Habari za Punde

PAC YABAINI UPOTEVU MAMILIONI YA UMMA

Wawakilishi Wataka Wahusika Wawajibishwe
Na Mwantanga Ame

JINAMIZI la matumizi mabaya na upotevu wa fedha za serikali bado linaendelea kuisakama Zanzibar baada ya kamati ya Mahesabu ya serikali ya Baraza la Wawakilishi (PAC), kubainisha kuwapo upotevu mamilioni ya fedha za umma.

Wakichangia ripoti ya kamati hiyo kabla ya kufungwa kwa kikao cha Baraza, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameilalamikia serikali kufumbia macho upotevu na ufujaji wa fedha za umma.

Lawama za Wajumbe hao zilielekezwa moja kwa moja kwa watendaji na wasimamizi wa majukumu ya umma wakiwemo Makatibu Wakuu na Wakurugenzi katika Wizara mbali mbali kwa kushindwa kuwajibika vyema kuzisimamia fedha za serikali.

Wajumbe hao walisema inashangaza kujirejea kila mwaka mchezo wa upotevu wa fedha za serikali huku zikitolewa sababu hizo kwa hizo zisizofutika kwa miaka yote.

Kwa upande wake, Omar Ali Shehe Mwakilishi wa Chake-Chake, alisema katika ripoti ya mwaka 2006/2007, fedha zilizopotea ni 1,273,364,649 huku fedha za kigeni zikiwa ni dola za kimarekani 72,893 na mwaka 2007/2008 zilizopotea ni shilingi 269,757,772 na fedha za kigeni zikiwa ni dola za kimarekani ni 145,480.

Alisema upotevu zaidi wa mali za serikali umekuwa ukijionesha kwa kutokuwepo kwa vielelezo vya mali za serikali huku kukiwa na baadhi ya watendaji hupandisha gharama wanunuzi wa vifaa vya serikali huku wengine wakitumia mwanya walionao katika kusimamia kazi za ujenzi.

Akitoa mfano Mwakilishi huyo alisema Mkandarasi mmoja wa ujenzi aliiambia kamati hiyo kuwa alipewa kazi na taasisi ya serikali na kutaka alipwe gharama ya shilingi 2,000,000 lakini alipewa vocha iliyokuwa na shilingi 20,000,000 na kugoma kuzipokea lakini baada ya majadiliano alipewa shilingi 500,000 ili akubali kusaini.

Naye Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu alisema suala la hoteli ya Bwawani kuachiliwa zabuni ya kampuni zenye fedha nyingi na kupewa kampuni yenye fedha kidogo linatia wasiwasi na kuitaka serikali kuchukua hatua.

Aidha aliiomba serikali ya Mapinduzi ni ikalidai deni lake katika shirika la Ndege Tanzania (ATC), kwani haiwezekani TANESCO ikawa inadai madeni Zanzibar kwa inadi na vishindo huku SMZ ikawa kimya katika kudai madeni yake.

Nae Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura Hamza Hassan Juma, alisema serikali iliangalie suala la ununuzi wa majenereta mapya ya ZECO baada ya kuwapo kwa taarifa ya majenreta saba tayari yanashindwa kufanya kazi kutokana na kuharibika.

Mwakilishi wa Kitope, Makame Mshimba, akichangia hilo alisema umefikia wakati wa kuona serikali inawafikisha mahakamani wahusika wote waliobainika kupoteza fedha za serikali kwani wana imani kuwa hazipotei bali baadhi ya watu wamekuwa wakinufaika nazo.

Wakijibu hoja za Wajumbe hao Mawaziri wa Serikali akiwemo waziri wa Fedha, Uchumi, Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alisema serikali imeshatowa agizo kwa watendaji wote wa serikali kuorodhesha mali za serikali.

Kwa upande wake waziri wa Nchi Ofisi Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyihaji Makame, aliahidi kudhibiti matatizo ya upotevu wa fedha za serikali hivi sasa tayari serikali inakamilisha mabadiliko ya uundwaji wa serikali za mitaa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheir, alisema serikali itahakikisha ripoti za mdhibiti na mkaguzi wa serikali inazifanyia kazi kwa kuwawajibisha wahusika wote.

Waziri wa Katiba na Sheria Abubakar Khamis Bakary, alisema kuanzia sasa serikali inapaswa kufikiria kuwapandisha Mahakamani wahusika kwani inaonekana vitendo hivyo vikiachwa huenda vikaendelea.

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano alisema ni kweli SMZ inalidai ATC 200 milioni, deni ambalo la mwaka 2008 na hivi sasa tayari wameanza kulishughulikia suala hilo katika vikao vya Muungano na matokeo yake yanaonekana huenda yakawa mazuri.

Nae Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdilah Jihad, alisema kuwa wizara yake itahakikisha inaiangalia upya mikataba yake ikiwa ni hatua itayowezesha kufuata taratibu za kisheria.

Nae Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ali Juma Shamuhuna, alisema hakuna ukweli juu ya taarifa za kuharibika kwa majenereta mapya bali yanashindwa kuwashwa hivi sasa kukabiliana na tatizo la mgao kutokana na hakuna mafuta ya kuendeshea majenereta hayo.

Akifunga mjadala huo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Omar Ali Shehe ameliomba Baraza la Wawakilishi kumuomba Rais wa Zanzibar kutoa neno zito juu ya ripoti ya mkaguzi wa serikali kwa watendaji wa serikali ikiwa hatua ambayo inaweza kusaidia kuondokana na vitendo hivyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.