MAELEZO YA SERIKALI JUU YA HOJA MBALIMBALI ZA KAMATI
YA PAC YA BARAZA LA WAWAKILISHI KUHUSU SHIRIKA LA UMEME LA ZANZIBAR (ZECO)
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa
kwamba katika Mkutano wa Saba wa Baraza la Nane la Wawakilishi, Mjumbe wa
Baraza la Wawakilishi wa kuchaguliwa na wananchi wa Jimbo la Kiwani, Mheshimiwa
Hija Hassan Hija kwa kutumia haki yake chini ya Kanuni za Baraza ya 27 (1) (m),
27 (3), 48 (1) na 49 (1) Toleo la 2011 aliwasilisha hoja binafsi kwa mujibu wa
Kanuni ya 117 ya Kanuni za Baraza na kulitaka Baraza liridhie kuunda Kamati
Teule kwa ajili ya kulichunguza Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).
Mheshimiwa
Spika, Vilevile itakumbukwa kwamba Baraza
lako Tukufu lilikubaliana kwamba hoja hiyo ya Mheshimiwa Hija Hassan Hija
ifanyiwe kazi kupitia Kamati ya Kudumu ya Baraza ya Kuchunguza na Kudhibiti
Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC) na Mheshimiwa Hija mwenyewe
kuingizwa katika kamati hiyo ili kusaidia katika uchunguzi huo.
Mheshimiwa Spika, kufuatia
uamuzi huo wa Baraza, Kamati ya PAC ikimjumuisha Mheshimiwa Hija ilianza
kufanya kazi hiyo rasmi tarehe 30 Aprili, 2012 na kuwasilisha ripoti yake
Barazani katika Kikao cha Baraza kilichofanyika Mwezi wa Machi, 2013. Baada ya
kuwasilishwa, Serikali iliahidi kuifanyia kazi ipasavyo Ripoti hiyo ya PAC na
baadae kuwasilisha taarifa rasmi katika Baraza lako hili.
Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepokea Ripoti ya Kamati ya PAC ya Baraza
lako kuhusu Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) kwa moyo mkunjufu na kuifanyia kazi kwa umakini mkubwa na
uadilifu wa hali ya juu ili kuona mapungufu yaliyoonyeshwa katika Ripoti hiyo yanafanyiwa
kazi kwa maslahi ya nchi yetu na vile vile wale walioguswa wanafanyiwa haki na
uadilifu kufuatana na matakwa ya Sheria za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, napenda
kuchukua fursa hii kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kukushukuru kwa dhati wewe mwenyewe binafsi kwa kukubali hoja ya Mheshimiwa
Hija Hassan Hija kufanyiwa kazi na PAC. Aidha,
nawapongeza kwa dhati Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati ya PAC kwa kazi
kubwa na nzuri walioifanya katika kuchunguza utendaji wa Shirika la Umeme la
Zanzibar na kuwasilisha vyema kwa Baraza taarifa yao. Aidha, niwashukuru
Wajumbe wote kwa michango yao
na kufikia mapendkezo yenye ufanisi. Kwa kweli taarifa hii imetuonesha mambo
mengi ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi na Serikali ili kuimarisha utendaji wa
Shirika kwa maslahi ya Taifa letu. Muelekeo huu wa mashirikiano miongoni mwa
mihimili mikuu ya Serikali ndio hasa utakao tusaidia katika kujenga mustakbali
mwema wa nchi yetu na kuimarisha dhana ya utawala bora na kupambana na vitendo
vyote viovu ndani ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar .
Mheshimiwa Spika, napenda
kulijulisha Baraza lako Tukufu kwamba Serikali tayari imeshaanza kuyafanyia
kazi mapendekezo yaliyotolewa na Baraza la Wawakilishi na kuchukua hatua
stahiki katika baadhi ya maeneo yaliyopendekezwa na Wajumbe.
2.0 MAELEZO KUHUSU HOJA MBALIMBALI ZILIZOTOLEWA
KATIKA RIPOTI YA KAMATI YA PAC
Mheshimiwa Spika, baada
ya kutoa maelezo hayo ya utangulizi sasa naomba uniruhusu kutoa ufafanuzi wa
Serikali juu ya hoja mbali mbali zilizojitokeza katika Ripoti ya Kamati ya PAC kama ifuatavyo:
Hoja Nambari 1: Wateja kupewa risiti zenye kiwango
kidogo kuliko malipo halisi waliyolipa.
Mheshimiwa
Spika,
katika Ripoti ya Kamati ilionyeshwa kasoro ya baadhi ya wateja wa Shirika
kupewa risiti zenye kiwango kidogo kuliko malipo halisi waliyolipa wateja hao
na hivyo Kamati kupendekeza kuwa watendaji wote waliohusika wachukuliwe hatua
za kinidhamu na kisheria.
Mheshimiwa
Spika, maelezo
ya Serikali kuhusu hoja hii ni kwamba Serikali inakubaliana na mapendekezo
yaliyotolewa na Baraza lako Tukufu na tayari hatua imeshachukuliwa na Shirika la Umeme kwa
kuliarifu Jeshi la Polisi kuanza kuchukua hatua za kufanya uchunguzi wa
malalamiko ya wateja waliolalamikia kulipa fedha nyingi lakini risiti
walizopewa zimeandikiwa fedha kidogo. Aidha, Serikali imelitaka Jeshi la Polisi
liwatake wateja hao kuwabainisha watendaji waliohusika na suala hili ili
liwachunguze na iwapo watabainika kuwa wamekiuka sheria na taratibu wachukuliwe hatua za kisheria.
