Timu ya NB imefanikiwa kutia kibindoni pointi tatu za kwanza baada ya kuifunga Black Sailors 1-0. Haukuwa mpira wa kukamiana kama ilivyotarajiwa na wengi, ingawa Black Sailors walionekana kucheza rafu za makusudi ambazo huenda zingeharibu mechi hiyo iwapo NB wangejibu rafu hizo na iwapo mwamuzi asingekuwa mkali kidogo. Hata hivyo, ukali huo haukuipunguza kasi Black Sailor, ambapo kuna wakati Samir aliumizwa makusudi akiwa bila ya mpira. Hakukuwa na adhabu yoyote, labda kwa sababu refa hakuona tukio lenyewe.
Tahadhari ya kuwapo mchezo wa kukamiana ilionekana mapema, pale askari kadhaa wa Kikosi cha Kuzuia Fujo walipomiminwa uwanjani kudhibiti fujo yoyote ambayo ingetokea.
Dakika sita tangu mpira kuanza, NB walikosa goli baada ya Juma Ame kupaisha mpira aliotanguliziwa na Rashid. Mashambulizi yakawa yanapishana kwa pande zote, ingawa ni mara chache mipira iliishia magolini.
Kwenye dakika ya 17, NB walikosa tena bao baada ya Ramadhani kupaisha mpira aliotanguliziwa kutoka katikati ya kiwanja. Dakika moja baadaye ikawa zamu ya Black sailor. Mpira wa adhabu ndogo nje kidogo ya eneo la hatari ulipaa kidogo tu juu ya goli la NB.
Kwenye dakika ya 35, mwamuzi alimwonyesha kadi ya njano mchezaji mmoja wa Black Sailors kwa kumrukia Mchezaji wa NB. Dakika tatu baadaye, mwamuzi akatoa faulu ya utatanishi ndani ya 18 ya NB baada ya Chege kubabatizana mpira na mchezaji wa mbele wa Black Sailors. Ilipofika dakika ya 39, Juma Ame tena alipaisha mpira baada ya gonga safi iliyoanzia kwenye nusu ya NB. Huenda ilikuwa ndio gonga safi zaidi kuliko hata iliyozaa goli pekee kwenye kipindi cha pili. Milango ikabaki imefungwa hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa msukosuko ndani ya goli la NB ambapo kwenye dakika ya pili tu mcheezaji wa Black Sailor alipiga shuti kali iliyopaa juu kidogo tu ya goli la NB. Dakika ya 8 NB wakajibu mapigo baada ya Juma Ame kupokea mpira uliookolewa moja kwa moja kutoka golini kwake, akamzidi mbio beki na mpira huo kuishia kuwa kona, iliyofuatiwa na kona nyingine iliyozua kizaazaa kilichoishia na mpira wa adhabu dhidi ya NB.
Dakika moja baadaye, mlinda mlango wa Black Sailors akadaka mpira nje ya eneo lake huku mshika kibendera akimwona, lakini akabaki kuwa mshika kibendera tu! Haikuwa lolote.
NB wakendelea na mashambulizi yaliyozaa kona kwenye dakika ya 20, lakini haikuzaa matunda. Samir aliingia dakika mbili baadaye badala ya Ramadhani aliyeonekana kuishiwa pumzi. Mpira wake wa kwanza aliupokea kutoka kwa Adam Kira aliyeruka juu na kuudondosha mpira huo njiani kwa Samir, aliyemwangalia kipa na kumtungua kirahisi. Dakika ya 67, NB 1- Black Sailors 0. Ulikuwa ndio mpira wake pekee, maaana dakika mbili baadaye alipigwa na kuumizwa akiwa bila ya mpira na mlinzi Said Shah. Alijaribu kuingia baada ya kutibiwa, lakini hakuweza tena. Nafasi yake ikachukuliwa na Bebedi.
Bao hilo likawafanya NB kujichanganya kwa kuondoa mipira ovyo kutoka golini kwao, jambo lililozidisha mashambulizi upande wao. Hali hiyo ilionekana kuwapoteza mwelekeo, kiasi cha Rashid na Juma Ame kupata kadi za kipuuzi za manjano kwenye dakika za 27 na 44.
Ndani ya kipindi hicho cha msukosuko golini kwa NB, kipa Khamis Wazir alidaka mipira zaidi ya mitatu ya hatari kwa ustadi mkubwa, kiasi cha kuonekana kuwa ndiye nyota wa mchezo. Mara zote hizo, alidaka michomo mikali ya juu bila ya kuitema wala kuipangua, huku umati mzima ukishangaa na hatimaye kushangilia.
Kueleka mwishoni mwa mchezo, NB wakaonekana wamejisawazisha, kiasi cha mpira kuvunjwa wakiwa wanajitayarisha kupiga kona.
NB iliwakilishwa na: 1. Khamis Wazir 2. Hussein Kilahe 3. Masoud 4. Ali Denda 5. Gado 6.Chege 7. Bably 8. Rama/Samir/Bebedi 9. Juma Ame 10. Adam Kira 11. Rashid
Kutoka mtandao wa www.newboko.com
0 Comments