Na Abdi Shamnah
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema ni jukumu la serikali kuhakikisha kila mkoa hapa nchini unakuwa na walimu wa kutosha na wenye sifa ili kuimarisha kiwango cha elimu.
Maalim Seif alisema hayo jana ofisini kwake Migombani mjini hapa alipokuwa akizungumza na ujumbe ya Chama cha Walimu Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine ulizungumzia changamoto mbali mbali zinazoikabili kada ya ualimu na sekta ya elimu kwa jumla.
Kauli hiyo Maalim Seif inafuatia malalamiko yaliotolewa na viongozi wa Chama hicho ya walimu wa kike walioko Pemba, kutengwa na familia zao (waume) zilioko Unguja, hata baada ya kuomba uhamisho kwa muda mrefu.
Alisema suala la walimu wa kike kisiwani humo kuishi mbali na familia zao linatokana na tabia iliojengeka miongoni mwa wafanyakazi kutopenda kufanyakazi kazi kisiwani humo.
Alisema imekuwa ni jambo la kawaida kwa wasichana kuomba ajira ya kufanyakazi kisiwani huko, lakini baada ya kuajiriwa hutumia ujanja wa kudai uhamisho kwa kile wanachodai ‘kwenda Unguja kuishi na waumezao’.
“Ni kweli kuwa kuishi mbali na familia ni tatizo, serikali haitaki watu watengane, lakini tukianza kukaribisha jambo hili kila mtu aje Unguja, Pemba itabaki bila ya walimu”, alisema.
Alisema kuna umuhimu wa kuliangalia suala hilo katika upande wa pili wa shilingi, kuzingatia ulazima wa walimu kubaki huko na kuondokana na tatizo la upungufu wa walimu maskulini.
Aliuhakikishia ujumbe huo kuwa serikali inalenga kuboresha maslahi ya wafanyakazi wakiwemo walimu, ambapo mishahara itategemea sifa na muda wa utumishi kwa mfanyakazi, kutoa nyongeza za mishahara kila mwaka, kulipa malimbikizo ya posho mbali mbali, ikiwemo za likizo pamoja na
kuwepo uwiano wamaposho kwa wizara zote ili kuondoa manung’uniko.
kuwepo uwiano wamaposho kwa wizara zote ili kuondoa manung’uniko.
Alieleza kuwa tatizo la kuchelewa mishahara kwa walimu kisiwani Pemba, kutokulipwa ‘area’ pamoja na kukosekana kwa fedha za likizo nayo ni miongoni mwa masuala yatakayopatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Alifafanua kuwa mazingira mabaya yaliokuwepo hapo nyuma ndiyo yanayopelekea vijana wengi kuikimbia nchi baada ya kusomeshwa na serikali, hivyo aliwahakikishia wajumbe hao kuwa serikali itafanya kila iwezalo kuona wataalamu wake wanabaki nchini.
Akizungumzia hoja ya Wizara ya Elimu kuwachangisha walimu na wafunzi, Maalim Seif alisema kuna ulazima wa kuwepo utaratibu ulio wazi na utakaofahamika na walimu, jinsi ya fedha hizo zinavyotunzwa na zinavyotumika.
Akigusia juu ya tatizo la fedha zilizotengwa katika Bajeti na kuidhinishwa na Baraza la Wawakilishi lakini hatimae kutotolewa zote, alisema ni tatizo la Wizara zote ambapo kiini chake ni uchache wa
fedha zilizopo hizo na kutokidhi mahitaji yaliolengwa, huku miradi ya maendeleo akisema ndiyo inayoathirika zaidi.
fedha zilizopo hizo na kutokidhi mahitaji yaliolengwa, huku miradi ya maendeleo akisema ndiyo inayoathirika zaidi.
Alisema fedha zinazopatikana hulengwa kutumika katika miradi iliopewa kipaumbele, na kutoa indhari katika matumizi ya fedha kwa ajili ya safari (kama kipaumbele), akisema sio kila safari yafaa kupewa kipaumbele.
Maalim Seif alitumia fursa hiyo kuwataka walimu nchini kote kuelewa jukumu lao kubwa kwa taifa la kuwapatia elimu yenye kiwango vijana, na kuainisha kuwa hakuna ‘haki bila ya wajibu’.
Mapema Katibu mkuu wa Chama hicho Mussa Omar Tafurwa alimweleza Makamu wa Kwanza wa Rais, changamoto mbali mbali zinazowakabili walimu, ikiwemo michango kadhaa kutoka mishahara yao inayokatwa na serikali kwa ajili ya masuala mbali mbali.
Michango hiyo ni pamoja na ule wa Tamasha la Elimu bila malipo, Juma la Elimu ya watu wazima, Siku ya Walimu Duniani na ule wa kuendeleza TC.
Mbali na kusema michango hiyo haiwanuafaishi walimu hao zaidi ya ule wa kuendeleza TC, viongozi hao walionyesha mashaka makubwa juu ya udhibiti wa fedha hizo na matumizi yake, sambamba na michango ya kila mwaka inayotolewa an wanafunzi.
No comments:
Post a Comment