6/recent/ticker-posts

Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais

MUHTASARI WA HOTUBA YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS
KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
-------------------------

UTANGULIZI:
1.0        Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja kwamba Baraza lako Tukufu likae kama Kamati ya Mapato na Matumizi ili lipokee, lijadili na hatimae liidhinishe Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya   Makamu wa Pili wa Rais kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015.

2.0        Mheshimiwa Spika, tumekutana tena katika kikao hiki cha nne cha Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa kwa mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya kuzungumzia mipango na masuala muhimu ya nchi yetu kwa nia ya kuleta maendeleo ya nchi na wananchi wake.  Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uwezo huu wa kukutana tena na ninamuomba aendelee kutupa afya njema na kutuwezesha kuendesha kikao chetu hiki kwa hekima, busara na uadilifu mkubwa. Ni imani yangu kuwa tutamaliza kikao hiki tukiwa tunaendelea kubakia wamoja na wenye mshikamano mkubwa katika kuendeleza nchi yetu.

3.0        Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumshukuru kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuiongoza nchi yetu kwa umahiri na umakini mkubwa.  Sote ni mashahidi kuwa chini ya uongozi wa Dkt.  Ali Mohamed Shein, nchi yetu imeendelea kupata mafanikio makubwa katika nyanja zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa.  Aidha, nchi yetu imeendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu mkubwa hali ambayo imetoa nafasi kwa wananchi kuendelea na shughuli zao za maisha za kila siku bila bughudha wala usumbufu wowote. Namuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema na umri mrefu yeye na familia yake, amzidishie hekima na busara ili aendelee kutuongoza katika hatua za kuiletea nchi yetu maendeleo zaidi.

4.0        Mheshimiwa Spika, vile vile, nachukua nafasi hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuendelea kumsaidia na kumshauri vyema Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na  kwa  mashirikiano yake mazuri kwa Ofisi yangu.

5.0        Mheshimiwa Spika, pongezi za pekee nazitoa kwako wewe mwenyewe binafsi Mheshimiwa Spika, kwa jinsi unavyoliendesha Baraza letu hili kwa umahiri na umakini mkubwa kwa kufuata sheria na kanuni za Baraza. Uongozi wako wa busara kwa hakika umeimarisha demokrasia ndani ya Baraza na kulipa Baraza letu mafanikio makubwa katika kutekeleza majukumu yake. Tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu akuzidishie uwezo na hekima katika kutekeleza majukumu yako makubwa katika Taifa letu.  Pia napenda kuwapongeza kwa dhati Naibu Spika, Mhe. Ali Abdalla Ali Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini na Wenyeviti wa Baraza Mhe.  Mgeni Hassan Juma, Mwakilishi wa Viti Maalumu na Mhe. Mahmoud Mohamed Mussa, Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni kwa namna wanavyokusaidia katika kuliendesha Baraza letu hili.

6.0        Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii pia kuwashukuru Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi kwa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa malengo na maagizo mbali mbali wanayoyatoa kwa Wizara wanazozisimamia. Aidha, natoa shukrani maalum kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Mhe. Hamza Hassan Juma, Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura, Makamu Mwenyekiti, Mhe. Saleh Nassor Juma Mwakilishi wa Jimbo la Wawi na Wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa kuyapitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na kutupa ushauri unaotuongoza na kutusaidia katika utekelezaji wa malengo na majukumu ya Ofisi yetu.

7.0        Mheshimiwa Spika, pia nawapongeza Wajumbe wote wa Baraza hili Tukufu kwa kuipitisha Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Bajeti hiyo ndiyo itakayotuwezesha kuendesha kazi za Serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015.

8.0        Mheshimiwa Spika, maelezo ninayoyasoma hapa ni muhtasari wa hotuba yangu iliyomo katika kitabu changu cha hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015 kilichowasilishwa katika Baraza hili. Aidha, naomba maelezo yaliyomo katika kitabu hicho cha bajeti yaingie katika hansard kama yalivyo.

HALI YA SIASA:
9.0        Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijaalia nchi yetu amani na utulivu. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 hakukua na matukio makubwa ya uvunjifu wa amani yaliyotokea katika nchi yetu. Hali hii inatokana na wananchi wengi kuzidi kuelewa umuhimu wa amani na kushirikiana na Serikali yao kudumisha amani na utulivu kwa maendeleo ya Taifa letu na Ustawi wa jamii.  