Mheshimiwa
Spika,
kwa mujibu wa Kifungu Nam .
44 cha Sheria ya Shirika la Umeme Nam . 3 ya mwaka 2006, Serikali
imemuagiza Waziri anaehusika na Sekta ya Nishati kuunda Kamati ya Rufaa za
Wateja ili kushughulikia malalamiko ya wateja. Napenda kuwaarifu kwamba, hatua
za kuunda Kamati ya Rufaa za wateja zinakaribia kukamilika. Mambo ya msingi
yanayozingatiwa katika uundaji wa Kamati hii ni namna itakavyotekeleza majukumu
yake. Hivi sasa Shirika la Umeme limo katika jitihada kubwa ya kushughulikia manung’uniko
ya wateja na kutoa huduma zake bila upendeleo na kuepusha kuwepo hisia za mianya
ya rushwa.
Mheshimiwa
Spika,
kuhusu suala la Fundi Salum Saad Khamis, naomba
kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba mfanyakazi huyo tayari amesimamishwa kazi
ili kuruhusu hatua za uchunguzi ziweze kuchukuliwa dhidi yake.
Mheshimiwa Spika, Vilevile napenda kuliarifu
Baraza lako Tukufu kwamba Shirika la Umeme tayari limeshaliandikia Jeshi la
Polisi kukumbushia kuhusu kesi yenye Nambari RB1250/2012 iliyopo Kituo cha
Polisi Chake Chake na RB302/2013 ya Kituo cha Polisi Konde zinazomuhusu Ndugu Abeid Mohammed Abeid ili
Jeshi hilo liharakishe uchunguzi haraka iwezekanavyo na upelelezi
utakapokamilika na kukidhi vigezo vya kisheria hatua za kisheria zichukue
mkondo wake dhidi ya mtuhumiwa huyo. Aidha, Kamishna wa Polisi Zanzibar
ametakiwa kusimamia kwa karibu ili utekelezaji wa suala hili uende
haraka.
Mheshimiwa
Spika,
napenda kuwajulisha Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwamba tayari
barua za onyo zimetolewa kwa Meneja Mkuu na Meneja wa Tawi la Pemba kwa kutokuwa
makini katika kusimamia majukumu yao na kushindwa
kuwasimamia vyema watendaji walio chini yao .
Barua hizo za onyo zimetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Nambari
2 ya 2011. Na bado Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo ya
watendaji hao ili kuona wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria
za utumishi wa umma. Iwapo wakibainika kwenda kinyume, hatua za kinidhamu
zitachukuliwa dhidi yao .
Mheshimiwa
Spika,
Serikali pia imetoa onyo la mwisho la maandishi kwa Ndugu Ahmed S. Yussuf kwa
kitendo chake cha kujifanya wakala wa wateja wanaotaka kuungiwa umeme wakati
yeye ni mfanyakazi wa Shirika. Aidha,
Serikali haitomvumilia mtendaji yeyote wa Shirika atakaekwenda kinyume na
maadili ya kazi yaliyowekwa.
Hoja Nambari 2: Fedha za Malipo ya kuungiwa
umeme kuingizwa katika Akaunti ya
Mtendaji wa Shirika, Ndugu Zakia Juma Azan
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Kamati ya PAC ilipendekeza kuchukuliwa hatua za
kisheria na kinidhamu dhidi ya mhusika Ndugu Zakia Juma Azan kwa kutokuwa
muadilifu katika utekelezaji wa majukumu yake. Ndugu Zakia alijihusisha na uwakala
wa mteja wa kuungiwa umeme wakati huo huo akiwa ni mfanyakazi wa Shirika la
Umeme. Hatua hiyo inapelekea kuwa na
mgongano wa kimaslahi baina ya Ndugu Zakia na Shirika la Umeme. Kutokana na
hali hiyo, Serikali inakubaliana na pendekezo hilo la Kamati na tayari hatua ya kumhamisha Ndugu
Zakia kutoka Shirika la Umeme imechukuliwa. Hatua hizo za kinidhamu
zimechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Nambari 2 ya mwaka 2011.
Mfanyakazi huyo amehamishwa kutoka Shirika la Umeme kwenda Wizara ya Ardhi,
Makaazi, Maji na Nishati na huku akiangaliwa utendaji wake.
Hoja Nambari 3 na 6:
Kuwepo kwa makisio ya aina mbili kwa
mteja mmoja.
