Habari za Punde

TUZO ZA MSANII BORA ZENJ NI JUNI 10

Na Mwashungi Tahir, Maelezo

MENEJA Zenj Entertainment, Seif Mohammed Seif, amesema, kazi ya sanaa hivi sasa imekuwa ajira muhimu ikilinganishwa na awali, ambapo ilikuwa ni burdani tu.

Hivyo kuwepo kwa wasanii mahiri ni kuendeleza na kuitukuza fani hiyo katika maendeleo ya muziki hasa kwa upande wa Zanzibar.

Hayo aliyasema jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tuzo za wanamuziki bora wa mwaka2010 na 2011 .

Alisema, lengo la tamasha hilo ni kuchangia na kukuza fani ya sanaa nchini ili izidi kuchangia pato la taifa na kuongeza vivutio vya utalii kwa vile sanaa ni moja ya vivutio vikubwa hasa kwa dunia ya sasa ya utandawazi.

Meneja huyo, alisema, tamasha hilo ni la sita tokea lilipoanzishwa mwaka 2005 na ndio pekee kubwa linaloonyesha taswira halisi ya kazi za wasanii wa Zanzibar ambapo vikundi 18 vinategemea kushiriki katika tamasha hilo,

Miongoni mwa kazi za sanaa zitakazoshindaniwa kwa mwaka huu ni pamoja na msanii bora wa kike na kiume, muziki wa kizazi kipya , mwanamuziki bora wa mwaka , kikundi bora cha mwaka, ngoma asilia , msanii bora wa taarabu asilia.

Meneja huyo, alisema, katika tamasha hilo miongoni wa tuzo zitakazoshindaniwa ni pamoja na ya mwanamuziki bora wa mwaka ambapo aliwataja kuwa ni Cholo Ganun, Juma 20, Sultan King na Rajab Suleiman.

Aidha, alisema, kwamba Vodacom Zanzibar Music Award huwa inawakumbuka na kuwatunuku wasanii mahiri na wakongwe wa Zanzibar walio hai na wale waliotangulia mbele ya haki.

Tamasha la mwaka huu limedhaminiwa na Kampuni Simu ya Vodacom ikishirikiana na Zanzibar Music Award ambapo kilele cha tamasha hilo kitafikia Juni 10, 2011 huko ukumbi wa Salama, Bwawani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.