Habari za Punde

MAALIM SEIF AKUTANA NA JOPO LA MADAKTARI WA KUJITOLEA KUTOKA UTURUKI

Na Abdi Shamnah
MAKAMU  wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema Serikali inalenga kupanua wigo wa ushirikiano kati yake na Serikali ya Uturuki, ili nchi hiyo iweze kuongeza nafasi za masomo katika sekta ya Afya, kwa vijana wa Zanzibar.

Amesema hayo leo Ofisini kwake Migombani wakati alipokutana na jopo la Madaktari 18  wa kujitolea, (wakiwemo madaktari bingwa) kutoka Uturuki waliokuja nchini kwa ajili ya kutoa huduma mbali mbali za tiba katika hospitali kuu ya Mnazimoja.
Madaktari hao katika nyanja mbali mbali, walikuwa nchini kwa kipindi cha wiki mbili na kusaidia utoaji wa huduma mbali mbali za tiba na uchunguzi kwa wagonjwa wa moyo,mifupa na maradhi ya wanawake sambamba na kuendesha mafunzo ya utoaji huduma katika mazingira ya dharura kwa wafanyakazi wa Hospitali hiyo.
Mbali na shughuli hizo pia madaktari hiyo walifika kisiwani Pemba ambako walitoa msaada wa vyandarua.
Maalim Seif amesema kwa kipindi kirefu sasa, Serikali ya Uturuki imekuwa ikiisaidia Zanzibar katika sekta ya Afya kwa kutoa nafasi za masomo pamoja na madaktari kusaidia huduma za afya nchini.
Alisema ili kupanua wigo wa ushirikiano, Serikali ya Zanzibar inakusudia tafanya mazungumzo na nchi hiyo ili itowe fursa zaidi za mafunzo na hatimae Zanzibar iweze kuwa na madaktari wa kujitosheleza.
Alisema Serikali ya Zanzibar pia itaiomba Uturuki kuwa na utaratibu utakaowezesha madaktari wake kuja Zanzibar kila mwaka, kwa ajili ya kutoa huduma za tiba na kuendesha mafunzo kwa madaktari wazalendo, kama zilivyo nchi za China na Cuba, ambazo zimekuwa na utaratibu wa aina hiyo.
Aidha alisema hatua inayoendelea hivi sasa,kwa madaktari kutoka nchi hiyo kuja nchini na kutoa huduma kupitia NGO, kufuatia ushawishi uliofanywa na Jumuiya ya Wazanzibar waliosoma  katika vyuo vikuu vya nchi hiyo, haina budi kupata msukumo kutoka Serikali kuu, kusimamia jambo hilo.
Alisema ujio wa madaktari hao umeiwezesha Serikali kuokoa fedha nyingi za kigeni ambazo zingepasa kutumika kusafirisha wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu, lakini pia mafunzo yaliyotolewa yamewajengea uwezo  na kuwapa mbinu mpya madaktari wazalendo.
Aliwapongeza madaktari hao kwa kujitolea na kutumia muda wao wa likizo pamoja na kutoa fedha mifukoni mwao kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zao, hatua aliyosema inadhihirisha uhusiano mwema uliopo kati ya watu wa nchi mbili hizo.
Alisema watu wa nchi mbili hizi wanakabiliwa na tatizo kubwa la mawasiliano ya lugha na kutoa rai kwa raia wa Zanzibar kujifunza Kituruki sambamba na  Waturuki nao kujifunza Kiswahili,akiainisha wepesi uliopo katika kujifunza lugha hiyo (Kiswahili).     
Mapema akitotoa ufafanuzi juu ya shughuli zilizoendeshwa na Madaktari hao, Kiongozi wa Jumuiya ya Wazanzibari waliosoma vyuo vikuu nchini Uturfuki Dr. Abdurahman alisema moja ya jambo kubwa lililofanywa an madaktari hao walipokuwa nchini ni kuendesha operesheni mbili za mifupa ambazo kama zingelifanyika nje ya nchi zingeiharimu zaidi ya shilingi Milioni tano kila moja.
Lakini pia kikundi hicho cha madaktari kinalenga kuendesha matibabu nchini Uturuki kwa wagonjwa wanne wa maradhi ya moyo, ambapo Serikali ya Zanzibar italazimika kugharamia nauli ya kwenda na kurudi kwa wagonjwa hao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.