10.0     Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, nchi yetu imefanya chaguzi ndogo mbili (2) ambazo zilihusisha Uchaguzi wa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Wilaya ya Magharibi Unguja na Uchaguzi wa Diwani Wadi ya Kiboje, Wilaya ya Kati Unguja. Tunavishukuru vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki katika chaguzi hizo ambazo ziliendeshwa kwa haki, uwazi, amani na utulivu mkubwa. Aidha, tunawapongeza sana viongozi walioshinda katika chaguzi hizo na tunawatakia mafanikio katika kuwatumikia wananchi waliowachagua na nchi yetu kwa ujumla. Vile vile, nachukua nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza sana wananchi wa Jimbo la Kiembesamaki  na wananchi wa Wadi ya Kiboje kwa kuweza kutumia demokrasia yao vizuri kuwachagua viongozi wao kwa imani ya kuwaletea maendeleo katika maeneo yao.

MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR:
11.0     Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha, nchi yetu imeadhimisha Miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Maadhimisho ya Sherehe hizo yalizinduliwa rasmi tarehe 15 Agosti, 2013 na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein na kufikia kilele chake tarehe 12 Januari, 2014, Uwanja wa Amani, Zanzibar.

12.0     Mheshimiwa Spika, kwa muda wote wa maadhimisho haya hadi siku ya kilele tumeshuhudia shughuli na matukio mbali mbali ambayo wananchi na viongozi walishiriki kikamilifu katika maeneo yote ya Unguja na Pemba. Miongoni mwa matukio hayo ni Maonesho ya Miaka 50 ya Mapinduzi yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), Kampasi ya Beit el Ras kuanzia tarehe 2 – 5 Januari, 2014; Maonesho ya Fensi; Maonesho ya Biashara yaliyofanyika katika viwanja vya Maisara; Utoaji wa Nishani kwa viongozi na wananchi mbalimbali waliotoa mchango wao katika Mapinduzi ya Januari 12, 1964 pamoja na waliochangia katika maendeleo ya Zanzibar kwa jumla.  Pia palifanyika Matamasha ya Michezo na Burudani, Ujenzi wa Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo Michenzani, Uwekaji wa jiwe la msingi na uzinduzi wa miradi ya maendeleo mbali mbali.  Na mwisho maonesho mbali mbali yaliyofanywa siku ya kilele katika Uwanja wa Amani.

13.0     Mheshimiwa Spika, sote ni mashahidi wa namna sherehe zetu hizi zilivyokuwa zimefana sana na kuleta haiba kubwa kwa nchi yetu. Hii imeonesha jinsi gani wananchi wetu wanavyoyathamini Mapinduzi yetu ya Januari 1964 pamoja na maendeleo wanayoyaona kutokana na Mapinduzi hayo.

14.0     Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako napenda kutoa pongezi na shukurani zangu za dhati kwa wananchi na viongozi wote walioshiriki kwa njia moja au nyengine katika kufanikisha Maadhimisho ya Sherehe hizo. Ni matumaini yangu kuwa sote kwa umoja wetu tutaendelea kudumisha Mapinduzi haya ili kuendeleza amani na maendeleo katika nchi yetu.

15.0     Mheshimiwa Spika, pamoja na kutoa pongezi hizo, naomba kutoa masikitiko yangu kuona kwamba hadi leo hii wapo watu wachache miongoni mwetu ambao wanauliza uhalali wa Mapinduzi Matukufu ya Mwaka 1964. Ni dhahiri kwamba hata hawa wanaohoji uhalali wa Mapinduzi kwa kiasi kikubwa wamefaidika na Mapinduzi haya.  Mwenye macho haambiwi tazama kwani ni baada ya Mapinduzi ya 1964 ndio nchi hii imeshuhudia mafanikio makubwa ya maendeleo katika nyanja zote. Hivyo, hatuna budi kuyalinda na kuyaendeleza Mapinduzi yetu kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo.

16.0     Mheshimiwa Spika, dhana ya Mapinduzi ilikuwa ni kuleta maisha bora kwa kila Mzanzibari na kuondoa ubaguzi wa aina zote na kuleta umoja na maendeleo na ndio kilichofanyika. Haya mengi ambayo leo tunayaona hayakuwepo kabla ya Mapinduzi ambayo ni pamoja na kuwepo kwa nyumba bora za kuishi, nyumba bora kwa wazee, kuimarika kwa huduma za elimu, afya na kupatikana kwa maendeleo makubwa katika Sekta ya Miundombinu, Kilimo, Maji na Umeme, Uchumi na Biashara, na kuwepo kwa uhuru wa kushiriki shughuli za kisiasa.

