Ilikuwa waende China jana kwa Qatar Airways
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KLABU ya Yanga, imewazuia wachezaji wake wawili Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Said Rashid Bahanuzi kwenda nchini China kufanya majaribio ya soka la kulipwa.
Wanasoka hao walitarajiwa kuondoka jana saa 10:00 jioni kwa ndege ya Qatar Airways kwenda nchini humo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb amesema sababu za kuwazuia wachezaji hao zimetokana na klabu inayowataka kutofuata taratibu.
“Hawajatuma barua, hawa wanataka kwenda kienyeji tu, na sisi si kama tumewazuia, tumeitaka kwanza hiyo klabu ifuate taratibu kwa kutuma barua huku na kujitambulisha, ili ikitokezea wakapata matatizo tujue tunaanzia wapi”, alisema Bin Kleb.
Mapema jana, Cannavaro ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Zanzibar, na nahodha msaidizi wa Yanga amekaririwa akisema kwamba wanakwenda China kwa wiki mbili na kama watafuzu majaribio, klabu inayowataka itafanya mazungumzo na klabu yao.
“Sisi sote tuna mikataba na klabu, hivyo tukifuzu itabidi klabu inayotutaka ituhamishe Yanga”, alisema beki huyo wa kati ambaye ni tegemeo kwa Yanga na timu za Taifa za Tanzania na Zanzibar.
Cannavaro yupo Yanga tangu mwaka 2006, aliposajiliwa kutoka Tembo ya Zanzibar (sasa haipo), wakati Bahanuzi amesajiliwa msimu huu akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Mwaka 2009, Cannavaro alichukuliwa kwa mkopo na klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada na baada ya miezi sita alirejeshwa Yanga alikoendelea kucheza hadi sasa.
Bahanuzi ameingia Yanga na bahati ya aina yake, kwani katika mashindano ya kwanza kuichezea klabu hiyo alifanikiwa kuibuka mfungaji bora wa klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame).
Hadi sasa, Said Bahanuzi maarufu kama Spider Man, ameifungia Yanga mabao 12 katika mechi 14, yakiwemo matatu ya penalti tangu ajiunge na timu hiyo Julai mwaka huu.
Kwa sasa China ni nchi ambayo nyota wengi waliokuwa Ulaya wanakwenda kumalizia soka huko, wakiwemo washambuliaji wawili wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba na Nicolas Anelka wanaochezea klabu ya Shenghua Shanghai
0 Comments