Aeleza mafanikio ya soka yanahitaji uongozi bora
Asema kwa ushirikiano, usimamizi mzuri yote yawezekana
Haoni sababu Zanzibar kutong'ara tena kisoka
Na Salum Vuai, Maelezo
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amekishauri Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kuelekeza nguvu katika kuleta maendeleo ya soka nchini kwa kuwa na usimamizi mzuri katika utendaji wake.
Akizungumza na wadau wa michezo katika hafla ya kuichangia timu ya taifa Zanzibar Heroes iliyofanyika hoteli ya Zanzibar Beach Resort juzi, Dk. Shein alisema wapenzi wa mpira wa miguu hawapendi kuziona timu zao zikikosa fursa za kujiendeleza kwa sababu tu ya mivutano inayotokana na uongozi mbovu.
Alisema Zanzibar inahitaji uongozi wa michezo ambao umejidhatiti kikamilifu kwa ajili ya ufanisi wa timu za nchi hiyo sambamba na uangalizi wa kutosha katika klabu za ndani.
"Tunapaswa kutambua thamani ya soka katika utamaduni wetu wa taifa, na umuhimu wake kwa maendeleo ya uchumi, umoja wa kitaifa na uhusiano wa kimataifa", alisisitiza Rais Shein.
Aidha aliongeza kuwa kadiri wadau na viongozi wa sekta ya michezo wanavyotaraji kuona matunda mazuri kutokana na wachezaji wa hapa, ni jukumu lao pia kuwapa nyenzo na kuwaunga mkono.
Dk. Shein alieleza kuwa, ni imani yake kwamba msaada unaotolewa na kampuni zilizoandaa hafla hiyo, utasaidia kuipanga upya ZFA ili kuwa chombo ambacho timu ya taifa 'Zanzibar Heroes', wataweza kukitegemea kuwafikisha katika kilele cha mafanikio wanachokitaka na kuifungulia milango Zanzibar katika soka la kimataifa.
Alifahamisha kuwa kihistoria alikuwa mchezaji mpira katika ujana wake, na kwamba licha ya sasa kutoweza kucheza, bado ana mapenzi makubwa ya mchezo huo na amekuwa akifuatilia kupitia televisheni na mara kadhaa anapoalikwa viwanjani.
Kutokana na kufuatilia huko, alisema anafarijika kuwaona vijana wa Zanzibar Heroes wakionesha kiwango bora na kupata sifa ya kuwa timu nzuri kuliko nyengine zilizoshiriki michuano ya Chalenji iliyofanyika Dar es Salaam mwanzoni mwa mwaka huu.
Rais Shein aliiambia hadhira iliyohudhuria hafla hiyo kuwa, hakuna sababu Zanzibar ishindwe kurudisha hadhi ya mpira wa miguu kama iliyokuwepo kwenye miaka ya sitini, sabini na mwanzoni mwa miaka themanini, bali akasema kinachohitajika ni ushirikiano na dhamira ya kweli katika kufikia lengo hilo.
"Tukiwa pamoja tunaweza......., pamoja tutafanya mabadiliko, tuunganishe nguvu kwa kushirikiana na wadau waliojitolea kutuunga mkono", alifafanua.
Alizishukuru kampuni na taasisi zilizojitokeza kudhamini hafla hiyo kwa azma ya kuona soka la Zanzibar linapiga hatua, akimtaja Rais wa kituo cha televisheni cha Super Sports cha Afrika Kusini Gary Rathbone, kwamba kuweko kwake kutafungua ukurasa mpya kwa kuwatangaza wanasoka wa Zanzibar.
Mapema, Mwenyekiti wa Future Century Helen Masanja, aliwataka wadau kufikiria ustawi wa mpira wa miguu kuwa unaweza kuwakomboa vijana kiajira na kuwataka waoneshe upendo kwa wanasoka wao hao na kuwachangia kwa kadiri wanayoweza.
Kiasi cha shilingi 58,981,000 zikiwa ahadi ziliweza kupatikana katika hafla hiyo iliyodhaminiwa na Future Century, PBZ, Shirika la Bima Zanzibar, Bandari, ZSSF, Explore Zanzibar, Zan Air, United Petroleum, kampuni ya simu ya Zantel na nyengine kadhaa
No comments:
Post a Comment