17.0     Mheshimiwa Spika, naomba tuelewe kwa nini tunatoa kipaumbele katika kuweka kumbukumbu za Mapinduzi hasa katika maadhimisho yake. Kwa kweli ni jambo la ajabu kuona miongoni mwetu bado wapo watu wanaohoji umuhimu wa Sherehe za Mapinduzi au kuweka vielelezo vya Mapinduzi. Tunasema tutaendelea kuenzi na kuheshimu kazi nzuri iliyofanywa na Wazee wetu ya kutukomboa na kutupatia Uhuru wa nchi yetu.

18.0     Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya kuweka kumbukumbu ya kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi, Serikali kwa makusudi imefanya uamuzi wa kujenga Mnara katika eneo la Michenzani. Hii inatokana na historia ya eneo hilo katika harakati za kuikomboa nchi yetu. Aidha, Serikali ina dhamira ya dhati ya kuendeleza azma ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kuendeleza eneo hilo na kulifanya kuwa eneo la biashara na kuwa kivutio kwa wageni, watalii na wananchi kwa ujumla.

19.0     Mheshimiwa Spika, mnara unaoendelea kujengwa utakuwa pia ni kituo kwa wananchi na wageni kusoma historia ya Mapinduzi na waanzilishi wake kwani kutakuwa na maktaba maalum. Katika eneo hilo kutakuwa na mkahawa na bustani ya mapumziko ambayo itasaidia sana kupunguza msongamano katika maeneo ya Forodhani hasa wakati wa sikukuu. Naomba wananchi waelewe kuwa mnara huo unajengwa kwa fedha za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) na utaendeshwa kibiashara na kwa faida.


MASUALA YA MUUNGANO:
20.0     Mheshimiwa Spika, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hivi sasa umetimiza miaka 50 (Nusu Karne) tangu ulipoasisiwa tarehe 26 Aprili, 1964. Sherehe za kutimiza miaka 50 ya Muungano wetu zilizinduliwa rasmi hapa Zanzibar na Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tarehe 01 Machi, 2014 katika Ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani na kilele chake kilifanyika Dar es salaam tarehe 26 Aprili, 2014.  Kipindi cha miaka 50 ni kirefu na nchi yetu ina kila sababu za kujivunia kutokana na kuudumisha Muungano wetu kwa kipindi chote hicho. Yapo mafanikio mengi yanayotokana na Muungano, lakini makubwa kati ya mafanikio hayo ni kuwa na amani na utulivu katika nchi yetu. Aidha, Muungano huu umeweza kutoa fursa ya kuendeleza na kuimarisha mahusiano ya kidugu yaliyopo kati ya wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.

21.0     Mheshimiwa Spika, licha ya kuwa na mafanikio hayo, Muungano wetu huu umekuwa na changamoto katika baadhi ya maeneo ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele na wananchi wa pande zote mbili za Muungano.  Juhudi kubwa tayari zimechukuliwa na viongozi wetu katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo ili kuimarisha Muungano wetu huu wa kihistoria. Mambo ambayo mpaka sasa yameshapatiwa ufumbuzi kupitia Kamati Maalumu inayoongozwa na Mhe. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kama yafuatayo:-

·         Utekelezaji wa Sheria ya Haki za Binaadamu.
·         Utekelezaji wa “Merchant Shipping Act” katika Jamhuri ya Muungano na uwezo wa Zanzibar kujiunga na Shirika la Kimataifa la Usafiri Baharini [International Maritime Organisation (IMO)].
·         Misamaha ya mikopo ya fedha kutoka IMF.
·         Uwezo wa Zanzibar kukopa ndani na nje nchi.
·         Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo wa SMT.
·         Kodi ya Mapato (Mgao wa Mapato yatokanayo na PAYE).

22.0     Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo ambayo yameshapatiwa  ufumbuzi  kuna mambo ambayo yapo katika hatua nzuri ya kupatiwa ufumbuzi,  mambo hayo ni kama yafuatayo:-
·         Mgawanyo wa mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu.
·         Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
·         Ushirikiano wa Zanzibar na Taasisi za nje.
·         Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano.
·         Usajili wa vyombo vya moto.
·         Tume ya Pamoja ya Fedha.
·         Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

MASUALA YA KIUCHUMI NA KIJAMII:
23.0     Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu hii nimegusia masuala mbali mbali ya kiuchumi na kijamii ikiwemo hali ya uchumi na mipango ya Serikali katika kuimarisha uchumi, uwezeshaji wananchi kiuchumi, Sekta ya huduma ya kiuchumi, Sekta ya huduma ya kijamii, masuala ya migogoro ya ardhi, masuala mtambuka pamoja na Sekta ya utumishi na maslahi ya wafanyakazi. Masuala haya yameelezwa kwa kina kuanzia ukurasa 12 mpaka ukurasa wa 24 katika hotuba ya makadirio.


