Na Salum Vuai, Maelezo
KUFUATIA matokeo ya pambano la ligi daraja la kwanza taifa kati ya Mlandege na Ngome, timu ya Polisi Bridge imeamua kupanda ngazi za Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kutaka ibatilishe ushindi wa Ngome.
Katika mchezo huo, Ngome ambayo awali ilihitaji ushindi wa magoli 7-0 ili isiteremke daraja, iliweza kushinda kwa magoli 9-2, matokeo ambayo yameifanya Polisi Bridge kushuka daraja.
Katika barua yake iliyoiandikia ZFA Taifa, Bridge imezilalamikia Mlandege na Ngome kuwa zilipanga matokeo ili kuinufaisha Ngome na kuikomoa timu ya maafande hao.
Bridge imeeleza kuwa, ni wazi Mlandege ambayo ilikwishashuka daraja na haikuwa na chochote cha kupoteza katika mchezo huo, ilijifungisha magoli tisa makusudi kitendo ambacho hakijawahi kutokea katika ligi msimu huo uliomalizika hivi karibuni.
"Kwa vile Mlandege ilikwishashuka, ilitumia mwanya huo kulazimmisha kupanga matokeo ili kuinusuru Ngome, kila aliyeshuhudia pambano hilo aliona hali ya ufungaji magoli, kwamba ilikuwa dhahiri imepangwa", ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu wa Bridge Suleiman Yussuf Said.
Aidha barua hiyo yenye kumbukumbu namba RPHQ/KUS/U/01/01 ya tarehe 16 Juni, 2011, imefahamisha kuwa, kitendo kilichofanywa na timu hizo, ni kwenda kinyume na kanuni za mpira wa miguu Zanzibar kifungu cha 18, hivyo imeiomba ZFA kuyafuta matokeo ya mchezo huo pamoja na kutoa adhabu nyengine zilizoelezwa ndani ya kanuni vifungu 18 (ii) na (iii).
Uongozi huo wa Polisi Bridge ulikumbushia kuwa, ZFA iliamua kupanga michezo yote sita kuchezwa kwa siku na wakati sawa, ili kuondosha dhana ya kupangwa matokeo, na kwamba kitendo cha timu hizo kimeonesha dharau kubwa kwa ZFA hivyo ni wajibu wa chama hicho kuchukua hatua ili kukomesha vitendo kama hivyo.
Ikihitimisha barua yake, Polisi Bridge imesisitiza kuwa ili Zanzibar iweze kupata maendeleo ya kweli katika soka, ni wajibu wa ZFA kuhakikisha kuwa inasimamia kikamilifu kanuni za uendeshaji mashindano na kutoa adhabu kwa kuzifuata bila ya upendeleo.
No comments:
Post a Comment