Habari za Punde

DK SHEIN AENDA UTURUKI

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE Zanzibar 27.4.2011

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuondoka nchini kesho (28.4.2011) kuelekea Jamhuri ya Uturuki kwa ajili ya ziara rasmi kufuatia muwaliko wa Rais wa nchi hiyo Mhe. Abdullah Gul.

Katika ziara yake hiyo, Dk. Shein atafuatana na Mkewe Mama Mwanamwema Shein, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Pandu Ameir Kificho, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Mhe. Omar Yussuf Mzee, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Abdilahi Jihadi Hassan.

Wengine ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Mahadhi Juma Mahadhi, Mkurugenzi Mwendeshaji ZIPA, Salum Khamis Nassor pamoja na Maafisa wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika ziara yake hiyo, Dk. Shein ataweka shada la maua katika kaburi la muasisi wa Jamhuri ya Uturuki marehemu Kemal Ataturk kabla ya mapokezi rasmi katika makaazi ya Rais ambapo pia, atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Mhe. Abdullah Gul na viongozi wengine.

Akiwa nchini Uturuki Dk. Shein atatembelea Chuo cha Utafiti wa Tiba kiliopo Ankara na baadae atazuru Bunge la Uturuki na kukutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Uturuki Mhe. Mehmet Ali Sahin. Baada ya mazungumzo hayo Dk. Shein atakuwa na mahojiano na radio na televisheni ya Taifa ya Uturuki TRT.

Wakati wa usiku Dk. Shein atahudhuria dhifa maalum iliyoandaliwa kwa heshima yake na Rais wa Jamhuri ya Uturuki Mhe. Abdullah Gul.

Aidha, Dk. Shein katika ziara yake hiyo anatarajiwa kutembelea Jimbo la Antalya ambako pamoja na shughuli nyengine atatembelea kituo cha Utafiti wa Kilimo ‘West Mediterranean Agricultural Research Centre’ na kuona maeneo ya asili ambayo ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii nchini Uturuki.

Katika ziara hiyo nae Mama Mwanamwema Shein amepangiwa kutembelea Taasisi za kazi za mikono zilizopo Ankara, Jumba la makumbusho pamoja na kushiriki katika baadhi ya shukughuli

Rais wa Zanzibar anatarajiwa kuondoka nchini Uturuki Jumatatu mchana na kurejea nyumbani baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara na wawekezaji wa Uturuki juu ya fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar.

Rais anatarajiwa kufika nchini siku hiyo ya Jumatatu Mei 2, 2011 jioni

Rajab Mkasaba , Ikulu

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.