MWELEKEO WA VIPAUMBELE VYA OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015:
24.0     Mheshimiwa Spika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais katika kutekeleza majukumu yake katika mwaka wa fedha 2014/2015 imejipangia kutekeleza vipaumbele vifuatavyo:-

         i. Kuimarisha huduma za usafiri na makaazi ya Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais.
        ii. Kuongeza hadhi katika Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa.
       iii. Kujenga uwezo wa kiutendaji kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa kuwapatia mafunzo na vitendea kazi.
       iv. Kujenga uwezo wa jamii katika kujikinga, kukabiliana na kuhimili majanga na maafa.
        v. Kushughulikia malalamiko na migogoro ya wananchi kwa kushirikiana na Sekta husika.
       vi. Kusimamia masuala ya utafiti kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa vya Utafiti (National Research Agenda).
     vii. Kuweka Muundo mpya wa Kitaasisi na Kiutumishi wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Dar es Salaam utakaoongeza ufanisi na tija.
    viii. Kuongeza mapato yatokanayo na kuongezeka kwa huduma za upigaji chapa.
       ix. Kuandaa mazingira bora kwa ajili ya kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa 2015, ikiwemo kutoa elimu ya wapiga kura, kufanya uchunguzi wa idadi, majina na mipaka ya majimbo na kufanya mapitio ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, na
        x. Kuendesha mikutano ya Baraza la Wawakilishi na kusimamia kazi za Kamati za Kudumu za Baraza.

UTEKELEZAJI WA MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014 NA MALENGO YALIYOPANGWA KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015:
25.0     Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Taasisi zake ilikadiriwa kutumia jumla ya Shs: 30,066,506,000. Kati ya hizo Shs: 22,094,970,000 ni kwa kazi za kawaida na Shs: 7,971,536,000 ni kwa kazi za maendeleo. Hadi kufikia mwezi Machi 2014, Ofisi iliingiziwa Shs: 19,416,893,755 (sawa na asilimia 65). Kati ya hizo Shs: 15,837,895,300 ni kwa kazi za kawaida (sawa na asilimia 72) na Sh. 3,578,998,455 kwa kazi za maendeleo (sawa na asilimia 45). (Kiambatanisho Nam. 1A na 1B).

26.0     Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa taarifa za jumla za utekelezaji kifedha kwa mwaka 2013/2014, sasa naomba kutoa taarifa za utekelezaji kwa kila Idara na Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.

OFISI YA FARAGHA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS:
27.0     Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Faragha ina jukumu la kutoa huduma zote muhimu kwa Mhe.  Makamu wa Pili wa Rais na familia yake pamoja na kutunza makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais yaliyoko Mazizini Unguja, Dar es Salaam na Dodoma.

28.0     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Sh. 780,034,000 kwa Idara ya Faragha.  Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Sh. 317,824,974 kwa ajili ya kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 41.

29.0     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 Ofisi ya Faragha imetekeleza kazi mbali mbali ikiwemo:-

      i.    Ununuzi wa vifaa kwa matumizi ya ofisi.
     ii.    Kufanya matengenezo madogo madogo kwa makaazi ya Mhe. Makamu wa Pili wa Rais.
   iii.    Kuratibu mikutano ya Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais na Mabalozi na Wana Diplomasia wengine.
   iv.    Kuratibu ziara  za ndani na nje ya nchi za Makamu wa Pili wa Rais.
     v.    Kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais.

30.0     Mheshimiwa Spika katika mwaka wa fedha 2014/2015 Ofisi ya Faragha imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-

         i. Kuimarisha Ofisi ya Faragha ya Makamu wa Pili wa Rais kwa ununuzi wa gari moja, samani na vifaa vya ofisi.
        ii. Kuratibu ziara 20 za ndani ya nchi na mbili za nje ya nchi za Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais.
       iii. Kuwajengea uwezo wafanyakazi wawili (2) wa Idara kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu pamoja na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi wanne (4).
       iv. Kuimarisha makaazi ya Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais kwa kuzifanyia matengenezo nyumba za Mazizini, Dar es Salaam na Dodoma.
        v. Kuimarisha uhusiano na ushirikiano na nchi na Taasisi mbali mbali za ndani, kikanda na kimataifa.

