Na
Kadama Malunde, Kahama.
CHAMA
Cha Wakulima wa pamba nchini (TACOGA), kimemlalamikia Mkuu wa Mkoa wa Geita,
Magalula Said Magalula, kikimtuhumu kutumia vibaya madaraka yake aliyopewa na
Rais.
Mwenyekiti
wa TACOGA, Elias Zizi, alisema Mkuu huyo wa mkoa anapingana na agizo la Rais
Kikwete la kuwataka wakulima kutolazimishwa kujiunga katika kilimo cha mkataba
mpaka kwanza wapewe elimu ya kutosha.
Malalamiko
hayo ya TACOGA yanatokana na hatua ya Mkuu wa mkoa kuagiza kukamatwa na kuwekwa
ndani kwa wawekezaji wa zao la pamba wanaofanya shughuli zao katika mkoa huo
kwa madai hawajatekeleza agizo la kufunga mikataba na wakulima wa zao la pamba.
Aiwataja
wawekezaji waliokamatwa na kuwekwa ndani kwa agizo la mkuu huyo wa mkoa kuwa ni
mwakilishi wa kampuni ya Fresho Investment, Kampuni ya ICK Cotton Co. Ltd na
Kahama Oil Mill Ltd ambao wote wanafanya shughuli zao katika mkoa huo.
Aidha
alisema TACOGA wameshangazwa na hatua ya mkuu mkoa na kudai ni matumizi mabaya
ya madaraka aliyopewa na kwamba suala la kilimo cha mkataba ilisitishwa kwa
muda.
Alisema
baada ya kujitokeza changamogo hizo wadau wote walikubaliana kusitishwa kwa
muda utekelezwaji wa mpango huo mpaka pale changamoto zilizojitokeza
zitakapopatiwa ufumbuzi.
Alisema
kitendo cha mkuu wa mkoa kimelenga kutaka kuzishinikiza pande mbili (wanunuzi
na wakulima) kujiunga na mpango huo pasipo hiari yao na kwamba kufanya hivyo ni kukiuka moja
kwa moja maazimio ya wadau wa sekta ya pamba.
Hata
hivyo, Mkuu wa mkoa pamoja na kukiri kutoa agizo la kukamatwa kwa wawekezaji
hao alikanusha sababu zilizotolewa na uongozi wa TACOGA.
Alisema
wawekezaji hao walikamatwa kutokana na kitendo chao cha kukiuka utaratibu wa
usambazaji wa pembejeo za kilimo katika upande wa viuatilifu ambapo walitakiwa
kuvisambaza kwa wakulima kwa njia ya mkopo na siyo kuwauzia.
0 Comments