Habari za Punde

KITUO CHA REDIO KUKUZA MAENDELEO MAKUNDUCHI

Na Ameir Khalid

WANANCHI wa kijiji cha Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja wameelezea kufaidika kwao, kwa kuwepo kwa radio inayotoa huduma za matangazo katika kijiji hicho.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wananchi hao walisema kuwa, ni jambo la kufurahisha kwa kijiji chao kuvumbuliwa kwa radio, ambayo inatoa matangazo na kusikika katika kijiji kizima cha Makunduchi.

Aidha waliongeza kusema kuwa tangu kuanza matangazo ya redio hiyo hivi sasa, wamekuwa wakinufaika zaidi, kwa kupata vipindi mbali mbali ambavyo vimekuwa vikiwaelimisha na kukuza maendeleo ya kijiji hicho.

Mapema Mkuu wa redio hiyo Saumu Ali alisema kuwepo kwa kituo hicho ndani ya kijiji cha Makunduchi, ni fahari kwao na atahakikisha kuwa radio hiyo inaendesha vipindi vilivyo bora kwa manufaa ya wananchi wote.

Alisema kuwa vipindi ambavyo vitakuwa vikiendeshwa hapo vitahakikisha vinaendana na kuzungumzia zaidi matatizo yanayowahusu jamii husika ili wananchi wapate kuelimika zaidi.

Aliongeza kuwa vipindi hivyo ni vile ambavyo vitakuwa vinaigusa jamii katika kuelezea matatizo ya wananchi, ili kuondokana na dhana ya kupeleka kila kitu mjini.

Pia alisema kuwa tayari wameshapata usajili wa muda kutoka tume ya utangazaji zanzibar, jambo ambalo limewapa faraja kubwa kwa kiona kuwa serikali inajali vipaji vya wananchi wake.

Nae mvumbuzi wa radio hiyo ijulikanayo kwa jina Mtegani Fm Radio, inayorusha matangazo yake kupitia masafa ya 107.2 Fm Ramadhani Bilal alisema aliamua kuanzisha radio hiyo baada ya kuwa na hamu ya jambo kwa siku nyingi.

''Wakati nikiwa skuli nilikuwa na hamu kubwa ya kuanzisha masafa ya Radio, na hii ni baada ya kujihisi ya kuwa uwezo wa kufanya hivyo ninao''alisema.

Alifafanua kuwa mara baada ya kufanikiwa kupata masafa ya kurushia matangazo hayo, alianza majarabio yake na hatimae kuanza matangazo rasmi, ambayo hunza kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 7 usiku.

Hata hivyo alisema kuwa kutokana na hali hivi sasa wanalazimika kutumia vifaa duni ambavyo ni vya zamani, hivyo amewaomba wahisani mbali mbali kuisadia vifaa ili iweze kupata vifaa vya kisasa.

Alisema kuwa kifaa kikubwa ambacho kwa sasa kinawasumbua zaidi ni Transmita ya kurushia matangazo, kwani hivi sasa radio hiyo inasikika kijiji cha Makunduchi tu

2 comments:

  1. All da best guy, this is how people drive their life sio kusoma na kutegemea serikali tu, pia thenk kaka othman kwa kweli unanirudisha nyumbani sana yaani lazima ipite siku nipite hpa, may almighty Allah bless u.

    ReplyDelete
  2. Ahsante mdau unakaribishwa si kupitia tu bali hata kuleta habari, picha na matukio huko uliko.

    Thanks

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.