6/recent/ticker-posts

Cannavaro na wenzake waripoti Zanzibar Heroes

Na Salum Vuai, Maelezo
 
WAKATI kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka Zanzibar Heroes Salum Bausi, leo akipanga kupiga mstari mwekundu kwa wachezaji waliochelewa kuripoti kambini, wanasoka wanaocheza ligi kuu Tanzania Bara wamejiunga na wenzao juzi usiku na jana.
 
Bausi amewataja wachezaji waliopiga ripoti juzi usiku katika kambi ya timu iliyoko Chukwani, kuwa ni Khamis Mcha ‘Viali’, Samir Haji Nuhu na Abdulhalim Humud kutoka klabu ya Azam, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga) na Amir Hamad kutoka JKT Oljoro.

 
Aidha, alisema mabeki Nassor Masoud (Simba) na Aggrey Morris wa Azam, wameshindwa kufika Zanzibar kutokana na kuwemo katika timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars iliyokuwa na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Kenya katika uwanja wa CCM Kirumba jana.
 
Hata hivyo, mchezaji Suleiman Kassim ‘Selembe’, alikwisharipoti tangu juzi lakini ameruhusiwa kwenda Pemba katika msiba wa baba yake mzazi aliyefariki siku mbili zilizopita.
 
Katika hatua nyengine, kocha huyo amemwita mchezaji Seif Rashid ‘Karia’ anayechezea JKT Ruvu, kujaza nafasi ya Hamad Mshamata ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam aliyekwenda masomoni.
 
Bausi alisema mlinda mlango Mwadini Ali anayekipiga na Azam FC aliripoti jana wakati wa mazoezi ya jioni, ingawa Taha Mohammed anayechezea Mtibwa Sugar ya Morogoro ameshindwa kuripoti kambini licha ya kuwepo Zanzibar, ingawa juzi alifika na kutoa dharura.
 
  Kikosi cha timu hiyo kimekuwa kimepiga kambi hukoChukwani nje kidogo ya manispaa ya Zanzibar, na taarifa za Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) zimefahamisha kuwa programu yote inakwenda vizuri, ikiwa pamoja na upatikanaji wa mahitaji yote muhimu na posho za kila siku za wachezaji na benchi la ufundi.
 
Zanzibar Heroes iliyopangwa katika kundi C la mashishidano ya Chalenji yanayoanza Novemba 24, jijini Kampala Uganda pamoja na timu za Rwanda, Eritrea na Malawi, inatarajiwa kuondoka nchini tarehe 22 mwezi huu tayari kwa ngarambe hizo zinazoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
 
Timu hiyo inatarajiwa kutupa karata yake ya kwanza katika michuano hiyo kwa kupambana na Eritrea Novemba 26, mwaka huu wakati wa saa tisa mchana katika uwanja wa Taifa Kampala.

Post a Comment

0 Comments