Na Rajab Mkasaba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein ameagana na Madaktari kutoka China wanaomaliza muda wao wa kazi hapa Zanzibar na kuwaeleza kuwa huduma zao walizozitoa zimeweza kuchangia juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar za kuimarisha sekta ya afya Unguja na Pemba.
.
Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar alipokuwa na mazungumzo na jopo la Madaktari kutoka China ambao wamemaliza muda wao wa kazi hapa Zanzibar na wanatarajia kurejea nyumbani mnamo tarehe 18 mwezi huu. Madaktari hao walifuata na Balozi mdogo wa China hapa Zanzibar Bi Chen Qiman.
Katika maelezo yake Dk. Shein aliwaeleza madaktari hao kuwa wananchi wa Zanzibar pamoja na serikali kwa jumla wamefarajika kwa kiasi kikubwa kwa kuwepo kwa madaktari hao kwa kipindi chote cha miaka miwili hapa nchini ambacho wameweza kutoa huduma kikamilifu.
Alieleza kuwa hatua hiyo imeweza kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar za kuimarisha sekta ya Afya Unguja na Pemba ambapo tayari hatua kubwa ya mafanikio imefikiwa katika sekta hiyo.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendeleza ushirikiano na uhusiano na China na kutoa pongezi kwa wananchi wa China pamoja na viongozi wao wakuu kwa kuendeleza ushirikiano na Zanzibar.
Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar inathamini sana ushirikiano na misaada mbali mbali inayotolewa na China katika sekta maendeleo ikiwemo sekta ya afya ambapo China ina miaka 47 tokea ianze kuleta madaktari wake hapa Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk. Shein alitoa pongezi kwa Madaktari hao wanaomaliza muda wao na kuwaeleza kuwa licha ya changamoto mbali mbali lakini wameweza kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa na kuweza kuwahudumia wananchi wa Zanzibar ambao nao wanakiri ubora wa huduma wanazozitoa madaktari hao.
Dk. Sheina alisema kuwa wananachi wa Zanzibar ni wakarimu sana hatua ambayo imeweza kusaidia kuishi vizuri na madaktari hao katika kipindi chote walichofanya kazi nchini.
Aidha, Dk. Shein aliwaeleza Madaktari hao kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar awamu ya saba imeamua kutekeleza kwa vitendo sera za afya kwa kuwashirikisha wananchi katika utekelezaji huo.
Alisema kuwa miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuiimarisha hospitali ya MnaziMmoja kwa kuipatia vifaa vya kisasa na wataalamu ili ifikie hadhi na kiwango cha hospitali ya rufaa.
Alisema kuwa huduma za afya zitaimarishwa ambapo tayari serikali anayoiongoza ina lengo la kuanzisha kitengo cha kushughulikia maradhi yanayotokana na matatizo ya figo, maradhi ya moyo, maradhi ya saratani na huduma nyengine.
Pia, Dk. Shein alieleza kuwa serikali imo katika mikakati madhubuti ya kuziimarisha hospitali ya Abdulla Mzee pamoja na kuifanyia ukarabati mkubwa hospitali ya Wete ili ziweze kufikia lengo lililokusudiwa la kufikia hadhi ya kiwango cha hospitali za Mkoa.
Nao Madaktari hao kutoka China wanaomaliza muda wao wa kazi hapa Zanzibar walitoa shukurani kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wananchi wa Zanzibar kwa kuweza kupata mashirikiano mazuri katika kipindi chao chote walichofanya kazi hapa Zanzibar.
Kiongozi wa kundi hilo la Madaktari Dr.Zhu Xiangju alimueleza Dk. Shein kuwa katika muda wao waliofanya kazi hapa Zanzibar wameweza kutoa huduma mbali mbali kwa wananchi zikiwemo zile zilizohitajia umakini na kuhitaji uharaka wa kupatiwa tiba.
Dk. Xiangju alisema kuwa mashirikiano makubwa wameyapata kutoka kwa Madaktari wazalendo pamoja na uongozi mzima wa Wizara ya Afya wakati wote walipokuwepo nchini na kukiri kuwa huduma za afya hapa Zanzibar zimeimarika kwa kiasi kikubwa.
Alieleza kuwa ni imani yake kubwa kuwa Zanzibar itaendelea kupata mafanikio zaidi katika sekta ya afya kutokana na kushuhudia juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kueleza kuwa timu nyengine ya madaktari kutokana nchini mwao iko njiani kuwasili hapa Zanzibar.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Mohamed Saleh Jidawi, alimueleza Dk. Shein kuwa Madaktari hao 21 wanaomaliza muda wao ni kundi la 23 tokea China ilete Madaktari wake hapa Zanzibar na kundi la 24 linatarajiwa kuwasili nchi tarehe 12 mwezi huu na kusifu huduma pamoja na mashirikiano wanayotoa madaktari kutoka China.
No comments:
Post a Comment