Na Said Ameir
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein anaondoa leo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tano nchini Uholanzi kufuatia mwaliko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo bwana Mark Rutte.
Akiwa nchini humo Rais wa Zanzibar Jumanne ijayo tarehe 27 Agosti, 2013 atatembelea bandari ya Rotterdam na baadae kufanya mazungumzo na makampuni katika sekta ya miundombinu ya usafiri wa bahari.
Baadae jioni siku hiyo Dk. Shein atakutana na Mfalme wa Uholanzi kwa mazungumzo na baadae kuhudhuria chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa heshma yake.
Siku inayofuata atakutana na Waziri wa Biashara ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, atakutana na wadau katika sekta ya Nishati na pia atatembelea Makamo Makuu ya Kampuni ya Mafuta ya Shell.
Mapema Alhamisi asubuhi Dk. Shein atakutana na Waziri Mkuu wa Uholanzi Bwana Mark Rutte. Baada ya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uholanzi Rais wa Zanzibar atatembelea Kampuni ya vifaa vya uchunguzi wa maradhi ya Sakura ambako atabadilishana mawazo juu ya masuala ya afya kati ya Zanzibar na Uholanzi.
Siku hiyo baadae mchana atatembelea bandari ya Scheveningen ambako atakutana na wananchama wa Muungano wa Wadau katika Sekta ya Uvuvi na kukutana pia na uongozi wa kampuni ya usindikaji na uuzaji wa mazao ya bahari nchini humo. Baadae jioni atakutana na watanzania wanaoishi nchini Uholanzi mjini The Hague.
Katika ziara hiyo Dk. Shein amefuatana na mke wake Mama Mwanamwema, Waziri Ardhi, Makazi, Maji na Nishati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ramadhani Abdalla Shaaban, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Rashid Seif Suleiman, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa KImataifa Mahadhi Juma Maalim, Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchum, Balozi Mohamed Ramia na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Zanzibar Balozi Ame Silima.
0 Comments