Na
Mwandishi wetu
CHAMA
cha Mapinduzi kimewapa onyo kali makada wake sita wanaotuhumiwa kupiga kampeni
za urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.
Taarifa
iliyotolewa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema baada ya
makada hao kuhojiwa kuhusu tuhuma
zinazowakabili, ilithibitika baadhi ya tuhuma
dhidi yao ni za
kweli na hivyo kupendekeza adhabu.
Alisema
mapendekezo hayo yalipelekwa kwenye Tume ya Udhibiti na Nidhamu na hatimaye Kamati
Kuu ya CCM ambayo ilitoa adhabu kwa wahusika.
Makada
hao ni waliokuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye na Edward Lowasa, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa,Bernard Membe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano
na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January
Makamba na Mbunge William Ngeleja.
Nape
alisema kwa ujumla waliohojiwa wamethibitika kuwa na makosa mawili ikiwemo
kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea Urais kabla ya wakati kinyume na
kanuni za uongozi na maadili za CCM.
Kosa
jengine ni kuthibtika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na
baadhi yao
kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.
Alisema
kosa hili nalo ni kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la
Februari 2010.
Alisema
kamati kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo imewapa watu wote sita waliohojiwa
adhabu ya onyo kali na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na
iwapo wataendelea na vitendo hivyo chama kitawachukulia hatua kali zaidi.
Alisema
tafsiri ya adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa kanuni za CCM, mtu aliyepewa adhabu ya onyo kali atakuwa katika hali ya
kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada zake za
kujirekebisha.
Aidha
alisema kamati kuu imeitaka pia kamati ndogo ya udhibiti kuwachunguza na
kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine (mawakala na
wapambe) kufanyika kwa vitendo hivyo vilivyovunja kanuni za chama.
Pia
alisema kamati kuu imewaonya vikali viongozi na watendaji wa chama na kuwataka
kujiepusha kujihusisha na matendo ya wanaowania urais yanayovunja na kukiuka
maadili ya chama.
0 Comments