Na Hashim Mlenge
KATIBU Mwenezi wa CCM Wilaya ya Maghribi Unguja, Muhija Haji Kombo amewataka wanachama wa chama hicho, kukichagua kwa kukipigia kura nyingi za ndio ili kiweze kuiongoza nchi kwa lengo la kuleta maendeleo.
Aliyasema hayo huko katika kiwanja cha Maungani wakati wa mkutano wa kampeni za chama hicho jimbo la Fuoni na kuwatambulisha wagombea wa chama hicho kwa nafasi ya Uwakilishi ,Ubunge na Udiwani.
Katibu huyo alisema kuwa CCM ndio chama pekee hapa nchini kutokana na kuwa na sera na ilani nzuri zenye kutekelezeka pamoja na kusimamisha wagombea wenye sifa katika nafasi ya Urais hadi majimboni .
Aliwafahamisha wanachama wa jimbo la Fuoni kuwa suala la maridhiano ya kisiasa kati ya ya chama hicho na CUF, yamefanyika kutokana na kukubaliwa na Serikali inayoongozwa na CCM na pia jambo hilo halihusiani na kugawana majimbo.
Alitoa wito kwa wanachama na wapenzi wa chama hicho kuwa mstari wa mbele siku ya tarehe 31 Oktoba katika vituo vyao vya kupigia kura walivyojiandikisha ili kuweza kutekeleza kwa vitendo kazi hiyo ili chama chao kiweze kuondoka kidedea na kutekelezewa ahadi walizoahidiwa.
Muhaji aliwatambulisha wagombea hao kupitia chama hicho kwa wananchi wa jimbo hilo la Fuoni kwa upande wa nafasi Uwakilishi ni Thuwaiba Kisasi, huku nafasi ya Ubunge akiwa ni Said Mussa Zubeir "Obama" na nafasi ya udiwani wadi ya Kijitoupele ni Jailan Kombo wakati wadi ya Fuoni ni Shaka Hamdu Shaka.
Aidha akiomba ridhaa kwa Wananchi hao mgombea Ubunge jimboni humo Said Mussa Zubeir aliwataka wanachama na wananchi wa jimbo hilo kumpa ridhaa siku ya kupiga kura kwa kumchagua kwa kura nyingi ili aweze kuwatekelezea ahadi alizowaahidi.
Zuibeir alifahamisha kuwa iwapo wananchi na wanachama wa jimbo hilo watampa ridhaa hiyo ataendeleza pale palipoachwa na viongozi waliopita kwa kuwatatulia kero zao ambazo zinazowakabili ikiwemo kujenga kituo cha Afya na Polisi katika maeneo ya Maungani.
Huku akisema licha hayo pia wanakusudia kuendeleza sekta ya elimu kwa kuwaendeleza wanafunzi wa jimbo hilo ili kuweza kutoa wanafunzi wenye sifa na kuzishinda skuli nyengine ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya sayansi na tekonolojia.
Nae Mgombea wa kiti cha Uwakilishi, Thuwaiba Kisasi, amesema hana wasi wasi wa ushindi na kuwataka wananchi na wanachama wa jimbo hilo kuwachagua viongozi wote wa CCM ili wapatiwe maendeleo ya haraka.
No comments:
Post a Comment