WAZIRI wa Fedha Zanzibar, Mhe. Omar Yussuf Mzee, amesema serikali ya China imeingia eneo jipya la kuinua uchumi wa Zanzibar na usalama kwa kutumia mifumo ya kisasa, itakayokuza ukusanyaji wa mapato na ulinzi katika bandari ya Zanzibar.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza katika ufunguzi wa mashine hiyo, pamoja na kuweka saini mkataba wa makabidhiano kati ya serikali ya China na Zanzibar.
Serikali ya China imetoa msaada huo kwa Zanzibar chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake ya kuisaidia mashine hizo nne zenye uwezo wa kukagua makontena 20 kwa saa moja bila ya kufunguliwa.
Mashine hiyo ni ya 30 katika bara la Afrika, ambapo kwa Tanzania ni ya kwanza kuwepo Zanzibar katika nchi 120 zilizopo duniani, na ina thamani ya yuani milioni 23, ambazo ni sawa na dola za Marekani milioni 3.
Saini na makabidhiano hayo yalifanyika ofisi kuu ya Mamlaka ya Mapato Zanzibar, Mlandege mjini Zanzibar, kati ya Waziri huyo na Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar, Xie Shiya na kushuhudiwa na vingozi na wadau wa TRA.
Alisema maamuzi ya China kutoa msaada huo utaiingiza Zanzibar katika eneo jipya la misaada ya kiuchumi inayotolewa na serikali hiyo kwa Zanzibar ndani ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema Zanzibar kwa muda mrefu imekuwa ikifaidika na misaada kutoka China, lakini ilikuwa ikiangalia eneo la huduma za kijamii kwa kusaidia kifedha kwenye miradi mbali mbali na msaada huo ni eneo jipya la kuinua uchumi.
Alisema serikali inafanya juhudi kufanya mabadiliko mbali na vifaa vya kisasa katika utoaji huduma zake ikiwemo bandari ya Zanzibar na kuja mashine hiyo kwa kiasi kikubwa kutaifanya serikali kuongeza mapato na usalama wa mizigo inayoingia nchini.
Alisema suala la usalama wa bandari ni moja ya mambo ya msingi kwa sasa, hasa ikizingatiwa Zanzibar ni visiwa.
Alisema serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwepo ukweli katika utendaji wake pia itafikiria kutoa mafunzo kwa Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali ili kuona taarifa zinazotolewa kati ya maofisa wa TRA, ziunakuwa na thamani halisi na ushuru unaotozwa.
Aliwataka watendaji wa mamlaka hiyo, kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao vyema huku serikali ikifikiria kuzungumza na serikali ya China, namna ya kuwapatia mafunzo wa kutumia mashine hiyo.
Mapema Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar, Xie Shiya, akitoa salamu zake alisema msaada huo ni muendelezo wa misaada yake kwa Zanzibar, tangu Mapinduzi na inafungua ukurasa mpya wa kiuchumi.
Alisema mashine hiyo kwa kiasi kikubwa zimeonesha mafanikio makubwa katika mataifa mbali mbali duniani ambapo Zanzibar itakuwa ni ya kwanza kati ya nchi 30 za bara la Afrika na 100 za Duniani kutumia mashine hiyo.
Nae Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar, Mcha Hassan Mcha, alisema mashine hiyo kwa kiasi kikubwa itasaidia kukuza huduma za usafirishaji na upokeaji wa mizigo.
0 Comments