31.0      Mheshimiwa Spika, ili Ofisi ya Faragha iweze kutekeleza malengo yake kwa mwaka wa fedha 2014/2015 naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shs: 483,116,224 kwa matumizi ya Ofisi. Kati ya hizo Shs: 330,616,224 kwa malipo ya mishahara, posho za wafanyakazi na michango ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Shs: 152,500,000 kwa matumizi mengineyo.


IDARA YA UENDESHAJI NA UTUMISHI:
32.0     Mheshimiwa Spika, Idara ya Uendeshaji na Utumishi ina wajibu wa kusimamia stahiki za watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na kusimamia mafunzo kwa wafanyakazi. Aidha, Idara ina jukumu la kusimamia usalama na mazingira bora ya kazi pamoja na uendeshaji wa kazi za kila siku za Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.

33.0     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Shs: 1,004,880,000 kwa Idara ya Uendeshaji na Utumishi. Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Shs:  577,298,515 kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 57.

34.0     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Idara ya Uendeshaji na Utumishi imetekeleza kazi mbali mbali ikiwemo:-
               i.      Kuratibu na kuwalipia ada na gharama nyengine za masomo wafanyakazi wanaoendelea na masomo ndani na nje ya nchi. (Kiambatanisho Nam. 2).
              ii.      Kulipia stahiki za wafanyakazi zikiwemo likizo, malipo baada ya saa za kazi na kutayarisha mafao kwa watumishi waliostaafu.
             iii.      Kufanya semina elekezi kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011.
             iv.      Ununuzi wa vifaa kwa matumizi ya Ofisi.

35.0     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Idara ya Uendeshaji na Utumishi imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
           i.Kuweka mazingira mazuri ya kazi za idara kwa ununuzi wa vifaa vya ofisi, samani pamoja na kulipia gharama za umeme na mawasiliano na utunzaji wa majengo.

          ii.Kuwajengea uwezo wafanyakazi kumi (10) wa idara kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu pamoja na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi tisa (9).

         iii.Kuufanyia mapitio Mpango wa Mafunzo kwa wafanyakazi pamoja na kuandaa utaratibu wa kutathmini utendaji kazi (Staff Appraisal System) na upandishaji vyeo wafanyakazi kwa kufuata muundo wa utumishi (Scheme of Service).

         iv.Kusimamia matumizi bora ya fedha na vifaa vya ofisi kwa kuandaa vikao vinne (4) vya Kamati ya Uongozi, vikao vinne (4) vya Bodi ya Zabuni, Vikao vinne (4) vya Kamati ya Ukaguzi wa ndani na kulifanyia mapitio Daftari la Mali za Serikali (Asset Registry).

36.0     Mheshimiwa Spika, ili idara ya Uendeshaji na Utumishi iweze kutekeleza malengo yake kwa mwaka wa fedha 2014/2015 naliomba Baraza lako tukufu liidhinishe jumla ya Shs: 704,166,316. Kati ya hizo Shs: 514,166,316 ni kwa malipo ya mishahara, posho na mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Shs: 190,000,000 ni kwa matumizi mengineyo.

IDARA YA MIPANGO, SERA NA UTAFITI :
37.0     Mheshimiwa Spika, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti inaendelea na jukumu la kusimamia masuala ya mipango, bajeti, sera na utafiti.  Pia Idara hii ina jukumu la kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kutayarisha ripoti za utekelezaji wa shughuli za kawaida na miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miezi mitatu, miezi sita, miezi tisa  na mwaka mzima.

38.0     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Shs: 295,240,000 kwa Idara ya Mipango, Sera na Utafiti. Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Shs: 125,771,732 kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 43.

39.0     Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 Idara ya Mipango, Sera na Utafiti imetekeleza kazi mbali mbali ikiwemo:-
           i.Ununuzi wa vifaa kwa matumizi ya Ofisi.

          ii.Kufanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo iliyo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.

         iii.Kuratibu utekelezaji wa Miradi ya Mfuko wa Dunia (Global Fund) ya Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria.

         iv.Kuandaa Mpango Mkakati wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.

          v.Kutoa vibali  vya kufanya utafiti na kuratibu vikao vya Kamati ya Taifa ya Utafiti.

         vi.Idara kwa kushirikiana na COSTECH imeratibu kikao cha Kamati ya Taifa ya Wataalamu ya Rasilimali za Asili juu ya kupitia vipaumbele vya utafiti (National Research Agenda).  Aidha, kwa kushirikiana na COSTECH, SUZA na Chuo Cha Sayansi ya Afya imeratibu na kushiriki Siku ya Utafiti na Ugunduzi ikiwa ni moja ya shughuli za maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

