Habari za Punde

DK MWINYIHAJI AIPONGEZA JKU PEMBA

Na Said Abdul-rahman, Pemba

WAZIRI wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyihaji Makame amelipongeza Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) Kisiwani Pemba kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yao.

Pongezi hizo alizitoa huko Gombani Chake-Chake Pemba wakati alipotembelea jengo la nyumba ya kuishi kamanda wa kikosi hicho Pemba katika moja ya ziara yake ya kutembea Idara zilizo ndani ya wizara hiyo.

Alisema amefurahishwa na uamuzi wa Jeshi hilo kubuni mbinu ya kujenga nyumba ya kuishi kamanda wa JKU Pemba, jambo ambalo limempa faraja na kuongeza mfano huo ni kuigwa na tasisi nyengine.

“Nimefurahishwa sana kuona kuwa mnafikiria mambo muhimu ambayo yatawaletea faida kubwa ndani ya jeshi lenu na pia niwapongeze kwa jitihada zenu kubwa kwa kujenga nyumba hii bila ya kutegemea msaada wowote”, alisema waziri huyo.

Aidha Dk. Mwinyihaji alilitaka jeshi hilo kupanda miti mbali mbali hasa ile ya matunda kama miembe, minazi ambayo itaweza kuwasaidia hapo baadae na pia kufikiria kujenga viwanja vya michezo katika sehemu hiyo ili paweze kuvutia.

Mapema Mwenyekiti wa kamati ya majenzi Luteni Kanali Khamis Dadi Khamis, alimueleza waziri huyo kuwa hadi sasa kiasi cha shilingi milioni 10 zimeshatumika katika jengo hilo ambalo limefikia hatua ya kuezekwa.

Mbali na jengo hilo mwenyekiti huyo alifahamisha kuwa hivi sasa wanampango wa kujenga “Rest House” katika eneo hilo jambo ambalo Waziri Mwinyihaji alisisitiza kuwa hiyo isiwe ya JKU bali iwe ni ya wizara kwa ajili ya kufikia wakuu wake.

Nae Mkuu wa JKU Zanzibar, Kanali Soud Haji Khatib alimueleza Dk. Mwinyihaji kuwa mbali na ujenzi huo pia wamekusudia kujenga nyumba za kuishi askari pamoja na familia zao huko Mfikiwa Pujini Wilaya ya Chake Chake.

Alisema jeshi hilo tayari limeshapata eneo la kutosha sehemu hiyo lakini kubwa linalowabili ni ukosefu wa fedha, hivyo alimuomba waziri huyo kuwatafutia njia mbadala ya kupata fedha ili waweze kuanza ujenzi huo.

Awali waziri huyo alitembelea Ofisi Kuu ya JKU Pemba iliyopo Wawi na eneo la Chuo cha Ufundi huko Chokocho na kujionea mwenyewe maendeleo yanayofanywa na jeshi hilo kisiwani Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.