Mheshimiwa Spika, kuhusu
hoja hii, Serikali inaishukuru Kamati kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kugundua
mapungufu haya ambayo yalichangia kulikosesha Shirika la Umeme mapato kutokana
na udanganyifu wa baadhi ya watendaji wa Shirika kutoa makisio ya aina mbili
kwa mteja mmoja. Serikali imelitaka Shirika la Umeme kuwa makini katika
utendaji wake na kuzingatia sheria na taratibu za kazi na Wizara husika
imetakiwa kuwa karibu zaidi kulisimamia Shirika ili mapungufu kama
haya yasitokee tena. Aidha, Shirika limetakiwa kuanzia sasa kuwa wazi kwa
kuweka bayana vigezo na viwango bila ya kuwepo mwanya wa ubabaishaji ili kila
mteja anaetaka kuunga umeme aweze kujua gharama zake. Vile vile, Shirika
limetakiwa kuwa makini katika kufanya tathmini ya gharama za wateja wakati wa
kuwaungia umeme na kutoa makisio na maelezo sahihi ya aina na sifa za vifaa vinavyotakiwa
(Specifications) kwa mteja ili kuepuka wateja kununua vifaa visivyokuwa na
viwango vinavyotakiwa au visivyohitajika.
Hoja Nambari 4, 17 na 18: Ushiriki wa Mohammed &
Bashir kwa niaba ya Sana
Express katika zoezi zima la uungwaji wa umeme katika Hoteli ya Misali.
Mheshimiwa
Spika,
kuhusu hoja ya Kamati juu ya ushiriki wa Duka la Mohammed & Bashir ambalo
halimo katika orodha ya maduka/makampuni yaliyopewa kibali na Shirika cha kuuza
na kusambaza vifaa vya umeme. Shirika tayari limeiandikia rasmi Kampuni ya
Mohammed & Bashir kusitisha mara moja biashara ya uuzaji wa vifaa vya umeme
na kwamba Shirika halitosita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Kampuni yoyote
itakayoendesha biashara inayohusu masuala ya umeme bila ya kibali cha Shirika. Aidha,
Serikali imeliagiza Jeshi la Polisi na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kufanya
uchunguzi wa kina kwa Kampuni hiyo ya Mohammed & Bashir kuhusu tuhuma za kutumia
risiti za Kampuni ya Sana na kwa kufanya hivyo kuna uwezekano wa
mhusika kukwepa kulipa kodi. Vile vile, Serikali imelitaka Shirika kuanzia sasa
kuhakikisha linajiandaa kuwa na vifaa vya kutosha vinavyokidhi mahitaji ya
wateja wanaotaka kuungiwa umeme sambamba na kuhakikisha kuwa vifaa vya umeme
vinavyotoka nje ya nchi vinakuwa na viwango bora kwa kuvifanyia ukaguzi
unaostahiki kabla havijaanza kutumika kwa kushirikiana na taasisi inayohusika
na ubora wa viwango (Zanzibar Bureau of Standards-ZBS)
Hoja Nambari 5: Namna ya upatikanaji wa vifaa vya
uungwaji wa umeme katika Hoteli ya Misali.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana
na hoja hii ya vifaa vilivyotumika kuunga umeme kwenye Hoteli ya Misali vilivyochukuliwa
kutoka katika ghala la Shirika, kumejitokeza mgongano wa maelezo yaliyotolewa. Hivyo,
Serikali imemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kufanya uchunguzi
zaidi wa suala hilo . Baada ya uchunguzi huo wa Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu, Serikali itachukua hatua muafaka kwa kuzingatia ushahidi utaopatikana.
Hoja nambari 7: Fundi Abeid Mohammed Abeid si
Mfanyakazi wa Shirika lakini anafanya kazi za Shirika kinyume na utaratibu.
Mheshimiwa Spika,
tunakubaliana na hoja ya Baraza lako Tukufu kuwa fundi Abeid Mohammed Abeid si
mfanyakazi wa Shirika la Umeme na kwa kutambua hilo, Serikali imelitaka Shirika
kuwa makini na watu kama hao ambao wanafanya kazi za Shirika lakini si
waajiriwa wa Shirika hilo na kupelekea kulihujumu Shirika. Shirika tayari limeliandikia Jeshi la Polisi na
kulitaka kufanya upelelezi wa kina kwa suala hili na kwa wahusika wote na
kuchukua hatua muafaka za kisheria dhidi ya wale wote watakaobainika kuhusika
na makosa hayo.
Hoja Nambari 8: Kukiukwa agizo la Bodi ya
Wakurugenzi kuhusu mgongano wa maslahi katika ushiriki wa Ndugu Hamidu Saidani
Ali na Ndugu Ali Abeid Haji katika ZECO na GECCO.
Mheshimiwa
Spika,
Suala la kuwepo kwa mgongano wa maslahi (conflict of interests) kuhusu baadhi
ya wafanyakazi wa ZECO pia kuwa ni wafanyakazi wa Kampuni binafsi ya GECCO ni
jambo ambalo halikubaliki hata kidogo. Ili kuondoa mgongano wa maslahi, Serikali imechukua hatua
ya kuwahamisha wafanyakazi hao na
kuwapeleka sehemu nyengine.
Hoja
Nambari 9: Watu walioungiwa umeme kinyume na utaratibu, na baadhi ya Wateja
kutumia huduma hii bila ya kusajiliwa na hivyo kutumia umeme bure. (Hawamo
katika orodha ya Wateja wa Shirika).