40.0     Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 Idara ya Mipango, Sera na Utafiti imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
         i.  Kuweka mazingira mazuri ya kazi za idara kwa ununuzi wa vifaa vya ofisi na samani.

          ii.Kuwajengea uwezo wafanyakazi 11 wa idara kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na wafanyakazi watatu (3) kwa mafunzo ya muda mrefu na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi watatu (3).

         iii.Kuufanyia mapitio Mpango Mkakati wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na kutayarisha Miradi mitatu ya Maendeleo.

         iv.Kuandaa Bajeti  kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016 na kufanya ziara nne (4) za ufuatiliaji wa kazi za Wizara na  utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.

          v. Kuandaa vikao 12 vya Kamati ya Kisekta  ya kuidhinisha Tafiti mbali mbali na vikao vinne vya Kamati ya Taifa ya Kutafiti Rasilimali za Asili.

         vi. Kwa kushirikiana na COSTECH kuwajengea uwezo watafiti wa Wizara za SMZ kwa kuandaa warsha mbili pamoja  na kuweka  utaratibu mzuri wa utoaji wa vibali vya Utafiti.

       vii.Kuratibu utekelezaji wa Miradi ya Mfuko wa Dunia (Global Fund) ya Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria

41.0     Mheshimiwa Spika, Ili Idara ya Mipango, Sera na Utafiti iweze kutekeleza malengo yake katika mwaka wa fedha 2014/2015 naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shs: 184,007,400 kwa matumizi ya Idara.  Kati ya hizo Shs: 100,718,400 kwa ajili ya malipo ya mishahara, posho za wafanyakazi na mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Shs: 83,289,000 kwa matumizi mengineyo.


IDARA YA URATIBU WA SHUGHULI ZA SERIKALI:
42.0     Mheshimiwa Spika, Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali ina jukumu la kuratibu Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Shughuli za Muungano ndani ya Zanzibar.

43.0     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Shs: 397,530,000 kwa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali. Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Shs: 223,282,110 kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 56.  Aidha, Idara iliidhinishiwa Shs: 840,000,000 kwa kazi za maendeleo ikiwa ni mchango wa SMZ. Kati ya hizo Shs: 80,000,0000 ni kwa Mradi wa TASAF na Shs: 760,000,000 kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo. Hadi kufikia Machi, 2014, Idara imeingiziwa Shs: 25,000,000 kwa mradi wa TASAF, sawa na asilimia 31.

44.0     Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 Idara imetekeleza kazi mbali mbali ikiwemo:-

    i.      Kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010 – 2015 katika Wizara za SMZ na Mikoa yote ya Unguja na Pemba.

   ii.      Kupokea na kuyafuatilia malalamiko ya wananchi yaliyowasilishwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
 iii.      Kufuatilia vikao vya Baraza la Wawakilishi.

 iv.      Kuratibu vikao  vya mashirikiano baina ya Wizara za SMZ na SMT.

   v.      Kusimamia utekelezaji wa mradi wa TASAF Awamu ya Tatu (Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini) na kaya masikini 2,675 kwa Unguja na Kaya 4,084 kwa Pemba  zimepatiwa malipo kwa awamu mbili (Januari na Machi 2014). Jumla ya Shs: 432,259,000 zimelipwa kwa Unguja na Pemba. (Kiambatanisho Nam. 3A-3F).

 vi.      Kutoa mafunzo maalumu kwa wawezeshaji 120 kutoka Wilaya zote za Unguja na Pemba (Unguja 60 na Pemba 60) wa kuibua kaya masikini.

vii.      Kufuatilia utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.

45.0      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 Idara imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
    i.      Kuweka mazingira mazuri ya kazi za Idara kwa ununuzi wa vifaa vya ofisi na samani.

   ii.      Kuwajengea uwezo wafanyakazi wanne (4) wa Idara kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu pamoja na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi saba (7).

 iii.      Kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuandaa Taarifa ya utekelezaji kwa kipindi cha Miaka miwili kuanzia Oktoba 2012 – Septemba 2014.

 iv.      Kufuatilia utekelezaji wa Ahadi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa kwa kila robo mwaka.

   v.      Kupokea na kufuatilia malalamiko ya wananchi na kusimamia utatuzi wa migogoro katika jamii.

 vi.      Kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo katika majimbo 50 ya Unguja na Pemba ambayo yamepatiwa fedha.

