Na
Amina Mmanga, Pemba
UONGOZI
wa uwanja wa ndege Pemba, umeziomba mamlaka husika kuwapatia mashine maalumu za
ukaguzi wa mizigo na abiria, ili kuepusha mizigo ya abiria kupekuliwa kwa
mikono, kitendo ambacho huwakera abiria.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, Meneja wa uwanja huo, Rajab Ali Massoud, alisema
tabia ya wafanyakazi wa uwanja huo kupekua mizigo kwa kuifungua, huwaudhi
abiria wengi na wakati mwengine kutoa lugha zisizo nzuri.
Alisema
kwa sasa wafanyakazi hao huwalazimu kuifungua mizigo ya abiria na kupekua na
wakati mwengine husababisha migogoro na abiria.
Alisema
wakati umefika kwa serikali kuharakisha ununuzi wa mashine hizo ili kuwa na
uhakika wa kile kinachopitisha badala ya kuangalia mizigo kwa macho na mikono
mitupu.
“Hivi
sasa wafanyakazi wa uwanja huu wanalazimika kutumia mikono wakati wa kupekua
mizigo ya abiria wanaosafiri kwa ndege, lakini tukipata mashine ndio
suluhisho,” alisema.
Aidha
alisema kuwepo uhaba wa wafanyakazi pamoja na baadhi ya vitendea kazi husababisha
kutokufanya kazi zao kwa ufanisi.
Alisema
kuanzia mwaka 2013-2014 idadi ya abiria wanaotumia uwanja huo imeongezeka kutokana
na safari za ndege kuongezeka.
Mkuu
wa ulinzi na usalama,Ali Sudi Ali, alisema ukosefu wa wafanyakazi pamoja na
mashine ya kukagulia mizigo ya abiria ni kikwazo katika uwanja huo.
Alisema
juhudi za kiomba serikali zimeshachukuliwa na hivi karibuni wanatarajiwa
kupatiwa kifaa hicho lakini ni vyema serikali kuharakisha upatikanaji wa kifaa
hicho.
1 Comments
Ukosefu Wa wafanyakazi??!! Mbona kuna vijana wengi wamemaliza vyuo vikuu hawana ajira? Si muwaajiri?
ReplyDelete