Mheshimiwa Spika, Serikali inakiri kwamba lipo
tatizo la baadhi ya watendaji wa Shirika ambao si waadilifu huwaungia umeme wateja
kinyume na utaratibu uliowekwa na Shirika kwa maslahi yao binafsi. Hivyo,
Shirika tayari limeshaliandikia Jeshi la Polisi kuanza uchunguzi wa kina kwa
wale wote waliotajwa katika Ripoti ya PAC kuwa wameungiwa umeme kinyume na
utaratibu na kuwataka watu hao kuwataja watu waliowaungia umeme huo. Baada ya
uchunguzi hatua za kisheria zichukuliwe kwa watakaobainika wana makosa.
Hoja Nambari 10: Mkurugenzi Mkuu wa ZBC aliruhusu Kampuni
Binafsi ya Zanzibar Data Com kutumia umeme kutoka katika mnara wa ZBC kinyume na utaratibu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Serikali inaendelea kulifuatilia
suala hili kutokana na kukosekana kwa taarifa zitakazowezesha kutoa maelezo
sahihi.
Hoja nambari 11 na 25: Ndugu Mohamed Hashim Ismail
aliagiza kurudishwa umeme kwenye mnara wa Kampuni ya Zanzibar Data Com. kinyume
na utaratibu.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya PAC ilimuona aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya
Shirika la Umeme Ndugu Mohammed Hashim Ismail kuwa ameliingiza Shirika katika
hasara kwa kuagiza kurudishwa umeme katika mnara unaotumiwa na Kampuni ya
Zanzibar Data Com kinyume na utaratibu. Serikali imefuatilia hoja hii na kuona
kwamba hakuna hasara iliyopatikana kutokana na amri ya Mwenyekiti wa Bodi, kwa
sababu wakati wa kurudishwa umeme huo Shirika liliiwekea Kampuni hiyo mita ya
TUKUZA na deni lake lote la nyuma liliingizwa katika mita hiyo. Kwa sababu hiyo
Serikali imeona hakuna sababu za kumchukulia hatua za kisheria Mwenyekiti huyo
wa zamani wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme.
Hoja Nambari 12: Bodi ya Wakurugenzi ya ZECO ikiongozwa
na Mwenyekiti wake Ndugu Mohamed Hashim Ismaili iliichagua Kampuni ya CRJE
badala ya Salcon iliyoshinda zabuni katika ujenzi wa misingi ya majenereta 32
na baadae kuvunja mkataba na CRJE uliopelekea Shirika kulipa fidia ya Dola za
Kimarekani 20,786.00 na kulitia hasara
Shirika.
Mheshimiwa Spika, ni kweli Bodi ya ZECO iliichagua
Kampuni ya CRJE badala ya Kampuni ya Salcon iliyoshinda zabuni ya ujenzi wa
misingi ya majenereta 32 na baadae kulazimika kuvunja mkataba na Kampuni hiyo
ya CRJE. Hata hivyo fedha zilizolipwa hazikuwa za fidia ila ni malipo ya kazi
iliyowahi kufanywa na CRJE. Aidha, Serikali baada ya kulichunguza suala hili
pia iligundua kwamba Kampuni ya MANTRAC
walilipwa fedha zao za ujenzi kama kwamba Kampuni ya CRJE haikulipwa kabisa. Hivyo,
Serikali imeliagiza Shirika la ZECO liliandikie MANTRAC kulipa fedha za CRJE.
Hoja Nambari 13: Tofauti ya malipo kwa kazi inayofanana,
au wakati mwengine kazi kubwa kuwa na
malipo madogo katika uungaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Shirika kutoza malipo tofauti kwa kazi zinazofanana Serikali
imelitaka Shirika liwe makini katika kufanya tathmini za gharama za wateja
wakati wa kuwaungia umeme. Vile vile
Shirika limeagizwa kuweka viwango vya bei vinavyoeleweka kwa ajili ya uungaji
wa umeme ili kila anaehitaji huduma aweze kujua gharama halisi.
Hoja Nambari 14: Upendeleo katika uungwaji wa umeme
ambapo baadhi ya wateja walioomba mwisho wanapewa kipao mbele kuliko wale
walioomba mwanzo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa dhamira ya Shirika si kufanya kazi kwa upendeleo, hivyo Shirika
litajtahidi kuepuka manung’uniko na litoe huduma bila ya upendeleo na liepushe
hisia za kuwepo mianya ya rushwa.
Hoja Nambari 15: Malipo yanayolipwa na baadhi ya Wateja
bila ya kupewa risiti kabisa. Baadhi ya wateja kuuziwa vifaa vya Shirika lakini
hakuna risiti za mauzo hayo Mfano: Atlas Hoteli.
Mheshimiwa Spika, Serikali imelitaka Shirika la Umeme litoe elimu kwa wananchi kwamba kamwe
wasikubali kulipa pesa mikononi kwa mtu yoyote kwa ajili ya kupata huduma za
umeme, malipo yote yalipwe katika Shirika na walipaji wapewe risiti
zinazolingana na kiasi cha fedha walizotoa. Shirika liwe makini kuhakikisha
kwamba watu wote wasiowaaminifu na wasiokuwa watendaji hawatumii jina la Shirika
kujinuafaisha binafsi. Programu ya kutoa elimu kwa wananchi tayari imeanza na
itaendelea kwa kutumia njia ya redio, televisheni na kwa maofisa wa Shirika
kutembelea maeneo mbalimbali ya wateja. Aidha, Serikali imeona hakuna haja ya
kuchukuliwa hatua yoyote kwa Hoteli ya Atlas kwa vile upo ushahidi wa risiti wa
kwamba hoteli hiyo imelipa gharama za vifaa vilivyotumika kwa kuungiwa umeme.
