Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akipata maelezo ya bei ya Tungule kutoka kwa mfanyabaishara Alawi Hamad wa soko la Mwanakwerekewe, wakati alipolitembelea soko hilo jana.Picha na OMKR
Awataka kuachana na tamaa na utajirishoNa Abdi Shamnah
MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar , Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wafanyabiashara nchini, kuuza bidhaa zao kwa kuangalia uwezo wa wananchi, badala ya kuelekeza tamaa na utajirisho.
Maalim Seif amesema hayo jana huko Darajani mjini hapa baada ya kukamilisha ziara yake ya kuyatembelea masoko ya Mwanakwerekwe na Darajani, kujionea upatikanaji wa bidhaa mbali mbali kutoka kwa wakulima pamoja na bei.
Ziara ya Maalim Seif inatokana kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya kupanda kwa bei za bidhaa katika masoko katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alisema ni kweli kuwa gharama za uendeshaji na upatikanaji wa bidhaa zimepanda, lakini si sahihi kwa wafanyabiashara kuongeza bei za bidhaa hizo maradufu ,wakilenga kujinufaisha.
Alisema dhana iliojengeka miongoni mwao kuwa kipindi hiki ni cha mchumo hakina mantiki kwa kuwa wanawaumiza waislamu, hivyo kukosa fadhila kubwa katika mwezi huu mtukufu.
Aliwataka kuangalia uwezo wa wanunuzi, ambapo wengi wao ni maskini, huku wakilazimika kupata futari sambamba na kukabiliwa na mahitaji makubwa ya chakula na nguo kwa ajili ya sikukuu ya Eid el Fitr siku chache zijazo.
Aidha aliwataka wafanyabiashara hao kuwa makini ili kuondokana na hatari ya kuingiza maradhi mbali mbali wakati wanapoiingiza bidhaa kutoka nje.
Maalim Seif alisema ameridhishwa na uwepo wa bidhaa mbali mbali katika masoko na kuainisha kuwa tatizo liliopo ni viwango vya bei hususan katika mazao ya matunda, samaki na nyama.
Aliwapongeza wafanyabiashara kwa juhudi kubwa wanazozichukua kuhakikisha katika kipindi chote cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kunakuwepo na chakula cha kutosha.
Nao baadhi ya wafanyabaishara waliopata fursa ya kuzungumza, walimweleza Makamu wa kwanza wa Rais, miongoni mwa sababu zinazopelekea kupanda kwa gharama za bidhaa kuwa ni pamoja na kupanda kwa gharama za uendeshaji kutoka kwa wakulima, hatua inayozifanya bidhaa hizo kupatikana kwa bei juu.
Aidha walisema bidhaa hizo pia hupanda wakati ule meli kutoka Pemba inapokuwa haijafika.
Lakini pia kuna waliosema kuwepo kwa utitiri wafanyabiashara nako kunachangia ongezeko la bei za bidhaa hizo katika masoko.
Katika ziara hiyo Maalim Seif aliambatana na Waziri wa Baishara, Viwanda na Masoko Nassor Mazrui, viongozi mbali mbali wa Serikali Mkoa wa Mjini Magharibi pamoja na viongozi wa Manispaa.
No comments:
Post a Comment