Habari za Punde

BAJETI YA ZANZIBAR BILIONI 613

Na Mwantanga Ame
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, inakusudia kutumia shilingi bilioni 613 ikiwa ni bajeti yake ya  mwaka ujao wa fedha wa 2011/2012.

Waziri Nchi Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee aliyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.


Akitoa muelekeo wa bajeti hiyo, waziri huyo alisema fedha hizo zitatumika kwa matumizi ya kawaida na matumizi ya shughuli za maendeleo ambapo imeongezeka ikilinganishwa na bajeti inayomalizika ambayo ilitumia shilingi bilioni 444.

Kati ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2011/2012 Waziri Mzee alisema mchango wa washirika wa maendeleo utakuwa ni shilingi bilioni 340.

Kuongezeka kwa bajeti hiyo, Waziri Mzee, alisema kumekuja kutokana na dhamira ya serikali kuipa kipaumbele sekta ya kilimo kwa kuweka mazingira bora yatayoisababishia jamii kuvutika nayo.

Alisema bajeti hiyo inakusudia kuifanya sekta hiyo iwe yenye kuwekeza zaidi badala ya mfumo wa sasa unaoangalia kilimo cha kula zaidi.

Alisema katika bajeti hiyo serikali inachokusudia kukifanya ni pamoja na kununua Matrekta mapya, kuwapatia wakulima mbegu bora, kuzifanyia matengenezo barabara za mashambani ili wakulima waweze kuyafikia masoko kwa urahisi.

Akiendelea alisema kuwa pamoja na hayo pia bajeti hiyo inakusudia kuongeza idadi ya mabwana shamba, kununua majembe madogo madogo na kutekeleza mpango wa kuwaonesha masoko wakulima.

Eneo jengine ambalo serikali italizingatia ni upandishaji wa mishahara ya Wafanyakazi wa Utumishi wa Umma, ambapo wataweza kuongezewa viwango vyao kwa kulingana na jasho wanalolitoa.

Akitoa mfano alisema Daktari bajeti ijayo imemuangalia kulingana na kazi zake, Mwalimu nae ataangaliwa hivyo hivyo na mwanasiasa ataangaliwa kulingana na jasho lake.

Jengine ambalo serikali italizingatia katika sekta ya Utumishi alisema ni namna ya kuwaweka wataalamu ikiwa ni hatua itayosaidia kupungua tatizo la kukimbia.

Alisema hilo wamelizingatia kutokana na hivi sasa Zanzibar tayari imekimbiwa na wataalamu wengi kulikosababishwa na maslahi duni ya utumishi wa umma ambapo bajeti ijayo itawawezesha kubakia nchini na kuitumikia nchi yao.

Alisema jambo la msingi ambalo serikali imeamua kuchukua hatua hiyo kwa lengo la kuwafanya watumishi wa umma kuona wanawajibika zaidi na waache tabia ya kulalamika.

Kuhusu suala la bajeti ijayo ina uwezekano wa kuongeza kodi ama kuwepo kwa misamaha ya kodi Waziri Mzee alisema hilo halipo kwani hakutakuwa na ongezeko la kodi hasa za ndani.

Alisema bajeti hiyo imezingatia kutokuwepo kwa mpango huo kutokana na viwango vya kodi vya Zanzibar vinatofautiana na Tanzania Bara kwa vile bara zipo nyingi zikiwemo katika sekta ya nishati ya mafuta.

Bajeti hiyo alisema pia inakusudia kuanzisha majengo mapya ya taasisi za serikali kwa baadhi ya Wizara pamoja na kujenga barabara zote za Mjini chini ya mpango wa Benki ya Dunia.

Aidha alisema pia serikali kwa vile serikali iliyopo hivi sasa imo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa katika bajeti ijayo inakusudia kujenga majengo ya makaazi kwa viongozi walioteuliwa kushika nafasi hizo kwa upande wa Kisiwani Pemba kutokana na hivi sasa kukosekana nyumba za viongozi hao.

Waziri huyo pia alisema sehemu kubwa ya bajeti hiyo itazingatia kufuata mpango wa taifa wa kukuza uchumi (MKUZA) namba mbili na kufuata dira ya maendeleo ya 2020 kutokana na hivi sasa tayari SMZ imeweza kufikisha miaka 10 ya mpango huo.

Kuhusu kama serikali ina mpango wa kufuta ziara za viongozi na safari za nje alisema hilo serikali italiangalia kwa kuweka utaratibu maalum ambao utawataka watendaji kufuata mwongozo wa serikali wa kupata vibali katika ngazi za juu.

Hata hivyo alisema tayari hivi sasa serikali imeanza kutekeleza hilo kwa kuona wanaokwenda nje wawe wahusika halisi na kupunguza siku za kuondoka kwa kuruhusu kuondoka siku ambazo mikutano hufanyika badala ya utaratibu wa zamani wa kufika kabla ya siku za mikutano.

Alisema wanalazimika kuweka utaratibu huo kutokana na uwepo wa ulazima wa kushiriki mikutano ya kimataifa kwa vile bila ya kufanya hivyo Zanzibar inaweza ikakosa msemaji wake hasa katika vikao vya nchi wanachama vikiwemo vya SADC, WTO, Benki ya Dunia na Umoja wa Mataifa.

Bajeti ya Zanzibar inatarajiwa kusomwa rasmi kuanzia kesho ambapo tayari Katibu wa Baraza la Wawakilishi Ibrahim Mzee, ametangaza kuanza kwa kikao hicho ambacho kinatarajiwa kuchukua zaidi ya mwezi mmoja kwa kujadili bajeti za Mawizara 16 ya serikali ya Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.