Hoja Nambari 16: Kazi kubwa ya kuunga umeme kwenye minara
ya simu za mkononi kupewa Kampuni binafsi badala Shirika kuifanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii ya kazi kubwa kupewa Kampuni binafsi badala ya kufanywa na
Shirika lenyewe, Serikali tayari imeliagiza Shirika la Umeme kuhakikisha kwamba
kazi ya kuunga umeme katika maeneo yote inafanywa na Shirika lenyewe isipokuwa
pale inaposhindikana ndio Shirika liidhinishe Kampuni binafsi kufanya kazi
hizo. Aidha, Shirika lihakikishe kuwa sheria na taratibu zinafuatwa kikamilifu
katika kuteua Kampuni binafsi na kwamba hakutakuwa na mgongano wa kimaslahi
baina ya ZECO na Kampuni hizo, viongozi au kwa watumishi.
Hoja Nambari 19: Shirika kuendelea kuiruhusu GECCO
kufanya Biashara ya Transforma wakati kuna agizo la Bodi ya Wakurugenzi ya
Shirika kufuta kibali cha biashara hiyo kwa Kampuni ya GECCO.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeshangazwa sana na kitendo cha ZECO kuwakataza GECCO kuuza
transfoma huku Shirika hilo likiendelea kuzikubali transfoma za GECCO
zinazoletwa na wateja na pia kutoheshimu maamuzi ya Bodi iliyolikataza Shirika
hilo kupokea transfoma kutoka Kampuni ya GECCO. Kutokana na hali hiyo, Serikali
imelitaka Shirika la Umeme Zanzibar kuheshimu maamuzi ya Bodi ya Wakurugenzi yanayotolewa
kwa Shirika hilo. Serikali tayari imeshamuonya Meneja Mkuu wa ZECO kuhusiana na
suala hili na kuliagiza Shirika kuchukua hatua za kinidhamu kwa wengine wote
waliohusika na suala hili.
Hoja Nambari 20: Upotevu wa kumbukumbu za Mteja Ras
Kichanga.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeliagiza Shirika la Umeme kufanya uhakiki kwa wateja wake wote
wakubwa na wadogo ili kujua idadi halisi ya wateja na kuweka kumbukumbu
zao. Aidha, Serikali imeliagiza Shirika
la Umeme kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wafanyakazi waliohusika na
kitendo cha kuyaacha majalada ya wateja wa Shirika hilo kuroa. Pia agizo
limetolewa kwa Shirika hilo kuwachukulia hatua za kinidhamu wafanyakazi wote
waliohusika na upotevu wa majalada ya wateja wakubwa wa Shirika pamoja na
wateja wa vituo vya minara ya simu. Shirika tayari limeanza kuchukua hatua za
kinidhamu dhidi ya wahusika wote kwa kuwataka kutoa maelezo kwa nini Shirika
lisiwachukulie hatua kwa makosa waliyoyafanya.
Hoja Nambari 21: Kutochukuliwa hatua za kisheria dhidi ya
Residence Hotel ambayo ilivuta umeme
kwa kutumia Kampuni ya CRJE badala ya ZECO. Na kuiruhusu Kampuni ya GECCO
kufanyakazi ya uungaji wa umeme huku
ikieleweka wazi kuwa sheria inakataza suala hilo.
Mheshimiwa Spika, Kuhusu hoja hii, Serikali imebaini
kuwa kazi ya uungaji wa umeme katika Hoteli ya Residence imefanywa na ZECO na
Kampuni ya CRJE imeilipa ZECO gharama za kazi ya uungaji (labour charge).
Kampuni ya GECCO imeiuzia kampuni ya CRJE vifaa vya umeme vilivyotumika katika
kazi hiyo.
Hoja Nambari 22: Kuruhusu uungwaji wa Umeme kwa Kendwa Beach Resort, Docrim Hotel na The Leisure Hotel bila ya kufuatwa
taratibu.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba masuala kama haya hayajirudii, Serikali imelitaka
Shirika la Umeme kuhakikisha kwamba linawahakiki wateja wote wakubwa na wadogo
ili kujua idadi halisi ya wateja na kumbukumbu zao, kazi ambayo tayari Shirika
limeanza kutekeleza kwa kuandaa mfumo wa kumbukumbu za wateja “Data Base” ambao utakuwa unafanyiwa
mapitio mara kwa mara. Aidha, Serikali imelitaka Shirika kuhakikisha kwamba
kila mteja anaetaka kuungiwa umeme anajaza fomu ya maombi ya kuungiwa umeme na
taarifa zake zinahifadhiwa vizuri ili ziweze kupatikana wakati
zitakapohitajika.
