Na Shifaa Said
WAZIRI wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk ameahidi kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT), katika kufuatilia kwa karibu mapendekezo ya wadau kuhusu mswada wa sheria ya habari na sheria ya haki ya kupata habari.
Akizungumza na watendaji wa Baraza la Habari Tanzania ofisi ya Zanzibar, alisema kuwa anathamini kwa dhati shuguhuli zinazofanywa na MCT hususan katika kukuza na kuimarisha kada ya habari hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Alisema kuwa shughuli hizo zinapaswa kuungwa mkono na wizara na kwamba hivi sasa wizara itafuatilia kwa karibu mapendekezo ya wadau kuhusu sheria za habari ili waandishi waweze kufanya kazi zao katika mazingira mazuri.
“Wizara inaahidi kuwa mapendekezo haya kamwe hayotabaki katika majarida na kuanzia mwezi wa Septemba mwaka huu, wizara itayafanyia kazi mapendekezo hayo”,alisema waziri Mbarouk.
Alisema kuwa kuwepo kwa Baraza na kuwa na ofisi iliyokamilika ni hatua muhimu katika kukuza kada ya habari na hivyo, shughuli zote za Baraza hazina budi kuungwa mkono kwani ni hatua muhimu ya kuendeleza na kukuza uhuru wa habari hapa nchini.
Aidha alitoa wito maalum kwa MCT kufuatilia kwa karibu masuala ya maadili ya habari ili kuhakikisha kuwa yanafuatwa na kutoa mafunzo ya mara kwa mara katika nyanja hiyo ambayo imekuwa ikikiukwa mara kwa mara.
Aidha waziri huyo alisema kuna haja kwa waandishi wa Zanzibar kujikita katika uandishi wa fani maalum, ili waweze kuwa mahiri zaidi katika kazi zao.
Alikumbusha waandishi haja ya kufanya utafiti wa kina katika kuandikahabari zao ili suala la haki ya kupata taarifa kwa wananchi liwezekuzingatiwa lakini pia ukweli na utafiti iwe ni suala kuu katika habari.
Waziri Mbarouk alisema kuwa utafiti katika uandishi wa habari nail ni suali muhimu ambapo huwawezesha kuandika habari hizo kwa umakini.
“Ni muhimu kutoa taarifa zenye ukweli, zilizofanyiwa utafiti pamoja nakuandika habari za vijijini ili serikali iweze kutambua matatizo yanayo wakabili wananchi walio wengi”, alisiisitiza.
Alisema kuwa bado habari za vijijini hazijapewa umuhimu wa kutosha ili sauti za watu wasio na sauti ziweze kusikika, na pia habari hizo zitasaidia kuibua changamoto na hivyo kuifanya serikali kuweza kufuatilia kwa karibu kuleta ufumbuzi wa changamoto hizo.
Naye Katibu Mkuu wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Dk. Ally Mwinyikai, alisema kuwa shughuli zinazofanywa na MCT katika kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi ni muhimu katika kuimarisha kada hiyo.
Aidha Katibu huyo alisema kwa kipindi kirefu Baraza limekuwa likishirikiana na wizara katika masuala mbali mbali hususan ya mafunzo na kutoa wito kwa Baraza hilo kuendelea kutoa mafunzo.
“Mafunzo yatolewayo na Baraza la Habari, hayana budi kuendelezwa kwani husaidia kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa Zanzibar ili waweze kukuza uelewa na ufahamu wao katika fani mbali mbali za habari’, alisisitiza.
Awali Meneja wa MCT Zanzibar Suleiman Seif Omar alitoa wito maalum wa kuimarisha mashirikiano baina ya Baraza la habari Tanzania na wizara hiyo.
“Ushirikiano uimarishwe kwani sote ni wadau wa habari na lengo, letu ni kukuza na kuiamarisha sekta hiyo hapa nchini”,alisema Meneja huyo.
Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Barza la Habari Tanzania na kuhudhuriwa na watendaji wa MCT, Zanzibar Press Club, pia ulihudhuriwa na Naibu waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Bihindi Hamad Khamis.
0 Comments