Habari za Punde

WARATIBU WAANDAE RIPOTI SAHIHI ZINAZOKWENDA NA WAKATI

Yunus Sose, STZ

KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Khalid Mohammed Salum, amewataka waratibu wa wilaya, mikoa na taasisi serikali kubadilika kwa kuandaa ripoti sahihi na zinazokwenda na wakati.

Katibu huyo alieleza hayo jana katika ukumbi wa kituo cha Elimu Mbadala alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili yanayohusiana na uandaaji wa ripoti.

Aliwaeleza waratibu hao kubadilika kiutendaji na kuandaa ripoti sahihi na zinazokwenda na wakati kwani ni muhimu na huisaidia serikali katika mipango yake ya maendeleo.

Alisema lazima ripoti zao zichambue utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwani ndiyo inayotoa miongozo kwa serikali na kufanikiwa kwake kutatokana na kuwepo kwa ripoti sahihi zenye uchambuzi wa
kutosha zitakazotokana na maafisa hao”, alisema.

Alisema serikali ina jukumu kubwa la kusimamia na kutekeleza shughuli za kiserikali katika kuwahudumia wananchi, hivyo waratibu wa serikali wa wilaya na mikoa wanapaswa kuwa makini katika kuandika ripoti sahihi zenye viashiria vya kimaendeleo.

Aliwataka maofisa hao kuwa na mageuzi ya kiutendaji wa kuandaa ripoti zao zitakazokwenda na wakati uliokuwepo kwa kuwasilisha taarifa zao kwa wakati uliopangwa.

Alisisitiza haja ya kuwepo mashirikiano ya kutosha baina sekta moja hadi nyengine suala ambalo litaweza kurahisisha uandaaji wa ripoti zahihi zitakazowasilishwa katika vyombo husika kwa wakati.

Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu katika ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Ahmad Kassim alisema kuwa mafunzo hayo yatakuwa endelevu kwa watendaji wengine ili kuona mpango kazi unaoandaliwa katika uaandaji wa ripoti unakuwa wa kisasa zaidi.

“Mafunzo yetu haya ni mwanzo tu wa safari yetu ya kuwajengea uwezo watendaji wa uratibu katika ngazi mbalimbali na baada ya kipindi kifupi kijacho watendaji hao watafanyakazi kwa ubora na ufanisi zaidi”, alisema Kassim.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.