Hoja Nambari 23: Kushindwa kuthibitisha wapi zimenunuliwa
nguzo na transforma zilizotumika katika nyumba ya kupumzikia ya Ndugu Shumbana
Amani Karume. Kushindwa kuthibitisha wapi imenunuliwa Transforma ya “The Sayyida Hotel” na wapi yamelipwa
malipo ya gharama za uungwaji wa umeme wa Hoteli hiyo na taratibu zipi
zilizotumika. Aidha, kusamehewa kodi ya VAT kwa Hoteli hiyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya ukaguzi wa eneo linalohusika na hoja hii na kubaini
kwamba nguzo zilizotumika katika kupeleka umeme huo ni ishirini (20) na Shirika
la Umeme ndilo lililopeleka nguzo hizo. Aidha, Serikali ilipeleka umeme kwa
kuelewa kwamba eneo hilo ni eneo la Uwekezaji na tayari hoteli mbili (2) zimeshajengwa.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa hoja inayoihusu “The Sayyida Hotel”, napenda kuliarifu Baraza
lako Tukufu kwamba hoteli hiyo ililipa kodi ya VAT kama ilivyohitajika. Aidha,
hoteli hiyo haikuunga umeme kwa kutumia transfoma yake.
Hoja Nambari 24: Upatikanaji wa transforma ya hoteli ya
Larosa Deivent na kwa nini taratibu za kawaida hazikufuatwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefuatilia suala hili
na kubaini kwamba transfoma iliyowekwa katika Hoteli ya Larosa Deivent imenunuliwa
na mmiliki wa hoteli hiyo kutoka kampuni ya OSAJU.
Hoja Nambari
26: Kampuni ya Zanzibar Data Com kwa
mnara wa Mtoni inadaiwa kiasi gani? na italipa kwa utaratibu gani na kwa muda
gani?
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Zanzibar Data Com ilikuwa inadaiwa jumla ya Dola za Kimarekani
9,600 na hadi kufikia mwezi wa Oktoba, 2013 Kampuni hiyo ilikuwa imekwishalipa
Dola za Kimarekani 3,600 na kubakia deni la Dola za Kimarekani 6,000. Shirika la
Umeme limeingia makubaliano na Kampuni ya Zanzibar Data Com ambapo utaratibu ni
kufanya malipo kila mwezi ambayo yanatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha
miezi 24 kuanzia mwezi Machi, 2013.
Hoja Nambari 27: Suala la kuhamishwa “Internal
Auditor” kutoka Pemba na kwa nini kwa muda mrefu Akaunti za hesabu za Pemba
hazijafanyiwa ukaguzi wa ndani na wala wa nje?
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba ni kweli Mchunguzi wa
Hesabu wa Ndani (Internal Auditor) wa Shirika la Umeme wa Pemba alipewa
uhamisho. Hatua za kumhamisha mfanyakazi huyo zilichukuliwa kutokana na kutowajibika
kwake ipasavyo, kitendo ambacho kilipelekea kutotoa ripoti za ukaguzi hata moja
kwa kipindi chote alichokuwepo katika nafasi hiyo. Hivi sasa Shirika tayari limeshampeleka Mchunguzi wa Hesabu wa Ndani mwengine wa
kudumu huko Pemba na pia Serikali imeiagiza
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuzifanyia ukaguzi
hesabu za Shirika hilo huko Pemba.
Hoja Nambari 28: Hakuna ruhusa iliyotoka kwa Bodi ya
Wakurugenzi kuhusu ajira ya wafanyakazi 16 walioajiriwa mwaka 2008.
Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na hoja ya Kamati ya PAC na kulitaka Shirika kutofautisha
baina ya kuidhinishwa kwa bajeti na kuidhinisha kwa uajiri. Hivyo, Shirika
limetenda kosa la kuajiri wafanyakazi 16 mwaka 2008 bila yakupata idhini ya
Bodi ya Wakurugenzi, na hivyo Serikali tayari imempa onyo Meneja Mkuu wa
Shirika la Umeme na kumtaka awe makini zaidi katika utekelezaji wa majukumu
yake na kufuata sheria.
Hoja Nambari 29: Kasoro zilizotajwa kuhusu uajiri kuanzia
2008 mpaka 2012.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kasoro zote zinazohusiana na masuala ya uajiri zilizotajwa katika
hoja hii, Serikali imeliagiza Shirika la Umeme kufuata kwa ukamilifu sheria na
taratibu zote za uajiri kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 2 ya
mwaka 2011, ikiwemo kuzitangaza nafasi za kazi, kuweka vigezo sahihi, kufanya
usaili na kuwepo mikataba ya ajira. Aidha, Shirika limetakiwa kuandaa mpango
wake mkuu wa mafunzo utakaotekelezwa bila ya upendeleo.
Hoja Nambari 30: Uuzwaji wa Gari Land Rover SLS 1023 na
Toyota Pick Up SLS 1045 ambazo ziliuzwa bila ya idhini ya Ofisi ya Rais, Fedha,
Uchumi na Mipango ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja hii naomba kulieleza Baraza lako Tukufu kwamba barua
iliyotoka Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo kuidhinisha
kuuzwa mali za Shirika la Úmeme haikuidhinisha uuzwaji wa gari Nam. SLS 1023
Land Rover na SLS 1045 Toyota Pick Up. Gari hizo ambazo hazikuidhinishwa
aliuziwa Ndugu Shaibu Hassan Kaduara. Hivyo, Serikali imeagiza kufanyika
uchunguzi wa kina kubaini mazingira yaliyopelekea Ndugu Kaduara kuuziwa gari
hizo. Serikali tayari imemuandikia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali kulishughulikia suala hilo. Aidha, hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa
kwa waliohusika iwapo itabainika kuwa gari hizo ziliuzwa bila kufuatwa
utaratibu.
