Habari za Punde

WAZIRI JIHAD TAKA KUENDELEZWA USHIRIKIANO NA IRAN

Na Ali Amour, WHUUM

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdillah Jihad Hassan amesema mashirikiano baina ya Zanzibar na Iran katika nyanja ya Utalii na mawasiliano itazidisha udugu wa kihistoria uliopo baina ya wananchi wa hizo.


Waziri Jihad alieleza hayo alipokutana na kufanyamazungumzo na Naibu waziri wa Filamu na Televisheni wa Iran Javad Shamaqdari huko Mnazi Mmoja mjini hapa.

Alisema kwa kiasi kikubwa Zanzibar imekuwa ikitegemea sekta ya utalii katika uchumi wake hivyo Iran ina nafasi kubwa ya kushirikiana na Zanzibar katika kuhakikisha sekta hiyo inaleta manufaa zaidi.

Waziri huyo alisema Zanzibar inafanya juhudi mbalimbali kujikita katika masoko ya kitalii kwa mataifa mbalimbali ikiwemo Iran, Turkey na nchi za Asia ambako soko hilo linaoyesha kukua kwa kasi.

Alisema mbali utalii lakini pia nchi hizo zinaweza kushirikiana katika sekta ya mawasiliano ambayo imekuwa na mchanho mkubwa katika maendeleo pamoja na utamaduni. 

Waziri Jihad aliiomba serikali ya Iran kutumia uzoefu na utaalamu iliyonao o kwa kuwapatia wanahabari wa Zanzibar elimu nchini Iran pamoja na kubadilishana uzoefu katika taaluma hiyo.

Waziri Jihad alisema Zanzibar na Iran zina utamaduni unaolingana unaowafanya raia wa nchi hizo kuwa kitu kimoja, na kueleza furaha yake kutokana na ujio wa Naibu waziri huyo akisema ziara hiyo itakuza jitihada zinazochukuliwa katika kuziendeleza hususan katika nyanja za utamaduni na mawasiliano ya habari.

Nae Naibu waziri wa Filamu na Televisheni wa nchi hiyo alisema mikakati ya nchi yake katika kukuza uhusiano na Zanzibar katika nyanja za utamaduni na mawasiliano kuwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kushirikiana na Zanzibar katika kukuza utamaduni kwa kuwa na makumbusho yanayo elezea asili ya Shirazi na washirazi.

Alisema mwaka huu atahudhuria katika tamasha la kimataifa la filamu la Zanzibar (ZIFF), ambayo itakuwa mara ya kwanza kushiriki katika maonyesho hayo yanayoandaliwa Afrika.

Shamaqdari alimuomba Waziri Jihad kuandaa taarifa za kihistoria za Shirazi na kitamaduni ili ziwe ni sehemu ya makumbusho yaliyoko nchini Iran ikiwa ni njia moja wapo ya kuutangaza utamaduni wa Zanzibar kimataifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.