Habari za Punde

POLISI YABAMBA MAGUNIA YA BANGI

Na Ramadhan Himid, POLISI

KITENGO cha kupambana na dawa ya kulevya kilicho chini ya Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, kimefanikiwa kuwakamata watu wawili wakiwa na viwango tofauti vya majani makavu yanayodhaniwa kuwa ni bangi.


Akithibitisha kukamatwa kwa watu hao Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar, Kamishna Msaidizi wa Polisi Muhudi Juma Mshihiri, alisema watuhumiwa hao wamekamatwa kutokana na ushirikiano wa wananchi kufuatia operesheni mbali mbali zinazoendeshwa na Jeshi hilo ili kukomesha biashara ya  bangi pamoja na dawa kulevya nchini.

Aliwataja watu hao kuwa ni Othman Issa Mdabe (22) wa Kilindoni Mafia aliyekamatwa na mafurushi 277 ya bhangi akitokea Tanzania Bara ambapo mafurushi hayo aliyahifadhi ndani ya mito ya sponji 11, mtuhumiwa huyo alikamatwa kutokana na ushirikiano wa wafanyakazi wa Bandarini kutoa taarifa za kumtilia shaka kijana huyo.

Mwengine ni Shaaban Salum Othman (40) wa Miembeni aliyekamatwa na mifuko 10 ya plastiki ikiwa na majani ya bhangi huko Miembeni Mjini Unguja.

 Wakati huo huo Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi imefanikiwa kuwakamata watu watatu wakiwa na bhangi, akithibitisha kukamatwa kwa watu hao Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Azizi Juma Mohammed amewataja watu hao kuwa ni Nyange Makame Ali (61) wa Shauri Moyo aliyekamatwa na robo kipolo cha bhangi huko Shauri Moyo Mjini Unguja.

 Kamanda Azizi pia aliwataja Hamad Said Omar (38)  wa Kilwa na Izshaka Yumbeshi (30) wa Saateni Unguja ambao wote walikamatwa na nusu kipolo kikiwa na bhangi, mkoba wa rasketi na nyongo 38 za bhangi.

Kamanda Azizi amewataka wananchi kuyendelea kutoa taarifa mbali mbali za wahalifu ili kukomesha utumiaji wa bangi pamoja na madawa ya kulevya.

 Watuhumiwa wote hao watafikishwa Mahakamani mara upelelezi utakapokamilika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.