Hoja Nambari 31: Uuzaji wa Mali
za Shirika ambazo ziliuzwa na Uongozi wa Shirika badala ya Kitengo cha Manunuzi
kama sheria inavyoelekeza (kifungu nam. 175(3) cha Kanuni za Sheria Nam. 9 ya
mwaka 2005.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Serikali inakubaliana na mapendekezo ya Kamati ya PAC na
hivyo imeiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika hilo kuwachukulia hatua za
kinidhamu kwa kupewa onyo wote waliohusika na kuuza mali za Shirika bila
kufuata utaratibu uliowekwa na Serikali.
Hoja Nambari 32: Tofauti kati ya orodha ya vitu
vilivyoidhinishwa na Bodi na vitu halisi vilivyouzwa na Shirika katika mnada wa
tarehe 18/12/2011.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida, tungetarajia kuwa kwa vile Shirika la Umeme Tawi la
Pemba liliorodhesha idadi ya vitu walivyotaka kuviuza, Afisi Kuu ya Unguja
ilipaswa kuorodhesha vifaa vyote vilivyoruhusiwa kuuzwa na vilivyokuwa
havikuruhusiwa kuuzwa na mauzo yafanywe kwa mujibu wa ruhusa hiyo. Hivyo, kwa
kuwa kuna vitu vimeuzwa bila ya kufuata utaratibu, Serikali inaendelea kufanya
uchunguzi na hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa kwa wahusika wote watakaobainika
na makosa
kwa mujibu wa Sheria ya
Utumishi wa Umma na Sheria ya Manunuzi.
Hoja Nambari 33: Transforma ya KVA 1500 ambayo haimo
kwenye vifaa vilivyopigwa mnada iliondolewa katika eneo iliyokuwepo na haijulikani
ilikopelekwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Serikali imeiagiza Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali kulifanyia uchunguzi ili kubaini uhalisia wa suala hili. Hatua
za kisheria na kinidhamu zitachukuliwa kwa wale watakaobainika kuhusika na
upoteaji wa transfoma hiyo.
Hoja Nambari 34: Kukodi gari kwa mtu binafsi kwa ajili ya
kazi za Shirika na kutumia pesa nyingi badala ya kununua gari yake kama hiyo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli muda wa miezi tisa (9) ni mrefu kwa kukodi gari ya mtu binafsi
kwa kufanya kazi za Shirika. Hivi sasa Shirika
la Umeme tayari limeshapata gari zake na hivyo limeachana kabisa na utaratibu
wa kukodi gari za mizigo za watu binafsi. Aidha, Shirika limetakiwa wakati wote
kuweka mawazo ya kibiashara na kuepuka kulitia hasara Shirika.
Hoja Nambari 35: Licha ya kuwepo na mkataba baina ya
Shirika na Mtu Binafsi (Mwenye gari) kwa nini alikuwa anatiliwa mafuta kutoka
katika vituo vya mafuta vya Shirika? Fedha alizokuwa akikatwa zilikuwa
zinakwenda wapi?
Mheshimiwa Spika, Serikali ilifuatilia hoja hii na kuona kwamba ni kweli baadhi ya siku gari
lililokodiwa lilitiwa mafuta na Shirika baada ya kukosekana mafuta katika vituo
vya mafuta. Gharama za mafuta aliyokuwa akitiliwa zilikuwa zinakatwa katika
malipo ya mwenye gari hiyo na fedha kurudi katika Shirika kwa faida kwa vile
Shirika lilikuwa linanunua mafuta hayo kwa bei ya jumla na kumkata mwenye gari
hiyo kwa bei ya reja reja. Hivyo, hakukuwa na upotevu wa fedha za Shirika.
Hoja Nambari 36 na 37: Majenereta 32 ya Shirika la Umeme
yaliyopo Mtoni yalipatikana kwa fedha za MDRI au Mfadhili na taratibu gani
zilotumika katika kuyanunua?
Mheshimiwa Spika, Napenda kutoa ufafanuzi kwamba Majenereta haya hayakununuliwa kwa fedha za
MDRI bali yalinunuliwa kwa fedha za Wahisani na Serikali. Aidha, ununuzi huu ulifanywa
kwa mashirikiano baina ya Wahisani na Serikali chini ya Mshauri wa Mradi wa Umeme
Vijijini aliyekubalika na Wahisani hao. Ununuzi huo ulifanyika chini ya
utaratibu wa manunuzi katika hali ya dharura
ambao ulikubalika na pande zote mbili.
Hoja Nambari 38: Mpango wa Shirika la Umeme Zanzibar wa
kuyatumia majenereta 32 ya dharura kwa ufanisi na kwa kutumia gharama nafuu.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja ya kutakiwa Shirika kuwa na Mpango wa matumizi wa
majenereta 32 ya dharura, Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati tayari
imeandaa mapendekezo kuhusu majenereta hayo ya dharura na Serikali itajadili
mapendekkezo hayo na itatoa maelekezo kwa Wizara husika hivi karibuni.
