Na Mwantanga Ame
MKE wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Seif Iddi, amevitaka vikundi vya SACCOS, Jimbo la Amani, kuacha kuviendesha vikundi vyao kienyeji ili viweze kuimarika na kuacha kuwa na vikundi vingi ambavyo vitakosa kuleta tija.
Hayo aliyasema alipozindua vikundi vitatu vya SACCOSS katika Jimbo la Amani, sherehe ambayo ilifanyika katika ukumbi wa CCM Mkoa Amani wilaya ya Mjini Unguja.
Alisema suala la kuwa pamoja ni moja ya jambo la msingi katika kuendeleza vikundi vya SACCOS, kwani mara nyingi huweza kufikiwa mahitaji na kuweza kutimiza malengo wanayojiwekea.
Alisema wingi wa vikundi katika majimbo ni moja ya sera muhimu ya ya Chama cha Mapinduzi lakini ni lazima waanzilishi wa vikundi hivyo wazingatie kuwa na umoja kwani ndio utaowawezesha kukuza mitaji ya vikundi hivyo.
Alisema kuwepo kwa SACCOS nyingi katika Jimbo moja zinaweza kuwafanya viongozi wa Jimbo ama wafadhili kushindwa kuzihudumia lakini hali hiyo itakuwa nyepesi pale watapoamua kuwa na kikundi kikubwa ambacho kitaweza kuwanufaisha wengi.
Alisema hilo ni moja ya jambo la kuzingatiwa kutokana na mifumo ya kibenki katika utoaji wa mikopo imekuwa ikizingatia wingi wa wanachama katika kikundi kimoja kwani husababisha kuwepo kwa mitaji mikubwa jambo ambalo taasisi hizo huzifukuzia.
“Kule Kitope tuna SACCOS kubwa moja ambayo ndio inayowajumuisha wanawake wote na wanaume katika umoja huo na imeweza kupata mtaji mzuri kutoka CRDB ambapo mwanzo walipewa milioni 50 wakarudisha na sasa wamepewa tena milioni 50 na nyinyi liangalieni hilo ili mpate mtaji mzuri” alisema Mama Asha.
Aliwataka wanachama wa CCM katika Jimbo hilo kuacha kuwaomba sukari, Chai na kanga Wawakilishi na Wabunge wao na badala yake waombe maendeleo ya jumla kwa matatizo yanayowakabili kwenye Jimbo lao.
Alisema tatizo kubwa linalojitokeza katika majimbo mengi hivi sasa kukosa maendeleo ni kutokana na mazoeya ya wapiga kura kushindwa kupeleka shida zinazowakabili katika majimbo yao na badala yake huwasilisha matatizo ya mtu binafsi.
Alisema Jimbo la Amani limepata viongozi wazuri ambao CCM inaamini wanaweza kuwatekelezea maendeleo mengi lakini ni lazima wafikirie kwenda pamoja badala ya mtu mmoja mmoja.
Naye Mwenyekiti wa umoja wa Wanawake Mkoa wa Mjini, Sania Mohammed, akitoa shukrani zake alisema watahakikisha ilani ya CCM katika kuimarisha SACCOS wanaiendeleza kwani ni moja ya ukombozi wa maendeleo ya wanachama wa Chama hicho.
Mapema Katibu wa Umoja wa Wanawake Mkoa, Ghanima Sheha Mbwana, akisoma risala ya SACCOS hizo alisema wameamua kuanzisha vikundi hivyo kwa kuondokana na utegemezi katika kupambana na umasikini ikiwa ni hatua ya kuwaletea heshima wao pamoja na familia zao.
Alisema ingawa vikundi hivyo hivi sasa vimeanza kufanya shughuli mbali mbali za maendeleo lakini vinakabiliwa na changamoto za kuwa na mitaji midogo kunakosababisha mikopo kutoka kwa kusuasua, ukosefu wa vifaa vya kufanyia kazi na kukosa usajili wa kudumu.
Mama Asha katika uzinduzi wa SACCOS hiyo alichangia shilingi 200,000 kwa kila kikundi na shilingi 100,000 kwa vikundi viwili vya Sanaa ambapo SACCOS zilizofaidika na mchango huo ni pamoja na ya Msimamo Imara, Amani Fresh na Tupo Imara.
No comments:
Post a Comment