Hayo yameelezwa na Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad , kwa nyakati tofauti alipozungumza na wananchi wa Majimbo ya Chonga na Chakechake kisiwani Pemba,ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kukutana na Viongozi wa majimbo ya Chama cha CUF, sambamba na kuzungumza na wananchi.
Amesema ili kuondokana na tatizo la usafiri lililoshamiri hivi sasa kati ya visiwa vya Unguja na Pemba , Serikali imeigiza Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano kufanya juhudi kupata meli kubwa ya kisasa itakayoweza kukidhi haja ya usafiri iliopo.
Alisema hali ya usafiri kati ya visiwa hivyo hivi sasa ni mbaya, ambapo meli zinazotoa huduma ya kusafirisha abiria ni chakavu mno na zisizo na uhakika wa safari, kiasi ambacho haziwahakikishia abiria usalama wao.
Alisema kumekuwepo na matukio mbali mbali ya kufadhaisha miongoni mwa meli zinazofanya safari kati ya Unguja na Pemba , hali inayowafanya wananchi wengine kuakhirisha safari zao kutokana na hofu ya kupatwa na majanga.
Alieleza kuwa meli itakayonunuliwa ina lengo la kuwaondolea kero ya usafiri wananchi wa visiwa hivyo, huku Serikali ikijizatiti kutoza nauli ndogo ili wananchi waweze kuitumia bila manung’uniko.
Aidha alisema, uamuzi wa kununua meli hiyo una lengo la kuepuka matumizi ya boti ziendazo kasi (Speed Boat) ili kuwaweza wananchi, wakiwemo wafanyabiashara kusafirisha mizigo yao bila ya usumbuufu.
Akigusia usafiri wa barabara, Maalim Seif aliipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Mstaafu Amaani Abeid Karume kwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kujenga barabara za lami Unguja na Pemba .
Alisema ni kazi ya Serikali ya awamu ya saba ilio chini ya mfumo wa Umoja wa Kitaifa, kukamilisha ujenzi wa barabara zilizosalia, hususan zile za vijijini.
Akizungumza na wananachi wa kijiji cha Kuungeni Tundaua, Jimbo la Chonga, Maalim Seif aliwahakikishia wananchi hao kuwa barabara yao ni miongoni mwa zile zilizopewa kipaumbele na zinatarajiwa kukamilika katika kipindi kifupi kijacho.
Alisema usafiri wa anga nao unaimarishwa kwa kuviimarisha viwanja vya ndege vya Unguja na Pemba , ili viweze kutumika na mashirika mbali mbali ya ndege ya Kimataifa.
Alisema baada ya upanuzi wa njia ya kurukia katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Karume, kazi inayoendelea ni ujenzi wa jengo la kisasa la kufikia abiria, ili kuondosha usumbufu kwa abiria na kuupa hadhi uwanja huo kuonekana kama kweli wa Kimataifa.
Alisema uwanja wa Ndege ulioko Pemba nao unatarajiwa kujengwa jengo la kisasa la kufikia abiria ili wananchi na wawekezaji waweze kukitumia kikamilifu kisiwa cha Pemba na kuwekeza miradi yao .
Katika hatua nyingine, Maalim Seif aliwahakikishia wananchi wa Majimbo hayo kuwa maendeleo yalioanza kujitokeza nchini, yanatokana na mshikamano mkubwa wa viongozi pamoja na kuwepo na kushamiri kwa hali ya amani, chini ya uongozi wa Serikali ya Umoja wa kitaifa.
No comments:
Post a Comment