Habari za Punde

MKANDARASI APIGWA STOP KWA MKATABA TATA

Na Mwantanga Ame

MIKATABA tata katika taasisi za serikali bado linaonekana kuwa tatizo baada ya Kamati ya Mifugo, Utalii Uwezeshaji na Habari ya Baraza la Wawakilishi, kupokea ripoti ya kuwepo kwa mikataba ya aina hiyo katika Chuo cha Utalii Zanzibar.

Hapo awali Kamati hiyo ilipokea taarifa za aina hiyo katika hoteli ya Bwawani na kuuomba uongozi wa Hoteli hiyo kuwasilisha Mikataba iliyofunga na Wawekezaji wa hoteli hiyo.

Aidha, mikataba mingine ambayo serikali imekuwa na wasiwasi nayo imejitokeza katika baraza la Manispaa inayohusu ujenzi wa soko la Saateni ambapo tayari baraza hilo limeunda kamati ya kuchunguza mikataba hiyo.

Kuwepo kwa mikataba tata katika Chuo cha Utalii Zanzibar imebainika jana baada ya kamati hiyo kupokea maelezo kutoka kwa Katibu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Ali Saleh Mwinyikai, aliyewasilisha ripoti ya utekelezaji wa shughuli za Wizara hiyo mbele ya kamati hiyo.

Maelezo ya Katibu katika kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Wawakilishi, alisema Chuo hicho hivi sasa kimefanya ukarabati mkubwa wa jiko pamoja na mkahawa ambapo ukarabati huo umeshakamilika.

Hata hivyo kamati hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wake Asha Bakari Makame ilihoji juu ya ujenzi wa Chuo hicho umefikia katika hatua gani kutokana na kupata tetesi kuwa hivi sasa umesitishwa na mkandarasi amezuiwa kuendelea na kazi hiyo.

Akitoa maelezo juu ya suala hilo, Mwinyikai alisema ni ukweli ujenzi huo umesita kuendelea baada ya mkandarasi huyo kuzuiwa na uongozi wa Wizara baada ya kuonekana mikataba aliyofungishwa ina utata.

Alisema mkandarasi huyo alionekana kushindwa kumalizia kazi aliyopewa kwa muda uliotakiwa huku akiwa tayari amelipwa fedha zaidi ya milioni 24 ikiwa ni sehemu ya shilingi milioni 400 ya mkataba wake hadi atapomaliza kazi.

Alisema kutokana na hali hiyo wizara baada ya kuichunguza walibaini Mkandarasi huyo hakuwa amefungishwa mkataba wa aina yoyote ila kulikuwa na makubaliano tu yaliyofanyika kati ya uongozi wa chuo na mkandarasi huyo.

Kutokana na hali hiyo alisema ndipo wizara ilipoamua kuuangalia upya mkataba wa mkandarasi huyo na kuubaini kuwa umekiuka taratibu za serikali katika utangazaji wa tenda ya ujenzi wa jengo la Chuo hicho.

Alisema taratibu za serikali zilikiukwa kwa asilimia kubwa na ndipo ilipoamua kumtaka Mkandarasi huyo kusitisha kazi hadi pale atapoweza kujitosheleza kufuata taratibu za kisheria ambapo hadi sasa bado hajafikia hatua yoyote.

Nae Mkuu wa Chuo Cha Utalii Zanzibar akizungumzia suala hilo alisema wakati akishika nafasi ya ukuu wa chuo hicho hivi karibuni alikuta baadhi ya vifaa vilivyowekwa na mkandarasi huyo nusu yake vikiwa vimeibiwa ikiwemo mchanga, nondo na kokoto.

Alisema wanachosubiri kuweza kuendeleza ujenzi huo ni baada ya Wizara kukamilisha taratibu zake za kisheria ili kuweza kumalizia Chuo hicho na kukamilika kwa wakati.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, aliuomba uongozi wa wizara hiyo kuiwasilisha mikataba ya Mkandarasi hiyo mbele ya Kamati hiyo ikiwa ni hatua ya kutaka kujiridhisha baada ya mkandarasi aliyepewa kazi hiyo kulalamikia kusitishwa kwa mkataba wake.

Akizungumzia juu ya utekelezaji wa shughuli za Wizara kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Machi, 2011, Katibu Mkuu huyo alisema jumla ya shingi 891,783,302 ikiwa ni sawa na asilimia 24 ya shilingi 3,761,781,212 ya fedha zilizoidhinishwa ajili ya shughuli za taasisi za Wizara hiyo na shilingi na kukusanya shilingi 761,649,705 ikiwa sawa na asilimia 68 ya makadirio ya 1,127,600,000 zilipangwa kukusanywa.

Alisema kwa upande wa miradi jumla ya shilingi 295,000,000 zimeingizwa sawa na asilimia 37 ya shilingi 795,000,000 zilizoidhinishwa kwa ujenzi wa chuo cha Habari, Kuimarisha viwanja vya Michezo, Kamusi ya Kiswahili Fasaha, maendeleo ya chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar na kumbukumbu ya kihistoria na mambo ya Kale.

Aidha, eneo jengine ambalo serikali imelifanyia kazi ikiwa ni kutimiza ahadi za Wizara hiyo mbele ya kamati hiyo ni pamoja na kuanza kwa mchakato wa kuwapatia mikataba ya kudumu ya wafanyakazi wa Hoteli ya Bwawani huku baadhi yao wakiwa masomoni.

Kuhusu Shirika la Utalii, Wizara hiyo ilisema serikali inaendelea kufanya tathmini ya kuangalia uwezo wa Shirika hilo kiutendaji ili liweze kujiendesha kibiashara huku ikiendelea kutafuta mbia wa kulifanyia ukarabati jengo la Living Stone ili kuongeza vivutio vya utalii vya kihistoria na kuchangia pato la taifa.

Katibu huyo alisema katika maeneo ya sekta ya Habari, Wizara hiyo inaendelea kuzitatua changamoto mbali mbali kwa kuzipatia vifaa vya kisasa baadhi ya Idara zake ikiwa pamoja na kuwapa elimu wafanyakazi wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.