Na Ahmada Ali, MCC
KITIMTIM cha ligi ya a daraja la pili Wilaya ya Mjini, kimeendelea juzi katika viwanja mbalimbali ambapo baadhi ya timu zilikuwa kazini kusaka pointi.
Katika uwanja wa Migombani jeshini, timu ya Muembemakumbi United ikawaadhiri watani wao wa jadi Small Pele kwa ushindi wa magoli 2-1.
Small Pele ndio waliokuwa wa kwanza kuzichana nyavu za wapinzani wao mnamo dakika ya 15 kwa goli lililofungwa na Is-haka Fumu, kabla Juma Hakimu hajaisawazishia Muembemakumbi katika dakika ya 25.
Mabao hayo yalidumu hadi wakati wa mapumziko na timu hizo zilikianza kipindi cha pili kwa kasi na mashambulizi ya kushtukiza.
Lakini walikuwa wapenzi wa Muembemakumbi waliotoka uwanjani na shangwe baada ya mchezaji wake Ahmada Mohammed kuifungia bao la ushindi mnamo dakika ya 70.
Na katika matokeo ya mechi nyengine, Muungano ikatoka kifua mbele dhidi ya FC Roma kwa kuichapa bao 1-0, huku katika uwanja wa KMKM Maisara El Hilal na AFC South zikaumiza nyasi kwa sare isiyokuwa na magoli.
Matokeo kama hayo pia yalijiri katia mechi kati ya Kwaalinato na Langasta, ambapo katika uwanja wa Amani nje, Rangers ikaifyatua Star Kids kwa magoli 2-1.
No comments:
Post a Comment