3.0 MTAZAMO
WA SERIKALI KUHUSU RIPOTI YA KAMATI YA PAC
Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa ufafanuzi juu ya hoja mbalimbali zilizotolewa katika Ripoti
ya Kamati ya PAC yapo mambo ambayo Serikali imeona ni vyema kutoa mtazamo wake
ili kuwa na uchambuzi unaostahiki (balanced scrutiny) na kuweka mwelekeo mwema
wa baadae. Aidha, mtazamo huo wa Serikali una nia ya kutoa ushauri juu ya masuala yaliyojitokeza
kwa Kamati wakati ikitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria. Hatua hii
itatusaidia pale itakapotokea haja ya kuwa na Kamati Maalum au Kamati Teule
inayoundwa kuchunguza jambo ili kamati hiyo iweze kufanya kazi zake kwa
uadilifu na bila ya kuonekana kuwa na upendeleo (bias).
Mheshimiwa Spika, Serikali inashauri katika kazi zijazo za Kamati ni vyema ripoti zikaonesha
kwa uwazi maelezo kamili yanayotolewa na watendaji. Aidha, Serikali inashauri
kwamba Baraza liangalie Kanuni ya 120 na kuona uwezekano wa kuifanyia
marekebisho ili mjumbe anaetoa hoja asiwe mjumbe wa Kamati itakayoundwa
kuchunguza hoja hiyo.
4.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar naomba kwa mara nyingine
tena kuchukua fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa jinsi unavyosimamia kazi
za Baraza kwa umakini na umahiri mkubwa na kuniwezesha kuwasilisha taarifa hii
ya Serikali kwa Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako. Vile vile naomba nichukue
fursa hii kwa mara nyingine tena kumshukuru sana Mheshimiwa Hija Hassan Hija,
Mwakilishi wa Wananchi wa Jimbo la Kiwani kwa ujasiri wake na uzalendo wake wa
kuibua hoja ambayo kwa kweli imetuonesha mapungufu tuliyokuwa nayo katika
Shirika, mapungufu ambayo Serikali
imeweka nia ya dhati ya kupambana nayo si kwa Shirika la Umeme tu bali kwa
taasisi zote za Umma.
Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuwashukuru na kutoa pongezi kwa Mwenyekiti wa Kamati ya
PAC, Mheshimiwa Omar Ali Shehe na Wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa kazi kubwa na
nzuri iliyoibua mambo mengi muhimu yenye
mustakbali mwema katika kulijenga Shirika letu na kuimarisha uchumi wa Taifa
letu. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi kwa
kuridhia kamati ya PAC kufanya kazi hii ambayo sote faida yake tumeiona na kwa
kufuatilia kwa utulivu na umakini mkubwa maelezo ya Serikali niliyoyatoa. Pia
nawashukuru wale wote waliyosaidia Kamati ya PAC kufanya kazi zake kwa
kuwapatia taarifa walizozihitaji. Ni imani yangu kuwa viongozi na watendaji
serikalini pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi sote kwa pamoja
tutaitumia fursa hii ya kuibuka kwa hoja hizi kujifunza na kubadilika kwa dhati
na kuachana na tabia ya kufanyakazi kwa mazoea ili kuzidi kuijengea heshima
nchi yetu, kuendelea kujenga imani kwa wananchi wetu na kuimarisha maendeleo ya
kijamii na kiuchumi katika nchi yetu. Haya yote yanawezekana, sote tushirikiane
na tutimize wajibu wetu.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
6 Comments
Kwakuwa haw smz wanajua znz sinch,nisehemu ya kugawana ulaji ndio maana, wana ibabaisha hata hiyo tume alio iyoundwa ndani ya baraza lao sasa wana nchi amkeni ccm na cuf, wezitu
ReplyDeleteSasa inakuaje mambo haya yanatokea halafu mtu anapewa warning, kisha anafundishwa au makini duh, yaani hadi raha hakuna kuwajibishwa hata kidogo.
ReplyDeleteDah nakumbuka maneno ya Mh Nahodha ! Hii ndiyo GNU yetu
ReplyDeletemungu yupo atawahukumu
DeleteAnaye dhulum mungu atamuhukumu na anayekubali kudhumiwa pia atahukumiwa, kwa kukubali kudhulumiwa, tunacho taka hapa visiwani ikifika uchaguzi mkuu, ccmna cuf, na gnu yao wasi chaguliwe, ni mafisadi wanaogopa kuwajibishana, kwasababu ute jahazimoja la rusha ya madaraka, cuf,siwatezi znz, yetu sas tuta ungana na mtikila adai tanganyika yake na sisi tudai znz yetu huru tuwatupennje ya madaraka ccm na cuf, walafi
ReplyDeleteKWANI HAYO MAOZA YAMEANZA LEO HATA HUYO NAHODHA KUSEMA UWOZA KWA GNU?? YEYE SI ALIKUWA KIONGOZI WA SEREKALI MBONA HAYAKUFICHULIWA WAKATI WAKE ???
ReplyDelete