vii.      Kufuatilia mijadala na utekelezaji wa Ahadi za Serikali zinazotolewa katika vikao vya Baraza la Wawakilishi.

viii.      Kuratibu vikao  saba (7) vya mashirikiano kati ya Wizara za SMZ na SMT.

 ix.      Kuratibu vikao vinne (4) vya Mawaziri na Makatibu Wakuu wa SMZ na SMT na vikao vinne (4) vya Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja ya Mambo ya Muungano.

   x.      Kusimamia utoaji wa fedha (Cash Transfer) kwa Kaya masikini za Unguja na Pemba zinazotolewa kupitia Mpango wa TASAF awamu ya Tatu.
 xi.      Kuimarisha kitengo cha ICE kwa ununuzi wa vifaa vipya na kutoa mafunzo kwa watendaji sita wa Kitengo.

46.0     Mheshimiwa Spika, Ili Idara iweze kutekeleza majukumu yake kwa mwaka 2014/2015 naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shs: 344,638,000. Kati ya fedha hizo Shs: 247,053,000 kwa malipo ya mishahara, posho za wafanyakazi na mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Shs: 97,585,000 kwa matumizi mengineyo. Kwa upande wa Miradi ya Maendeleo naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shs: 1,060,000,000. Kati ya hizo Shs: 1,010,000,000 kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo na Shs: 50,000,000 mchango wa Serikali kwa ajili ya Miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF awamu ya Tatu.


IDARA YA URATIBU WA SHUGHULI ZA SMZ, DAR ES SALAAM:
47.0     Mheshimiwa Spika, Idara ya Uratibu wa Shughuli za SMZ Dar es Salaam imehamishiwa rasmi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais tangu mwezi wa Septemba, 2013. Kabla ya hapo Idara hii ilikuwa chini ya Iliyokuwa Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo.

48.0     Mheshimiwa Spika, Idara hii ina jukumu la kuratibu kazi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huko Tanzania Bara.  Aidha, Idara inaratibu masuala ya SMZ na Ofisi za Balozi mbali mbali zilizopo Tanzania, Wadau wa Maendeleo pamoja na Mashirika ya Kimataifa yenye ofisi zao Dar es Salaam.

49.0     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Shs: 326,970,000 kwa Idara ya Uratibu wa Shughuli za SMZ Dar es Salaam. Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Shs: 119,053,550 kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 36.

50.0     Mheshimiwa Spika, Idara ya Uratibu wa Shughuli za SMZ - Dar es Salaam katika mwaka wa fedha 2013/2014 imetekeleza kazi mbali mbali ikiwemo:-
 i.      Kushiriki kwenye Mkutano wa Nane wa Tume ya pamoja ya Ushirikiano wa kiuchumi, kiufundi na Sayansi baina ya Tanzania na India. 

   ii.      Kushiriki katika kikao cha mashauriano baina ya Tanzania na Japan, ambapo Zanzibar iliwasilisha mapendekezo ya miradi saba kupitia Tume ya Mipango Tanzania Bara kwa ajili ya kuombewa misaada kutoka Serikali ya Japan (TICAD V).

 iii.      Kushiriki katika matayarisho ya Mkutano Mkuu wa Mawaziri unaojadili masuala ya kiuchumi ambao ulifanyika nchini Kenya.

51.0     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 Idara ya Uratibu wa shughuli za SMZ Dar es Salaam imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
           i.Kuweka mazingira mazuri ya kazi za Idara kwa ununuzi wa vifaa vya ofisi na samani.

          ii.Kuwajengea uwezo wafanyakazi watatu (3) wa Idara kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu pamoja na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi tisa (9).

         iii.Kuandaa Muundo mpya wa Kitaasisi na Kiutumishi wa Idara utakaoleta ufanisi zaidi na tija.

         iv.Kuimarisha mashirikiano baina ya Idara na Taasisi za SMZ na Taasisi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Ofisi za Kibalozi na Taasisi za Kimataifa.

52.0     Mheshimiwa Spika, ili Idara ya Uratibu wa Shughuli za SMZ Dar es Salaam iweze kutekeleza malengo yake katika mwaka wa fedha 2014/2015 naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shs: 353,178,160.   Kati ya hizo Shs: 208,178,160 kwa ajili ya malipo ya mishahara, Posho za wafanyakazi na mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Shs: 145,000,000 kwa matumizi mengineyo.

IDARA YA KUKABILIANA NA MAAFA:
53.0     Mheshimiwa Spika, Idara ya Kukabiliana na Maafa ina jukumu la kuratibu masuala ya maafa hapa Zanzibar, kama ilivyoelezwa katika Sheria ya Kukabiliana na Maafa Nam. 2 ya mwaka 2003.

