6/recent/ticker-posts

Dkt Shein Akutana na Balozi Mteule wa Tanzania, Sweden.

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                 21 Mei, 2014
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema bado kuna haja kubwa kwa mabalozi wa Tanzania nchi za nje kuendelea kuitangaza Tanzania kiuchumi kama ni hatua muhimu ya kutekeleza sera ya taifa ya uchumi na diplomasia.
Akizungumza na Balozi mteule wa Tanzania nchini Sweden Mheshimiwa Dora Msechu ambaye alifika Ikulu mjini Zanzibar kusalimiana na Rais wa Zanzibar, Dk. Shein amesema Sweden na nchi nyengine za Scandinavia kama vile Norway, Denmark na Finland zimejenga uhusiano mzuri na Tanzania kwa muda mrefu, jambo ambalo linatoa fursa nzuri kwa Tanzania kuwashajiisha wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta mbali mbali za kiuchumi na maendeleo.
Rais wa Zanzibar amesema Zanzibar inayo maeneo mengi ya kuwekeza na kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji kwa lengo la kuongeza kasi ya utekelezaji.
“Tumeimarisha miundombinu ya barabara, uwanja wa ndege na bandari miongoni mwa hatua ambazo Serikali imekuwa ikichukua kuwavutia wawekezaji” alisema.
Rais wa Zanzibar akiongeza kuwa kwa kuzungukwa na bahari kunaifanya Zanzibar kuwa na eneo pana la uwekezaji katika sekta ya uvuvi hasa wa bahari kuu lakini hadi sasa bado hapajawa na uwekezaji katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.
Kuhusu suala la utalii, Dk Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuiimarisha sekta hiyo na kwamba mafanikio yameanza kuonekana kutokana na ongezeko la idadi ya watalii wanaoingia nchini.
Alibainisha kuwa sekta hiyo ni miongoni mwa sekta ambazo zimeweza kuvutia wawekezaji wengi kutoka nje na kwamba bado kuna fursa zaidi za uwekezaji.
Mbali ya uwekezaji Dk. Shein alimuomba Balozi huyo mteule kuwashajiisha wananchi wa Sweden kufanya safari za kitalii kuitembelea Zanzibar ambayo alisema ina vivutio vingi zikiwemo sehemu za kihistoria na fukwe nzuri za bahari.
“Zanzibar kuna maeneo mengi ya kuvutia watalii kama vile fukwe za aina yake na sehemu nyingi za kihistoria, tunakusudia kuongeza idadi ya watalii kutoka idadi ya sasa ya watalii wapatao 181,000 kwa mwaka hadi kufikia watalii 500,000 ifikapo mwaka 2015” Dk. Shein alieleza.
Kwa upande wa kilimo, Rais wa Zanzibar alisema Zanzibar bado haijaanzisha maeneo makubwa ya kilimo kama ilivyo kwenye nchi zilizoendelea, ingawa dhamira ya kufanya hivyo ipo na yapo maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hizo za kilimo hasa kilimo cha umwagiliaji maji.
Kwa hiyo alimtaka Balozi Msechu kulizungumzia pia suala hilo kwa azma ya kuwaomba wawekezaji kutoka nchi anazoiwakilisha kuja kuwekeza kwenye eneo hilo.
Naye balozi Mteule aliahidi kuitangaza vyema Tanzania wakati wote atakapokuwa anatekeleza majukumu yake ya kazi nchini Sweden.



Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

Post a Comment

0 Comments