Na Radhia Abdulla, Pemba
MWENYEKITI wa Chama cha AFP, Soud Said Soud, amesema Tume itakayoundwa kukusanya maoni ya utengenezaji wa katiba mpya ya Tanzania lazima iwe na uwiano sawa wa wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Soud alisema Rais Kikwete azingatie uwiano sawa wa wajumbe atakapoteua Tume hiyo kwani ni suala lenye kugusa pande mbili za Muungano.
Mwenyekiti huyo alisema katika katiba hiyo ni vyema suala la kuimarisha kwa jeshi litakalokidhi ulinzi wa nchi, wananchi na mali zao sambamba na kuimarisha ulinzi wa baharini ili kudhibiti vitendo vya kiharamia lielezwe kwa kina katika katiba hiyo.
Akizungumzia suala la elimu mwenyekiti huyo alishauri kuwepo na mwingiliano katika sekta hiyo kwa kutoa fursa sawa kwa wanafunzi wa bara na visiwani katika vyuo mbali mbali vya ndani na nje ya nchi. Alisema katika kuimarisha Muungano, alishauri kuwepo na vitambulisha utaifa na ambavyo vitatumika kama paspoti ya kusafiria jambo ambalo litadumisha utaifa kwa maslahi ya sasa na baadaye.
Kwa upande wa katiba ya Zanzibar, Mwenyekiti huyo alisema katiba hiyo ina mapungufu ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho ili iendane na mfumo wa vyama vingi . Alisema mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa ulipo sasa unapaswa kuendelezwa lakini usiwe ni vyama viwili kwani Zanzibar kuna vyama vingi ambavyo vina wanachama hivyo navyo vinafaa kushirikishwa katika serikali.
Hivyo alitaka katiba ya Zanzibar iandikwe upya na sio kutiwa viraka kwani ndani yake kuna vipengele vingi ambavyo vimetungwa zaidi ya miaka 45 iliyopita na sasa havina manufaa kwa taifa na wananchi wake.
No comments:
Post a Comment