54.0     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Baraza lako Tukufu liliidhinisha jumla ya Shs: 262,528,000 kwa Idara ya Kukabiliana na Maafa kwa kazi za kawaida. Hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Idara iliingiziwa jumla ya Shs: 112,283,620 kwa kazi za kawaida ambazo ni sawa na asilimia 43. Kwa upande wa miradi ya maendeleo Idara iliidhinishiwa Shs: 340,000,000. Kati ya hizo Shs: 70,000,000 ni mchango wa Serikali na Shs: 270,000,000 ni mchango kutoka kwa Washirika wa Maendeleo na hadi kufikia mwezi wa Machi 2014, Idara imeingiziwa Shs: 10,000,000 kutoka mchango wa Serikali sawa na asilimia 14. na Shs: 175,176,000 kutoka  kwa Washirika wa Maendeleo sawa na asilimia 65.

55.0     Mheshimiwa Spika, Idara ya Kukabiliana na Maafa katika mwaka fedha wa 2013/2014 imetekeleza kazi mbali mbali ikiwemo: -
        i.  Kutayarisha na kurusha vipindi vya kukabiliana na maafa kwa lengo la kuelimisha jamii kupitia ZBC Radio.

       ii.  Kutoa mafunzo ya kukabiliana na maafa kwa Shehia 36 zilizofanyiwa tathmini ya kujua uwezo wa kukabiliana na maafa katika Wilaya za Magharibi, Mjini na Kaskazini ‘A’ (Kiambatanisho Nam. 4A & 4 B).

     iii.  Kutoa elimu ya kukabiliana na maafa kwa watu wenye ulemavu na wanafunzi wa skuli za msingi na Sekondari katika Wilaya za Mjini na Kaskazini ‘A’ Unguja na Chake Chake na Mkoani Pemba.

     iv.  Kukamilisha Mipango ya Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa kwa Wilaya za Mjini, Magharibi na Kaskazini ‘A’. 

56.0     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Idara imepanga kutekeleza malengo yafuatayo: -

        i.  Kuweka mazingira mazuri ya kazi za Idara kwa ununuzi wa vifaa vya ofisi na samani.

       ii.  Idara kwa kushirikiana na Washirikia wa Maendeleo (USAFRICOM, Benki ya Dunia na Kamisheni ya Bahari ya Hindi) itaendesha mafunzo mbali mbali ya kukabiliana na maafa kwa watendaji na wadau wa kukabiliana na maafa pamoja na kuendesha mazoezi mawili (2) ya kukabiliana na maafa.

     iii.  Kuwajengea uwezo wafanyakazi wanne (4) wa Idara kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu pamoja na kulipa stahiki za likizo kwa wafanyakazi sita (6).

     iv.  Kuyafanyia matengenezo maghala mawili (2) na kununua vifaa vya kukabiliana na maafa kwa Unguja na Pemba.

       v.  Kujenga uwezo kwa jamii katika kukabiliana na majanga na maafa kwa Shehia 10.

     vi.  Kukamilisha sheria mpya ya kukabiliana na maafa.

57.0     Mheshimiwa Spika, ili Idara ya Kukabiliana na Maafa iweze kutekeleza malengo yake katika mwaka wa fedha 2014/2015, naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shs: 298,447,800 kwa matumizi ya Idara. Kati ya hizo Shs: 128,875,500 kwa ajili ya malipo ya mishahara, posho za wafanyakazi na mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Shs: 169,572,300 kwa matumizi mengineyo. Aidha, naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shs: 1,322,880,000 kwa ajili ya Miradi ya maendeleo, Shs: 40,000,000 ikiwa ni mchango wa Serikali na Shs: 1,282,880,000 ni mchango kutoka washirika wa Maendeleo.

IDARA YA SHEREHE NA MAADHIMISHO YA KITAIFA:
58.0     Mheshimiwa Spika, Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa ina jukumu la kuratibu Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa pamoja na shughuli za kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa. Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa yanayoratibiwa na Idara ni Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na ushiriki wa Viongozi na wananchi wa Zanzibar katika Sherehe za Uhuru wa Tanganyika. Aidha, kwa upande wa shughuli za kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa, Idara inaratibu mazishi ya Viongozi kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Kuwaenzi Viongozi Nam. 10 ya Mwaka 2002, Hitma na Dua ya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na kutunza kumbukumbu za viongozi hao.
...

Post a Comment

0 Comments