Na Ameir Khalid
TUME za Mipango za Zanzibar
na Tanzania Bara zimeshauriwa kufanya
kazi kwa pamoja katika kupendekeza masuala mbali mbali yanayohusu utekelezaji
wa malengo ya melenia.
Wakizungumza katika mkutano wa siku moja
uliowashirikisha watendaji wa tume hizo na viongozi wa taasisi zisizo za
kiserikali, ambao uliofanyika ukumbi wa hoteli ya Bwawani Zanzibar, walisema
ushirikiano ndio utakaosaidia kutekeleza malengo ya millennia ifikapo 2015.
Mkutano huo ulikuwa na lengo la kujadili
ripoti ya Tanzania
yenye mwelekeo wa kuwa na ajenda moja baada ya utekelezaji wa malengo ya
maendeleo baada ya mwaka 2015.
Wajumbe hao walisema licha ya mafanikio
yaliyofikiwa katika mipango mbali mbali ya maendeleo, bado upo umuhimu mkubwa
wa tume hizo kushirikiana kwa karibu ili kuona malengo mengine yanafanikiwa.
Walisema licha kuwepo baadhi ya mambo yaliyofanikiwa
ikiwemo elimu, afya na barabara, lakini tatizo kubwa ni jinsi ya kupata huduma
bora kama vile madaktari wa kutosha, walimu wa sayansi na wananchi jinsi ya
kuweza kutumia miundombuni ya barabara katika kujileta maendeleo.
Walisema asasi za kiraia na serikali ni
vyema zikafanya kazi kwa pamoja katika kupanga mipango inayokusudiwa kufikishwa
Umoja wa Mataifa wakati wa vikao vyake, kwa kuzingatia kuwa, Zanzibar bado baadhi ya watu hawajafunzwa
kutumia miundombinu.
Mapema akiwasilisha mada katika mkutano
huo Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Biashara, Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy, alisema bara la Afrika bado
lipo nyuma katika kutekeleza malengo ya melinia.
Alisema tayari mikutano mingi imefanyika
kuanzia mwaka 2000 katika kujadili maendeleo, ambapo mikutano yote hiyo
imerahisisha kuleta ajenda ya maendeleo kwa nchi, ingawaje kuna tatizo la
utekelezaji wa mipango hiyo.
0 Comments