Na Salum Vuai, Maelezo
NAIBU Waziri wa Urithi na Utamaduni wa Oman, Hamed Bin Hilal El Maamary, ameishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuiandikia barua rasmi Serikali ya nchi yake iweze kulifanyia kazi ombi la kuanzisha kitivo cha lugha ya Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Ushauri huo aliutoa jana kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdilahi Jihad Hassan, alipomtembelea na ujumbe wake, Waziri huyo kumsalimia na kuishukuru Serikali kwa mapokezi mazuri pamoja na kufanikisha tamasha la utamaduni la nchi yake.
Naibu Waziri huyo aliongoza tamasha hilo lililozinduliwa juzi huko Beit El Ajaib, alisema fikra ya kuitaka Oman ifungue kitivo hicho ni njema na inastahili kufanyiwa kazi haraka kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar na Oman.
Kutokana na umuhimu huo, alisisitiza haja ya kuwasilisha ombi rasmi na kuwahakikishia Serikali yake italipa uzito mkubwa kwa lengo la kukuza na kuendeleza uhusiano na mawasiliano kati ya wananchi wa nchi mbili hizo.
“Nimefurahishwa na fikra ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi wakati akizindua tamasha letu, kuitaka nchi yangu ianzishe kitivo cha lugha ya Kiarabu (SUZA), hili linawezekana, naahidi kulifanyia kazi baada ya kupokea barua rasmi kutoka kwenu”, alifafanua.
Aidha, aliwasilisha salamu za Waziri wa Urithi na Utamaduni wa Oman, Haitham Bin Tariq Al Said kwa Waziri huyo na Serikali ya Zanzibar na wananchi wake na kusema kufanyika kwa tamasha la utamaduni la nchi yake hapa ni ishara njema na muhimu katika kuimarisha udugu wa damu wa wananchi wa nchi zao.
Akimkariri Waziri wake kupitia salamu hizo, El Maamary alisema tamasha hilo ni sehemu ya utekelezaji makubaliano yaliyofikiwa na nchi hizo katika mkataba uliotiwa saini baina yao Agosti 17, mwaka jana na kusisitiza haja ya kutanua wigo wa ushirikiano utakaoleta manufaa kwa wananchi wao.
Kwa upande wake, Waziri Jihad alisema ni matumaini yake kuwa wananchi wa Zanzibar watajifunza mengi kutokana na maonesho ya utamaduni yanayoendelea, na kwamba mavazi yanayooneshwa ambayo ni ya staha sawa na yanayovaliwa hapa, yatawapa changamoto ya ubunifu wa mitindo mipya.
Aidha, alisema mbali na uhusiano wa kiutamaduni, ziara ya ujumbe wa Oman itafungua milango ya kuimaraisha sekta ya utalii, kwani ujio wao unaitangaza nchi yao sambamba na wao kuinadi zaidi Zanzibar wakiwa nchini kwao na kwengineko wanakoendesha matamasha kama hayo.
Jihad aliuhakikishia ujumbe huo kulifanyia kazi pendekezo la Makamu wa Pili, na kwamba Wizara yake haitachelewa kuandika ombi rasmi la kuanzishwa kitivo cha lugha ya Kiarabu katika chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Alisema anaamini kuwa Wazanzibari wataweza kujifunza lugha hiyo kwa wepesi kutokana na lugha yao ya kiswahili kujengeka mno kwa misamiati ya kiarabu, pamoja na dini ya Kiislamu ambayo inasimama kwa msingi wa lugha hiyo.
Jihad alitumia fursa hiyo kuwakaribisha katika ufunguzi wa tamasha la utamaduni wa Mzanzibari lililopangwa kufanyika Julai 18, mwaka huu huko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alimshukuru Naibu Waziri huyo, ujumbe aliokuja nao, na Serikali ya Oman kwa kuendeleza udugu wao na Zanzibar, na kuwatakia ziara ya furaha na marejeo mema watakaporudi kwao.
El Maamary pia alimzawadia Jihad zawadi ya kazi ya mkono iliyosanifiwa katika sahani ya fedha, inayoonesha ngome zinazotumiwa na Waomani katika mambo mbalimbali, pamoja na kumpa mualiko wa kufanya ziara Oman ili kuangalia maeneo na namna ya kufanya tamasha la utamaduni wa Zanzibar nchini humo.
Katika mazungumzo hayo, alikuwepo pia Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Majid Abdallah Al Abadi, watendaji wengine wa ofisi yake, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Dk. Ali Mwinyikai, na maofisa wa ngazi za juu wa wizara hiyo.
No comments:
Post a Comment