pamoja zimeshaandika Waraka na kuuwasilisha Serikalini ili mgao wa Zanzibar wa Mafuta wa lita milioni sita uingizwe katika utaratibu Maalum badala ya ule wa jumla.

Aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar izungumze na Serikali ya Muungano wa Tanazania kufikiria Tenda zinazotolewa pia zilenge na Zanzibar.

Post a Comment

1 Comments

  1. Hivi ndivo viongozi wanavotakiwa sio kikaa ofisini tuu, napenda nimpongeze Mh Seif na wengine waige mfano wake

    ReplyDelete