Na Aboud Mahmoud
CHAMA cha Mazoezi ya Viungo Zanzibar (ZABESA), kwa kushirikiana na klabu wanachama mbalimbali, kinatarajia kufanya bonanza lake la nne la mazoezi Januari 1, mwaka 2013.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa ZABESA, Khamis Mohammed kwa waandishi wa habari, imeeleza kuwa, lengo kuu la bonanza hilo ni kuwahamasisha wananchi ambao bado hawajaamua kufanya mazoezi peke yao au katika vikundi, kuona umuhimu wa kufanya hivyo.
Aidha alisema, bonanza hilo linalenga kujenga uhusiano mwema kati ya chama hicho na serikali pamoja na taasisi nyengine za kijamii.
Mohammed alisema, bonanza hilo la mwakani, litakuwa tafauti na mengine yaliyofanyika miaka iliyotangulia, ambapo alisema kuwa, tukio hilo halitakuwa na mashindano ya wiki.
"Awali tulikusudia bonanza lijalo liandaliwe na kamati tendaji mpya, lakini kuchelewa kwa shughuli za uchaguzi, kumeathiri matayarisho ya bonanza hilo", alifahamisha.
Bonanza la wanamazoezi hufanyika kila ifikapo siku ya kwanza ya mwezi Januari kila mwaka, likijumuisha vikundi mbalimbali vya mazoezi, ambapo mara hii limepangwa kushirikisha klabu 33 za wanamazoezi
0 Comments